MASHUJAA WA ISRAELI

Na Frank Philip


“Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa” (2 Samweli 14-17).

Nimesoma habari za mashujaa wengi wa Israel, watu wa vita, waliopigana vita mbele za BWANA kwa UADILIFU na UAMINIFU mkubwa. Nimeona habari za Uria Mhiti, na Yoabu mwana wa Seruya, nami nimejifunza jambo la kushangaza. Hebu fikiri ni watu wangapi ambao wanaweza kubeba ujumbe wa mtu mwingine na wakautunza bila kutaka kujua kilichandikwa? Hii unaweza kusema ni rahisi, angalia kwa kona hii, je! Ni watu wangapi ambao wanaweza kubeba habari za watu wengine, hasa MBAYA, na wakazitunza bila KUWASEMA hao watu? Uria Mhiti alibeba habari yake mwenyewe, tena mbaya ila hakujua! Akafa akiwa mwaminifu mbele za BWANA.

Kuna namna ya watu kusengenyana, kutetana, kupeleka majungu na umbea, kwa jina la USHUHUDA au jambo la KUOMBEA (prayer point). Kweli kuna wakati Mungu ataruhusu shuhuda fulani za mambo yaliyopita katikati ya watu kusemwa kwa namna ya KUMWINUA Mungu, lakini na kwambia, kuna watu WENGI wanasema MAMBO ya WATU wengine kama UMBEA tu, na wala si kwa ajili ya BWANA. Hebu fikiri tu, “hiyo” habari UNAYOTANGAZA , ingekuwa wewe, je! Ungesimama madhabahuni na KUTANGAZA? Ukiona kwamba huwezi KUSEMA kwa sababu ni wewe, basi ujue sio sahihi kuisema kwa sababu ni ya mwingine.

Fikiri Yoabu anaagizwa na Mfalme habari ya kumpeleka mtu wake wa karibu, Uria Mhiti, jemadari mwenzake, ili akafe! Lakini Yoabu anabeba ujumbe huo MZITO bila kusema jambo lolote kwa Uria! Na Uria akiisha kufa, Yoabu anabaki mwaminifu, mwadilifu na mtiifu kwa KIONGOZI wake, anarudisha taarifa, bila KUHUKUMU (2 Samweli 11:18-25). Sasa angalia hapa, “itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani?” (2 Samweli 11:20). Najiuliza tu, kwanini akina Uria na wenzake, walitii AMRI ya kamanda wao Yoabu, na kusonga mbele, huku wanajua kwamba watakufa? Mashujaa hawa wa Israel walijifunza KUTII hata kama itawagharimu maisha yao!

Angalia tulivyo leo, kila siku tunamwita Yesu BWANA wa vita; je! Tunamtii kama ipasavyo? Ni mara ngapi tunabishana na BWANA, na kujichagulia mambo yetu wenyewe tukidhani “tutakuwa salama?” Je! BWANA hakusema “mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili Yangu ataiona”? Je! Yeye mwenyewe hakuonesha mfano wa KUTII, naam, hata MAUTI ya msalaba, na akiisha kumaliza, akakirimiwa JINA lipitalo majina yote? Jina lake aliitwa “Mwana wa Daudi”, kuna jambo la zaidi la kujifunza. Huu utii ambao unauona kwa mashujaa wa Israel, ulikuwepo kwa kiongozi wao Daudi mwana wa Yese, naam, Daudi naye amekirimiwa jina pia, ndio maana Mungu ameimarisha ufalme wake hata milele. Hebu fikiri Jina la Yesu likitajwa, linatajwa pamoja na jina la Daudi! “Utasikia simba wa kabila la Yuda (kabila la Daudi)”, “Yesu mwana wa Daudi nirehemu”, nk., watu walimtambulisha BWANA kwa kupitia JEMADARI huyu mwaminifu, SHUJAA wa ISRAEL, ambaye nyuma yake kulikuwa na majemadari wengine waliofuata nyayo zake sawa sawa, akina Uria Mhiti, Yoabu na wengine “wachache”.

Ndipo mtume Paulo akasema, “nifuateni mimi, kama nimfuatavyo Kristo”. Umeona mfano huu? Je! Tuna ujasiri wa kumfuata Kristo kwa namna ambayo TUNAJUA kwamba watu wakitufuata sisi watakuwa salama? Jiulize mwenyewe njia zako, kama kweli unamfuata BWANA wa majeshi, na unachukua AMRI zake bila KUJIJALI (yaani kujikana). Bwana alisema mapema kabisa, “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona” (Mathayo 10:37-39).

Neema na Amani ya Kristo, viwe kwenu tangu sana na hata milele. AMEN.

Frank Philip.

Comments