NJIA YA KUKWEA

Na Frank Philip


Hakuna afikaye JUU bila KUPANDA/KUKWEA. Walio JUU wanajua kwa uzoefu (experience) MAUMIVU ya kupanda, hasa kama mlima ni MREFU. Kwa uzoefu huo, tunajifunza kwamba MUDA wa kupanda unavyokuwa MREFU, ni dalili tu kwamba KIMO cha KUPANDA ni kikubwa, “ILA” KAMA ukidumu katika NJIA halali za BWANA, bila kupoteza mwelekeo. Kumbuka, Wana wa Israel walitembea JANGWANI miaka 40, kumbe! Ilihitajika siku 3 tu kumaliza safari yao, sababu ya msingi ni KUTOMSIKIA Mungu, na KUMKASIRISHA katika safari yao. Basi najifunza tena jambo hili, sio kila wakati UREFU wa muda wa KUKWEA utakupelekea kufikilia KIMO cha juu zaidi; ila UKIISIKIA sauti ya BWANA Mungu wako, na kutenda yote akuagizayo, japo upo katika KUKWEA au NYIKANI, hakika kuna mahali PAZURI unakwenda, USIKATE TAMAA.

Ajapo kuwa kipenzi cha Mungu, Daudi hakufika KILELENI kwa kupaa, ilimpasa KUKWEA na kuishi NYIKANI, tena kwa muda mrefu sana. Hakujua kwamba urefu wa MUDA wa kukwea kwake ni UMBALI wa mahali Mungu alitaka afike! Aliona sasa kinachofuata ni kifo, wakati Mungu anaona kinachofuata ni kiti cha enzi! Akiwa kijana mdogo tu, Daudi alianza vita na wanayama wakali, kisha ikafuata vita kali zaidi akiwindwa na Jeshi la nchi, na mfalme wake Sauli! Haikuwa safari ya mwaka mmoja au miwili, ila miongo, akikwea tu. Katika njia zake, Daudi alizidi kumpendeza Mungu. Kumbuka, KIPIMO cha JANGWANI au katika MWINUKO hakidanganyi. Huwezi kuigiza umeshiba kwenye njaa na kiu, na usipokuwa na NIDHAMU ya kweli, huponi. Hapo ndipo UAMINIFU wako unapopimwa vizuri.

Ilimchukua Yusufu miaka mingi KUKWEA hadi nafasi ya juu sana, mtu wa pili katika ufalme wa nchi. Hakukaa mwaka mmoja tu kama kijakazi (house boy) kwa Potifa, na hakukaa mwaka mmoja kama mfungwa gerezani; ilimchukua MUDA mrefu wa KUPIMWA sana na KUSAFISHWA sana, ili afikilie KIMO cha juu zaidi.

Kama unataka kufika MBALI, jua kuna MAHALI utapita na sio mteremko. Uonapo NYIKA inakukabili au KILIMA kinakukabili, bila shaka jua unapanda kuelekea hatua zingine za JUU. Kaa sawa-sawa, ukijua VIPIMO vya nyikani na mlimani ndivyo vitakupa alama nzuri zaidi za ushindi.

Frank Philip.

Comments