MAZINGIRA MAZURI YA KUKULIA KIROHO

Na Frank Philip.



“Hivyo dhambi yao wale vijana (watoto wa Eli) ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA. Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani.” (1 Samweli 2:17,18).

Nimesikia watu wengi wakilalamika, eti, wamerudi nyuma/anguka dhambini/kumwacha Yesu, kwa sababu ya “mazingira” yao ya kazini, nyumbani, shuleni, mtaani, ndoa zao, nk. Wengine wamesema “nikihama MAHALI hapa, na kukaa mbali na “hawa watu”, nitasimama na wala sitatenda dhambi tena”. Nakubali, kweli kuna mazingira magumu ambayo ukiyatazama kwa MACHO ya DAMU na NYAMA, HAKIKA utasema “hapa hawezi kusimama mtu”. Ngoja nikupe habari mpya leo, watu wengi sana waliosimama, na kukua vizuri kiroho (yaani kukua katika kumjua Mungu), hawakupita mazingira marahisi tu. Ukisubiri Mungu akuhamishe (akutoe darasani), ili ndio ufaulu mitihani yako, jua wewe sio mwanafunzi! Wanafunzi hukaa shuleni, na kufanya mitihani shuleni, tena hawachagui mtihani, ila mwalimu ndiye ajuaye mtihani (na mazingira yafaayo), kisha ukifaulu, utahamishwa kwenda KWINGINE, sio kurahisi, ila kama unataka kuongezeka katika kumjua Mungu, utaenda KIDATO cha juu ambacho masomo yake na mitihani yake ni migumu zaidi.

Sikiliza, hakuna mahali pagumu umepita, ambapo hawajapita wenzako wengi tu, na wakasimama bila kumtenda Mungu dhambi; wamevuka kwa ushindi, na watu wakajua kwamba yuko Mungu katikati yao. Sitaki kurudia habari za akina Yusufu, mfalme Daudi, Danieli, Shadrak, Meshak, Abdnego, Nabii Jeremia, na wengine wengi. Kuna MAZINGIRA ambayo ukiyaangalia, utajiuliza ni kwanini Mungu aliwapitisha watu huko? Ona jinsi Mtume Paulo, na usomi wake wote, na vyeo vyake vyote, na ujuzi wake wote, na UPAKO wake wote, na heshima yake yote, anachapwa viboko tu hadharani, anapigwa tu na kuvurugwa huku na kule, anapatwa na majanga mengi hata kufikia mahali pa kukata tamaa ya kuishi. Najiuliza tu, hivi, mbona sikuhizi ni “tai na suti” tuu ndio baraka? Je! Mungu wa akina Petro (aliyesulubiwa kichwa chini miguu juu), Stefano (aliyepigwa nawe hadi kufa), bado ni Mungu wetu ambaye TUKIFANIKIWA ndio tunashangilia na kushuhudia mafanikio, TUKIBANWA kidogo tu tunageuka na kumwacha Mungu kwa haraka? Je! Bado kosa la “kuuza HAKI ya mzaliwa wa kwanza” kwa mlo wa siku moja (chakula/mshahara/kipato), bado litaendelea tu hadi lini? Je! Imani yetu kwa BWANA inategemea MAFANIKIO tu, kwamba tusipofanikiwa tunarudi nyuma?

Nataka nikuoneshe MAZINGIRA aliyokulia nabii Samweli, kisha tujifunze jambo hapo. “Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri (1 Samweli 3:1). Samweli akakua, naye BWANA alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini. Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA. Naye BWANA akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.” (1 Samweli 3:19-21).

Ona jambo hili, Samweli alipelekwa HEKALUNI akiwa mtoto mdogo sana, tunaambiwa alikuwa akilala hekaluni (1 Samweli 3:3). Mazingira ya hekaluni YALIPASWA kuwa matakatifu, lakini watoto wa Eli walifanya machukizo mengi mbele za BWANA, ikiwemo na kuzini na wanawake waliokuja kutoa sadaka hekaluni. Samweli aliona kwa macho, sio kusikia tu. Mazingira yalikuwa ni ya dhambi kila upande, LAKINI Samweli aliamua KUMHESHIMU Mungu. Hakutenda kama WENZAKE waliokuwa hekaluni, aliishi maisha ya KUTENGWA japo alikaa na kuishi katikati yao.

Ona tena hapa “Samweli akakua, naye BWANA alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.” Ukisikia mtu anasema “kila mtu anafanya hivi, na mimi nimefanya kama wao”, au “maisha ni magumu sana mjini, we ulidhani mimi nitaishije?”, “usipofanya ujanja huu (dhambi hii) kweli nakuapia hutoki”, “bila kuongea na watu vizuri (i.e. kukubaliana na uchafu wao), huwezi kufanikiwa”, nk., mtu wa namna hii bado hajamjua Mungu wa Israel. Lini utamwona BWANA akikuvusha mahali pa gumu, nawe ukavumilia na kupita salama, hata siku moja usimame na kushuhudia matendo makuu ya BWANA? Je! Umesahau Paulo alisema juu ya “kushindana kwa HALALI”? (2 Timotheo 2:5) kweli umeshindana, umepanda cheo, umepata gari/pesa/mafanikio, nk. Sawa, je! Umeshindana kwa halali? Je! Ukitizama njia zako una ujasiri wa kusema ni BWANA alinivusha?

Angalia vyema mazingira yako. Kuna misimu ya kupanda na kushuka, je! Unampendeza Mungu katika mazingira na misimu yote? Jua jambo hili, misimu na tofauti za siku na siku zimewekwa ili UJIFUNZE kumtafuta Mungu, na kumwona, naam, ukimtafuta kwa bidii, hata kama ni kwa kupapasa papasa, utamwona kwa maana hayuko mbali na ulipo.

Neema ya BWANA na UPENDO wake mkuu uwe nawe tangu sana na hata milele.

Frank Philip.

Comments