MWACHE MUNGU WAKO AJITETEE NA KUJIJULISHA MWENYEWE KUWA HAKUNA MUNGU MWINGINE KAMA YEYE


Bwana Yesu Asifiwe Wateule wa Bwana!
Ni mara nyingi tumeona malumbano ya kidini hapa duniani katika nchi, na jamaa, na dini mbalimbali. Kila dini inataka Mungu wake ndiwe awe Mungu anayeheshimiwa na kila mwanadamu – jambo ambalo toka zamani hadi leo limekuwa gumu kutekelezeka. Vita kadhaa hapa duniani vimeanza kwa sababu ya malumbano ya kidini. Tena machafuko mbalimbali katika nchi nyingi duniani yameanzishwa na malumbano ya kidini katika nchi hizo.
Na Nyandula Mwaijande.
Nabii Eliya aliwahi kufanya kosa la kutaka kuanzisha malumbano ya kidini na manabii wa baali, lakini manabii hao wa Baali walikataa kuingia kwenye mtego huo. 1Wafalme 18:21 imeandikwa “Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? BWANA akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Biblia inasema “wale watu hawakumjibu neno”. Hii ikiwa ina maana ya kuwa hao watu walikataa kuingia katika malumbano ya kidini, au malumbano juu ya nani anafaa kati ya Mungu wa Eliya na yule mungu wao! Mara naye Nabii Eliya akatambua ya kuwa, aliokuwa anatofautiana nao kiimani, walikuwa hawako tayari kuingia katika malumbano ya kidini, juu ya Mungu yupi ndiye aliyefaa kufuatwa na watu.
Ndipo Nabii Eliya akaja na pendekezo la pili ili kutafuta kumaliza ushindani huo. Pendekezo hili lilikuwa ni kuhusu pande zote mbili kutoa sadaka, na kila upande uombe kwa Mungu wake imeandikwa katika 1Wafalme 18:24 “Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri”. Watu walionyesha wazi ya kuwa badala ya kulumbana na kubishana juu ya nani na ni yupi Mungu aliyefaa, ni bora zaidi kutafuta ufumbuzi wa jambo hili kwa njia ya maombi! Ukiona malumbano ya kidini yameibuka na kupamba moto katika eneo fulani, ujue hiyo ni ishara ya maombi kutokuwepo katika eneo hilo; na kama maombi yapo basi ni maombi kidogo kiasi ambacho hayana uwezo wa kutoa maamuzi katika ulimwengu wa roho ili Mungu wa Eliya atawale! Manabii wa baali waliomba kuanzia asubuhi hadi jioni, lakini mungu wao hakujibu chochote! Nabii Eliya aliomba kwa Mungu wake, naye akajibu kwa moto machoni pa kila mtu! Na ubishi wa kidini ukakoma! Malumbano ya kidini yakakoma! Malumbano ya kidini yakaisha!
Ndugu zangu ni ushauri wangu kwa kila mmoja wetu badala ya kulumbana kidini ni bora kufanya maombi na Mungu wa kweli atajitetea na kujijulisha mwenyewe! Hatupaswi kulumbana kwa maneno na hata kwa vitendo hata kidogo maana hapo tutakuwa tunakwenda kinyume na Neno la Mungu! Tuangalie sana tusiingie kwenye mitego ya vita ya maneno ya kidini maana mwisho wake ni ugomvi na chuki vitainuka. Kukaa kimya ni hekima mno kuliko kulumbana juu ya Mungu wa dini ipi ni bora.
ANGALIZO: Kundi hili halifungamani na dini au dhehebu lolote bali tuko hapa kwa ajili ya kujifunza Neno la Mungu maana hiyo ndiyo kweli ambayo itatuweka huru hivyo isingefaa kabisa mwanakikundi yeyote kupost mafundisho ambayo yanakashifu dini nyingine au dhehebu lingine, ukiona kwamba huwezi kabisa kutokupost mafundisho ya aina hiyo ni bora ukajitoa mwenyewe na kutafuta mahali ambapo wanaruhusu mafundisho ya aina hiyo. Ukishindwa kujitoa ukaendelea kupost mafundisho ya aina hiyo itabidi nikutoe ili wale wenye hamu ya kumtafuta Mungu wasije wakashindwa uvumilivu na kujitoa wakati mahali hapa panawasaidia. Tuko mahali hapa lengo letu likiwa ni kula (Neno la Mungu) na kukua kiroho na si kuingia katika malumbano ya dini ama madhehebu hivyo ni vema ukapost mafundisho ambayo yatatusaidia katika safari yetu ya imani na kupelekea kumaliza mwendo salama.
Naomba niwape habari hii ambayo ilinitokea mimi mwenyewe katika makundi ambayo nilikuwepo huku facebook. Kipindi cha nyuma nilikuwa kwenye makundi mawili tofauti ambayo yalikuwa yanafundisha neno la Mungu! Lengo langu katika hayo makundi lilikuwa ni kupata mafundisho ili niweze kudumu na kukua katika maisha ya kiroho lakini nikawa kila nikiingia katika hayo makundi post nyingi zilikuwa ni malumbano ya kidini ama madhehebu niliamua kuvumilia japo ile hali sikuipenda kabisa lakini mambo ndo yalipamba moto maana ilifika wakati hata comments zilibadilika zikawa za kukashifu dini nyingine na hata kugombea madhehebu! Kuna siku nikajiuliza sana kwamba nimeingia katika haya makundi kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu lakini mambo yamekuwa tofauti badala ya kujifunza neno la Mungu nimeishia kuumizwa na kile kinachoendelea. Na kwa sababu nilikuwa mchanga kiroho sikuweza kusimama vizuri kwenye zamu yangu kwa maombi ili kubadilisha ile hali ikabidi tu nijitoe ili niweze kuendelea kuwa na amani na kumtafuta Mungu kupitia makundi mengine! Kadiri siku zilivyozidi kwenda ndipo nikajifunza kwamba kutokusimama imara kwenye maombi kunaweza kufanya malumbano mahali fulani. Hivyo nitoe changamoto ukiwa mmojawapo wa wanafamilia wa kundi hili weka nia ya kuomba kwa ajili ya kundi hili ili Mungu wako ajitukuze mahali hapa na si kuingia katika malumbano ambayo yatapelekea kuharibika kabisa lengo la kuanzishwa kundi hili. Popote ulipo kwa ajili ya kumtafuta Mungu weka bidii na nidhamu ya maombi Mungu wako atajitetea na kujijulisha yeye mwenyewe kwamba hakuna Mungu kama yeye. Heshima ya Mungu wako katika eneo ulilopo inategemea maombi yako!
Mungu awabariki sana kila mmoja na jina lake.
By Nyandula Mwaijande.

Comments