KUNA FALME MBILI TU, JE WEWE NI WAUFALME GANI?

Biblia inasema wazi kwamba dunia yote inaongozwa na falme mbili tu: 

1. Ufalme wa Mungu (Ufalme wa Mbinguni) ambao mfalme wake ni Yesu Kristo. Raia wa ufalme huo ni wale wanaomwamini na kuukubali uongozi wake na mamlaka yake. 

2. Kuna ufalme mwingine unaoitwa ufalme wa giza ambao mfalme wake ni Ibilisi, Yule malaika mkuu aliye muasi Mungu. Ibilisi ameifanya dunia ndipo mahali pa utawala wake. Raia wa ufalme huo ni watu wote ambao wameukataa mpango wa wokovu.
Shetani na raia wake ni adui wa Mungu. Shetani anajitahidi kuwafanya wanadamu wawe waovu , wasio mwamini na kumtii Mungu ili wakifa wafe katika dhambi zao, aende nao jehanamu. Silaha yake kubwa ni Dini. 

Hutumia Dini kuwalaghai watu waamini kwamba: 

1. Kuna dini ambayo mwanadamu akijiunga nayo anakubaliwa na Mungu kwa sababu dini hiyo pekee ndiyo dini ya Mwenyezi Mungu. Dini hiyo ni kumpokea YESU KRISTO kama BWANA na mwokozi wa maisha. Kumpokea YESU KRISTO ni zaidi ya dini ni mpango kamili wa uzima kwa wanadamu wote watakaomwamini.

2. Mungu humkubali mwanadamu kwa kuyapima matendo yake mema na matendo yake mabaya.
Kama matendo ni mema mwanadamu huyo atakubaliwa na Mungu.

wanadamu wengi wanaukataa mpango wa Mungu wa kuwaokoa kutoka katika ufalme wa shetani na wanakufa wakiwa watoto wa shetani, wanakufa wakiwa katika dhambi zao.
Biblia inatufundisha kwamba dhambi humtenga mtu na Mungu na kwamba wanadamu wote wametenda dhambi (Isaya 59:2, Warumi 3:23).
Hii inamaana kwamba wanadamu wote, kwakutenda dhambi, hujiunga na ufalme wa shetani.
Biblia inatueleza mpango wa Mungu wa mwenye dhambi kuweza kupokelewa kwenye ufalme wa Mungu. 

Njia hiyo ndiyo njia pekee kwa watu wote: 

1. Wale wanaotubu na kuiamini injili ndio wanaokubali mpango wa kuokolewa na ndio wanao fanyika raia katika ufalme wa Mungu. “Amini, amini nakuambia mtu asipo zaliwa kwa mara ya pili hawezi kuuona…………kuuingia ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3, 5) “Naye alituokoa katika nguvu (ufalme) wa giza akatuamisha na kutuingiza katika ufalme wa pendo la mwana wake( Yesu)” (Wakolosai 1:13). 

2. Wale wanaokataa wanaangamia “Huku akiwalipiza kisasi wao wasio mjua Mungu na wao wasioitii injili ya Bwana wetu Yesu watakao adhibiwa kwa maangamizo ya milele kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake”. (Wakolosai 1:8-9) Mungu anataka watu wote waokolewe kutoka katika ufalme wa shetani. Hataki hata mmoja aangamie. Anataka watu wote wawe katika ufalme wake, 

Swali langu ni hili: JE MUNGU AMESHAKUOKOA KUTOKA KATIKA UFALME WA SHETANI, au umeuamini uongo wa shetani na umeukataa mpango wa Mungu?

Kama unaamua akuokoe leo sema sala hii: 

“Ee, MUNGU nihurumie mimi mwenye dhambi. Natubu mbele zako naomba unisamehe na uniokoe kutoka katika ufalme wa shetani na unihamishe na kuniingiza katika ufalme wa Mwana wako YESU KRISTO, BWANA YESU futa jina langu kwenye kitabu cha hukumu na liandike leo kwenye kitabu cha uzima, kuanzia leo mimi ni wako BWANA YESU. Naufunga ukurasa wa dhambi kuanzia leo na nafungulia mlango wa utakatifu pamoja na kuliishi neno lako. Asante BWANA YESU kwa kuniokoa. Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba. Amen.” 

Kama umesema sala hii kwa kumaanisha; MUNGU amekusamehe na kukuokoa. Jiunge na kanisa la watu waliookoka.


UBARIKIWE SANA .

Comments