ROHO NYUMA YA MAFANIKIO YAKO – II

Na Frank Philip.

“Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake” (1 Samweli 23:14).

“Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo” (Kumbukumbu la Torati 8:12-17).

Somo lililotangulia tuliona siri iliyoko katika KUTENGWA wakati Mungu anakupitisha katika mafunzo na michakato mbalimbali ya kukuandaa kupokea nafasi kubwa, na za juu katika maisha yako. Sehemu ya pili ya somo hili, nitakuonesha NJIA au MAHALI pa zuri ambamo Mungu huweka darasa lake la kufundisha watu wake mambo mazuri. Hili darasa nimeliita “darasa nyikani”.

Nyikani au kwa lugha nyingine, jangwani, ni mahali pa kupungukiwa. Ni mahali pasipo na chakula kizuri, cha kutosha na hakuna maji ya kutosha. Makazi na hali za jangwani ni magumu kwa sababu ya ari na vurugu nyingi, lakini hapo ndipo ambapo Mungu amechagua kufundisha watu wake masomo mazuri (the best lessons are learnt in the desert).

Kuna hali za kimaisha ambazo mimi nimeamua kuziita nyika/jangwa. Unapopita katika vipindi vigumu, na misukusuko, hapo napafananisha na nyikani/jangwani. Kumbuka, kusudi la Mungu sio UKAE jangwani, ila UPITE jangwani. Usisahau, jangwani ni njia tu, kama umejenga, hilo litakuwa ni hema, kwa maana sio mahali pa kudumu.

Kila nikifikiri safari ya wana wa Israel kutoka Misri (utumwani) kwenda Kaanani (nchi iliyojaa asali na maziwa), najikuta napata somo jipya. Hebu fikiri walisafiri Nyikani/Jangwani kwa miaka 40, kumbe! Ki kawaida ilipaswa kuwa ni safari ya siku 3 tu! Hapo naona MUDA (mrefu) na NJIA (ngumu). Kumbuka, Mungu alikuwa na wana wa Isarel muda wote, lakini na Ibilisi alikuwepo pia! Pamoja na kwamba watu waliona nguzo ya wingu, na nguzo ya moto, kwa macho ya damu na Nyama, uwepo wa Mungu haukuwa wa kutafuta, ulikuwepo tu, BADO shida na adha za jangwani zilijitokeza kwa namna mbali mbali. Kumbe! Mungu alikuwa anawafundisha mambo, wengi hawakuelewa. Wengi sana waliangalia MATESO na SHIDA za jangwani, hata wakakumbuka starehe za MISRI badala ya KUMJUA Mungu wao sana katika MAPITO yao! Wakanung’unika, na kufarakana wao kwa wao, na kumlalamikia Mungu wakitaka KURUDI NYUMA (Misri/utumwani). Wengi sana waliangamia njiani, na wachache walipona.

Kama lengo ni kwenda Kanaani, kwanini Mungu hakuwapitisha njia ya mkato wafike haraka? Angalia hapa, lengo sio KUFIKA tu, lengo ni KUMJUA Mungu KABLA ya kufika. Ndio maana BWANA alisema, “JAMBO la KWANZA sikuwaambia mtoe sadaka (KUNITUMIKIA), ila MSIKILIZE SAUTI YANGU”, kwa sababu walikuwa DARASANI. Kwa mfano, hebu fikiri Mungu analeta nyoka za moto, watu wanang’atwa (gongwa), wanakufa huku na kule, halafu Mungu anasema “Musa, tengeneza nyoka wa shaba na mtundike mtini, kila aliyeng’atwa akimtizama atapona”. Angalia darasa la UTII hapo, hapo ni nyikani! Usipoweza kujifunza kwa sauti za mitume na manabii, kisha kutii sauti yao katika njia zako za kupanda, Mungu ataleta nyoka za moto (hali ya kukuvuruga), na usiposikia tena, na ukapata maarifa, ile hali inaweza kukuangamiza.

Unajua, kuna mazingira ambayo jaribu fulani likija, linakuwa sio jaribu; lakini jambo lile lile likija katika mazingira mengine (nyikani) kwa mtu yule yule, linakuwa jaribu. Kwa mfano, fikiri mtu ameolewa, yuko na mume wake, wanapatana vizuri tu na kila akigeuka huku, mume wake huyu hapa. Kila anachotaka anapata, halafu anatokeza jamaa anamjaribu huyu mama kutenda dhambi ya uzinzi. Sasa, hilo sio jaribu kwa huyu mama, kwa maana kwanza hayuko nyikani; na AKIANGUKA katika uzinzi, kila mtu atamwona ni mjinga kuliko wanawake wote. Akishinda jaribu hilo, pia asijisifu sana kwamba anamjua Mungu, hadi ashinde jaribu hilo hilo akiwa nyikani (yaani, kwa mfano kuna ugomvi mzito ndani ya ndoa, mambo hayaendi kila kona, hakuna pesa wala mahitaji yake ya muhimu, nk).

Nitakupa mfano mwingine. Fikiri mtu anakuja kuomba shilingi laki moja, wakati una milioni kumi mfukoni, na hazina kazi maalumu. Ukimpa, usijisifu kwamba wewe sio MCHOYO. Subiri wakati una shilingi elifu kumi tu, halafu mtu anakuomba shilingi elifu mbili; uone jinsi ambavyo hujawahi kuona elfu mbili kwamba ni kubwa sana.

Angalia jambo hili, wakati Daudi anatishiwa maisha, yeye mwenyewe hana amani, yeye mwenyewe ana uhitaji hata wa kipande cha mkate tu, hapo ndipo alipoita watu wenye shida na mahitaji akae nao; sio ikulu, No! aliwaita akae nao huko nyikani; Huko mapangoni alikokuwa anakimbia adui zake. Ona hapa mwenyewe, “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne” (1 Samweli 22:1,2).

Ukiangalia kwa upande wa pili, Sauli yeye lipoenda kupigana vita, kila alipoona mtu hodari alijikusanyia kwake. Kila mtu shujaa na mwenye uwezo mkubwa, hao ndio Sauli aliwatafuta ili wamzunguke (1 Samweli 14:52). Je! Umeona jambo hili katikati ya waaminio pia? Kwamba akaribishwaye ni yule aliye na kitu mkononi? Iwapi nafasi ya yatima, wajane na masikini katikati ya makusanyiko ya BWANA au huko mitaani tuishipo? Je! Umesahau BWANA alichosema tutakapo kukaribisha watu karamuni? Kwamba tutafute watu ambao hawawezi kutulipa wema au yale tuwatendeayo!

Je! Utasubiri ufike “ikulu” ndio utende mema? Bila shaka kuna tofauti ya THAMANI ya wema uliotenda katika vipindi vyako vya NYIKANI (japo ni kidogo), na wema uliotenda wakati wa kuwa na ZIADA. Ukitaka kujua nasema nini, kumbuka yule mama mjane aliyetoa “nusu pesa” na kuweka kwenye sanduku la hazina, mbele za BWANA hekaluni (Marko 12:41-44). Matajiri walitoa pesa nyingi ila yenye THAMANI kidogo kulinganisha na “pesa kidogo” ya huyu mama yenye THAMANI kubwa. Kumbe! Thamani ya sadaka yako sio thamani ya pesa/kitu! Ndio, thamani inapimwa kulingana na NYIKA unayopita. Huyu mama mjane alikuwa NYIKANI! Sasa basi, ukisubiri ufike “ikulu” (nchi ijaayo maziwa na asali), ndipo utoe sadaka zako, au ufanye wema, jua unakosa kutoa vitu vya thamani sana, hata kama ni vichache. Jifunze KUJUA vipindi vya kupita nyikani, na ufanye yakupasayo bila kuangalia adha za nyikani.

Basi wapendwa wangu, tazameni sana njia zenu, mkijua kwamba yupo BWANA ajuaye mapito yenu, taabu yenu ni ya kitambo tu, akiisha kuwajaribu na kujua mnampenda na kumtegemea yeye, na kushika amri zake, Atawainua bila shaka.

Kumbuka siku zote, hata kama uko jangwani, hiyo haimaanishi uko chini ya laana, wewe ni umebarikiwa tayari, jangwani ni mahali tu ambapo kuna darasa, au njia kukufundisha mambo muhimu upate kumjua BWANA Mungu wako. Kama BWANA wetu alikaa nyikani siku 40, akiwa amefunga (bila kula wala kunywa), usiku na mchana, akijaribiwa, jua vipo vipindi kila mmoja wetu atapita vya ukame/kukaukiwa/uhitaji, nk., ili imani zetu, na upendo wetu kwa Mungu vipimwe. Uwe hodari na moyo mkuu, usizimie moyo wala kurudi nyuma, BWANA hatakuacha wala kukupungukia.

Amani na baraka za Kristo Yesu, ziwe nawe tangu sasa, na hata milele. AMEN.

Frank Philip.

Comments