KUMBUKA SIKU ZA KWANZA

Na Frank Philip

“Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye” (Waebrania 10: 32-38).

Katika maisha ya imani, kuna mambo mengi ya kusonga sana, na mengine ni mazito, ila kila jambo huja kwa kusudi jema, hata kama kwa SASA huelewi. Mungu ana kusudi jema, na imekupasa kumshukuru Mungu katika kila jambo, na kuomba ili Mungu akuokoe na saa ya kujaribiwa kwako, usishindwe kusimama.

Kumbuka ulivyoanza na BWANA kwa nguvu nyingi na ujasiri mkubwa, na mambo yale uliyojiapia mwenyewe na hadharani kwamba hutafanya kamwe. Je! uvumilivu wako na saburi yako ilienda wapi? Basi kumbuka upendo wako wa kwanza, angalia mahali pale ulipojikwaa, ukatengeneze mapema kabla mambo yako mazuri uliyoyapata kwa BWANA hayajafa yote.

Wengine wameingia mahali pa gumu kwa sababu ya usaliti, au mambo wasiotarajia kwa watu wao wa karibu, naam, sasa wamekata tamaa, mioyo imeinama kwa ajili ya wengine. Kumbuka, angalia sana asije mtu akaitwa taji yako, wala usiipoteze kwa sababu wengine eti, kwa sababu wameamua kurudi nyuma. Kama Lutu na binti zake, kaza mwendo, macho yako yawe mbele kushika maagizo ya BWANA. Okoa nafsi yako, BWANA yu karibu.

Natazama, bado kitambo kidogo, yuaja na mawingu kama alivyoahidi. Hutahuzinika wala kulia milele, siku yaja, hayo nayo yatapita.

Amani ya Kristo iwe nawe tangu sasa na hata milele, AMEN.

Frank Philip.

Comments