KUOKOLEWA KATIKA VITA AU SHIDA YAKO KUTOKEA NDANI (THE RESCUE FROM INSIDE)

Na Frank Philip


Kama kuna faida kubwa unaweza kuipata, ni kujua unachotarajia kwa baba yako mzazi, kabla hujapata uhitaji. Kwa lugha nyingine, ukijua jinsi baba yako atashughulika na shida yako, utakuwa na amani hata usikiapo shida inakuja.

Sasa nisikilize, Mungu ni Baba yetu. Kadri unavyokaa katika UHUSIANO mzuri, na wa karibu Naye, kuna TABIA za Baba, ambazo ukizijua, utakuwa na AMANI hata TUFANI zivumapo. Kuna mambo mengi nimejifunza kwa habari ya Baba yangu, na sasa nakupa hii moja. Baba huokoa watoto wake kutokea ndani, yaani kutokea katika mazingira waliyopo na kuwatumia wao wenyewe. Nitakupa mifano. BABA aliposikia kilio cha watu wake, Israel, kule Misri, Alishuka KUWAKOMBOA, ila alitafuta mtu katikati yao kuifanya hiyo kazi. Najaribu kujiuliza, kwanini Mungu hakutafuta JESHI lenye magari ya vita, na silaha kali kuliko za Farao, ila aliinua mtu mmoja kati ya WATUMWA, ili kuwakomboa watumwa wenzake?

Nitakupa mfano mwingine. Wana wa Isarael walipovuka kuelekea Kaanani, walipambana na maadui wengi njiani. Iliwapasa wajifunze VITA kwa KUPIGANA vita, na ukombozi wao kwa adui zao WALIUTWAA wao wenyewe! Ona hapa, walipofika nchi ya Kaanani, BABA hakumaliza maadui wote kwa kupitia MASHUJAA wa vita ambao alijipatia katika vita zilizotangulia; BABA aliacha maadui kidogo, ili hao vijana wadogo ambao hawajui vita, wajifunze kupigana vita kwa kwenda vitani, sio kwa kusimuliwa tu habari za vita ambazo wenzao walipigana! (Waamuzi 3:1-3)

Angalia mfano mwingine. Akina Shedrak, Meshak na Abedinego, walipokuwa wanatishiwa maisha na mfalme Nebkadreza, na watu wake, Mungu alikuwepo, ila ALIKAA KIMYA! Hakutuma jeshi, au mtu kutoka nje kuwapigania, wokovu wa vijana hawa watatu ulianzia katikati yao, na ndipo BABA akasema, nitatangulia katika moto ili kuwaokoa! BABA ALIFANYA ukombozi kutokea ndani ya tanuru la moto! Hali kadhalika, Danieli hakutahayari alipojua sasa anatupwa katika tundu la simba; Baba alingoja kule ndani ya tundu, hakuleta watu kutoka nje, watu wenye hekima na ushawishi mkubwa kuja kumsihi mfalme na kuomba msamaha kwa ajili ya Danieli, BABA alifanya ukombozi kutokea ndani ya tundu la simba! Na Mungu akajitukuza kati ya watu wote.

Nikajiuliza tena, kama Mungu anaona mahali pa boma palipobomoka, kwanini asitume malaika walio hodari katika kutenda mambo mengi, hadi atafute mtu MIONGONI mwa hao hao watu, ili asimame hapo mahali pa boma palipobomoka, ili nchi isiangamie! Je! Kwanini asitume nabii kutokea mbali, mtu mkamilifu aje kuokoa taifa lisiangamie hadi atokee mtu ndani ya taifa/mahali husika?

Ukisoma kitabu cha Waamuzi utaona jambo hili kwa upana zaidi. Kila wana wa Israel walipofika mahali pa gumu, mateso na vita, Mungu aliinua mtu katikati yao, ili kufanya UKOMBOZI. Hebu tufikiri habari za BWANA Yesu kidogo. Ilimpasa azaliwe kama mtu, na kupigana vita akiwa huku upande wetu kama mtu, akaleta UKOMBOZI akiwa katikati yetu. Alikula nasi, na kukaa katikati yetu. Wala hakuita majeshi ya Mbinguni (mamuluki kutoka Mbinguni), kuja kupigana na adui zake huku chini. Alikesha akiomba milimani, alifunga na kupambana katika ulimwengu wa roho kama mimi na wewe! Ilimpasa kutwaa UKOMBOZI, ila kutokea alipo, duniani na sio nje.

Angalia hali zako unazopita, kweli kuna vita na mambo mengi ya kutisha mbele yako. Ndoa yako, shule yako, watoto wako, kazini kwako, nk., ni ngumu. Kila ukiangalia pande zote unaona vita au dalili za vita. Nakupa habari hii leo, Mungu anaangalia mtu katikati yako atakayesimama kuleta UKOMBOZI katika hiyo vita. Ukisubiri MAMULUKI waje wakupiganie vita zako KILA SIKU tu, jua sio utaratibu wa kawaida sana katika taratibu za Baba yetu. Sawa Anaweza kuinuliwa mtu kuja kusaidi shida yako, jua huo ni msaada kama “huduma ya kwanza tu”, imekupasa kusimama na kupigana vita vyako vya imani, na ukiisha kupigana, usimame.

Jifunze jambo hili, hutajifunza VITA kwa kusimuliwa; utajifunza vita kwa kupigana vita HALISI, na hii ndio maana ya IMANI kwa matendo. Mchungaji wako, walimu na wahubiri mbalimbali watakufundisha Neno, ila ujue wewe utalitenda hilo Neno kwa VITENDO. Darasa haliishii kwenye kusikia maandiko tu, ila kwenye matendo, hapo ndipo utasema unamwamini Mungu.

Frank Philip.

Comments