UKIFA WAKATI UNAFANYA DHAMBI UTAENDA WAPI?

Neno la kuwapa ufahamu wanadamu kutoka kwa Peter Michael Mabula

Je umewahi kujiuliza maswali kama haya kwamba;
Ukifa wakati ukifanya dhambi ya uzinzi na uasherati utaenda wapi?
Ukifa unaiba au unafanya ujambazi utaenda wapi?
Ukifa unaroga utaenda wapi?
Mhubiri 3:1-2a ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa...''
Kuna wakati wa kuzaliwa na pia kuna wakati wa kufa.
Wanaokufa wakiwa hawana YESU maishani mwao huelekea matesoni kuzimu na baadae jehanamu. lakini waliompokea BWANA YESU wakifa wanapelekwa mbinguni na kuanza furaha ya milele maana wanakuwa wameshinda ya dunia.

MUNGU anapotutaka tuache maovu ana maana kubwa sana kwamba ili tusiende motoni.

Ayubu 2:9 ''Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru MUNGU, ukafe. ''
Ayubu alishawishiwa na mkewe ili atende dhambi ili afe, jiulize ingekuaje kwa Ayubu kufa tu baada ya kutenda dhambi. ingekuwa hatari lakini Ayubu alikuwa mcha MUNGU, alikuwa na hofu ya MUNGU na aliutaka uzima wa milele.
Leo wapo maelfu ya watu wanashawishiwa kutenda dhambi, na wengine wanatenda dhambi kipindi ambacho muda wao wa kukaa duniani ukiwa umeisha. jiulize je wanaenda wapi watu hao ambao wanakufa wakifanya dhambi?
Watu wengi kwa kuwahofu wanadamu wanajikuta wanafanya dhambi kila siku hata siku ya kuondoka ikifika wao watakutwa tu kwenye dhambi. Unakuta binti amegeuzwa hawara wa mwanaume ambaye ni mme wa mtu , na kwa sababu mwanaume huyo ndio humpa binti huyo pesa za kujikimu, hujikuta kila siku akifanya dhambi kuu, sasa akifa akiwa kwenye dhambi itakuaje?


Mathayo 10:28 ''Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. ''
Usijidangaye kwamba utatubu ukiwa mzee maana sio wote watafika uzeeni.
Kama unampangia BWANA YESU siku ya kumpokea unakosea sana.
Ndugu zangu Wokovu ni sasa.

Dhambi ni mbaya, dhambi huwatenga wanadamu na muumba wao milele.

Warumi 12:21 '' Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema. ''
Ndugu yangu hakikisha haushindwi na mabaya bali shinda ubaya kwa kufanya wema yaani heri kumtii MUNGU na sio wanadamu.
Wanadamu hawana mbingu ya kukupelekea, anayeokoa ni BWANA YESU pekee ni heri kumtii yeye na kukimbilia kwake kwenye uzima.
Hakuna ambaye hataondoka duniani lakini ni heri kuondoka na kwenda uzima wa milele kwa sababu BWANA YESU alikuokoa kipindi uko hai na ukaushika utakatifu wake daima.
Kuna furaha sana siku ya mwisho kwa wale ambao tuliokoka tukiwa hai na tukaliishi neno la MUNGU. Biblia inasema '' Kwa sababu BWANA mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.- 1 Thesalonike 4:16

Ndugu, uovu hautakiwi, kuna maangamizo ya milelel kwa wanaomkataa BWANA YESU.
Biblia inasema kwamba ''Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.-Mathayo 25:46.
Ndugu zangu hakuna haja ya kuikosa mbingu kwa ajili ya furaha tu za muda mfupi.
Maana wenye haki yaani waliookoka wataenda uzima wa milele na huko watakaa na BWANA milele, bali watenda dhambi ambao walipokuwa duniani walikufa bila kuokoka na kumtii KRISTO wao wataenda motoni kwenye adhabu ya milele. Biblia inatushauri kwamba
''Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.-Yakobo 1:21-24

 
Ndugu yangu Ogopa dhambi, ikimbie dhambi, usifanye dhambi na ichukie dhambi maana dhambi huzaa mauti yaani maangamizi ya milele.


BWANA YESU anashauri kwamba '' Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.-Marko 9:43.

 
Ndugu zanguni saa ya uzima ni sana tena ni muda huu. mpokee BWANA YESU na utaitwa heri. Zaburi 32:1 inasema '' Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.'' 

Huyu amesamehewa dhambi akiwa hai hivyo tunatakiwa tutafute kusamehewa dhambi zetu tukiwa hai.
MUNGU anatupenda sana na hakika hataki wala hahitaji hata mmoja wetu apotee.
Ndugu uliyesoma ujumbe huu hakikisha umeokoka na kumtii KRISTO huku ukianza kuongozwa kwa ROHO MTAKATIFU na acha kutazamia tamaa za mwili.
Huwa kunakuwa na furaha kuu mbinguni bada tu ya mtu mmoja kumpokea YESU, Biblia inasema ''Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.-Luka 15:7.

Ndugu hakikisha umeokoka na baada ya kuokoka hakikisha familia yako, ukoo wako, marafiki zako na wafanya kazi wenzio wote hakikisha wanaokoka.
Tuko zama mbaya sana ila neema ya BWANA YESU ingalipo, YESU anakungoja tu umpokee. Warumi 6:23 Biblia inasema '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.''

Ndugu yangu, ni heri kuwa ndani ya YESU mwenye uzima wako wa milele, nga'ang'ania uzima huu wala usimwache YESU aende zake kwa wengine huku wewe ukibaki kwa shetani. Biblia inasema '' atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.-1 Yohana 3:8''
Ndugu zangu, ni heri kukimbilia kwa Mwana wa MUNGU YESU KRISTO ambaye pekee ndiye anayeweza kukupa uzima wa milele.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292

mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.

Comments