MWILI KAMA SADAKA

Na Frank Philip


“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu” (Warumi 12:1,2).

Sikujua maana halisi ya sadaka, hadi nilipotafakari habari ya yule mama mjane aliyetoa “nusu pesa” kwenye sanduku la hazina, halafu BWANA akasema “huyu mama ametoa sadaka kubwa kuliko ya wale matajiri waliotoa pesa nyingi zaidi” (Marko 12:41-44). Nilizidi kushangaa maana ya sadaka nilipotazama jinsi Mungu alivyoitakabali sadaka ya Habili na kuikataa ya Kaini! Wote wawili walitoa sadaka, Habili alitoa VINONO vya wazaliwa wa KWANZA, ila Kaini alitoa BAADHI ya mazao ya nchi (Mwanzo 4:1-16). Wakati huo wote, kwa Habili na Kaini (Agano la Kale), na kwa yule mwanamke mjane (Agano Jipya), watoaji wa sadaka walitoa kimya, ila Mungu alisoma taarifa ya sadaka zao mioyoni mwao! Ndipo wingi au ukubwa haukuwa kitu, ila nafsi/moyo utoao.

Angalia hapa, Paulo anasema “tutoe miili yetu kama sadaka takatifu, iliyo hai ya kumpendeza Mungu”, na akasema KUSUDI lake, “ndiyo ibada yenu yenye maana”. Kwa hiyo, sadaka ni sehemu ya ibada. Unapotoa mwili wako mahali, au KUUZUIA kuutoa mahali, hapo kuna mawili, umempendeza Mungu au Ibilisi, hakuna free ground! Uchaguzi ni kati ya mambo mawili: kwa Mungu au kwa Ibilisi, Joshua anasema, leo yamewekwa mambo mawili mbele yenu…, kisha yeye akasema “mimi na nyumba yangu nitamtumikia BWANA”. Sehemu nyingine, Paulo anauita mwili “hekalu takatifu”, yaani mahali pa ibada au Mungu alipo (2 Wakorinto 6:14-16), huku akisisitiza kukaa mbali na uovu.

Nilipotafakari habari ya KUTOA, nikaona kwamba kuzuia nako kwaweza kuwa kutoa! Yaani unauzuia mwili wako, kufanya jambo fulani (wanaita kutiisha mwili), kumbe bado maana yake ni ile ile, ni kuutoa huo mwili kwa BWANA, kwa kukataa kufanyika SADAKA kwa Ibilisi kwa kutenda uovu! Na Paulo anasema hiyo ni ibada! Sasa kama unatoa mwili wako kwa uasherati/uzinzi, ufisadi, nk., je! Unamtolea nani sadaka wakati huo? Je! Unamwabudu nani saa hiyo?

Nilipotazama mwili, nikaona jambo hili, nalo ni gumu. Maumivu na mateso katika mwili imekuwa mtego wa wengi. Utasikia mtu anasema “nimevumilia kweli hata Mungu anajua”, “mpendwa mwili ni dhaifu, japo roho iradhi”, nk. Je! hatukuitwa KUPIGA vita vya imani kwa mfano wa Paulo? Kwa upande mwingine, nimeona AIBU kuwa kwazo la kuangusha, mtu akiona “aibu mbele za wanadamu”, nakujikuta akiachia mwili wake kuwa sadaka za ibilisi! Mungu akamwambia Sauli, “umewaheshimu hawa watu kuliko mimi”, ufalme wake ukararuliwa. Sasa, ukiangalia habari ya Sauli, BWANA anasema “kutii ni bora kuliko dhabihu..”, yaani vile vitu tuvitoavyo, miili yetu ni dhabihu bora zaidi. Sauli, alijitahidi kumkusanyia BWANA sadaka, ila alishindwa KUJITOA yeye kuwa sadaka kwa kumtii Mungu! Akaona aibu mbele za watu, akafanya yasiyostahili, BWANA akamkataa asiwe mfalme juu ya watu wake.

BWANA Yesu akiliona jambo hili kuwa nyeti, akasema, “mtu akimwonea AIBU yeye na NENO lake mbele za WANADAMU, na yeye atamwonea aibu mtu huyo mbele ya BABA yake na malaika watakatifu”. Mwili hupiga kelele, huhitaji huruma na kusikilizwa, kumbe! Unaishia mavumbini tu!

Frank Philip.

Comments