HAKIKISHA UNASAMEHE NA KUSAHAU.


BWANA YESU asifiwe.
Karibu  tujifunze neno la MUNGU.
Leo tunazungumzia kusamehe.
 ''Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na BABA yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. -Marko 11:25''
Mfano mimi Peter nimemkosea mtu kosa  kubwa sana, ameumia sana na nimemuomba msamaha lakini amekataa kunisamehe kwa kusema hawezi kunisamehe hata kidogo, ni kweli nimemkosea sana na nimejuta sana kwa kukosea huko lakini nimeamua kumwomba MUNGU anisamehe dhambi zangu zote, MUNGU amenisamehe na jina langu lipo kwenye kitabu cha uzima daima, Kwa MUNGU mimi niko sahihi kabisa na niko huru hakuna shitaka hata moja juu yangu, nadunda na nasonga mbele tena huduma ndio inapanuka na maelfu ya watu BWANA YESU anawaokoa kupitia mimi. Lakini mimi kwa huyo ndugu  ni adui kwa sababu hajanisamehe, akifa bila kunisamehe anaenda motoni na mimi ambaye ndiye niliyekukusea naenda mbinguni kwa sababu MUNGU alinisamehe. Ndugu zangu, Hasara ni kwa huyu ambaye hajanisamehe hata kama niliyemkosea ni mimi, ndugu huyu alidhani ananikomesha kwa kutokunisamehe kumbe anajiangamiza yeye mwenyewe. Kanuni ya MUNGU kwamba kila mwanadamu asamehe kama vile yeye anavyoweza kusamehewa na MUNGU kama akimpokea BWANA YESU. Huu ni mfano tu wa madhara ya kutokusamehe. Hakuna aliyewahi kukusewa kama alivyokosewa BWANA YESU kwa kugongomewa misumari mikubwa  msalabani na kuteswa sana lakini BWANA YESU aliwaombea msamaha waliomkosea.''YESU akasema, BABA, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. -Luka 23:34a''.
Tabia ya MUNGU ni kutusamehe kama tukitubu. BWANA YESU kwenye andiko hilo hapo juu anatufundisha jambo kubwa zaidi yaani aliyekosewa anamuombea msamaha kwa MUNGU yule mtu aliyemkosea. BWANA YESU anawasamehe huku wakimchoma na mkuki tena wanagawana nguo zake, ni jambo kubwa sana hili. Ndugu yangu wewe kutukanwa tu ndio hutaki kusamehe je ungetendewa kama ilivyokuwa kwa BWANA YESU ingekuaje?
 ''Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. -Mathayo 5:7'' 
Rehema maana yake ni msamaha, Heri wenye kusamehe maana na wao watapata msamaha . ''Kisha Petro akamwendea akamwambia, BWANA, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? YESU akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. -Mathayo 18:21-22'' 
Wengi wamedhani wanawakomesha watu ambao wamewakosea, kwa kukataa kuwasamehe. na madhara yamewapata wao huku maadui zao wakiendelea mbele baada ya kutubu kwa MUNGU. ''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. -Luka 6:37''  usipoachilia na wewe hutaachiliwa na MUNGU, na  kama hutaachiliwa na MUNGU wewe huhusiki na mbingu,ukishindwa kunisamehe MUNGU hatakusamehe na MUNGU asipokusamehe dhambi inabaki kwako. mimi niko huru na nasonga mbele na wokovu wa BWANA.
Kusamehe ni muhimu sana kwa kila mwanadamu.
 ''mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. -Wakolosai 3:13''
Kutokusamehe kumewakosesha uzima maelfu ya watu.
Kusamehe ni jambo la lazima kwa wateule wa MUNGU wote.
Kama umeamua kwenda mbinguni au kupata uzima wa milele lazima uwe mtu wa msamaha.
MUNGU anapenda moyo wa msamaha na anapenda sisi watu wake tusamehe.
''Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. - Mathayo 6:14-15''.
MUNGU anapenda kutusamehe kama tukiamua kutubu, MUNGU anataka toba la kweli, usiposamehe watu na wewe MUNGU hatakusamehe, asipokusamehe MUNGU huwezi kwenda uzima wa milele. ''tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi. -Waefeso 4:32''
 Ndugu yangu, hata kama jambo gumu sana umekosewa unatakiwa tu usamehe maana hata wewe MUNGU amekusamehe na kukuvumilia katika mengi sana.
Hakuna faida inayotokana na kutokusamehe bali ni hasara tu siku zote. MUNGU anataka tuachilie. ''Kwa maana Wewe, BWANA, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao. -Zaburi 86:5'' 
MUNGU amekuwa ni mwepesi kutusamehe pindi tukiamua kutubu, kwanini sisi tusiwasamehe wengine? 
Kuna Watu Wanamishikaki Mioyoni Mwao, Yaani Hawajawasamehe Watu Fulani Waliowakosea Sana Na Wamewaweka Moyoni, Yaani Wakiwaona Waliowakosea Wanatamani Vidole Vyao Vya Mikono Vigeuke Bastola Wawapige.
  Ndugu Yangu Hakikisha Unaondoa Huo Mshikaki Moyoni Mwako, Wewe Wapo Wengi Tu Uliowakosema Ila Wamekusamehe Istoshe Ulipomkosea BWANA MUNGU Yeye Wala Hakukudhuru, Je Wewe Ndio Wa Kipekee Kuliko Wote Duniani Hata Usisamehe? BWANA YESU Anakushauri Leo Kabla Dhambi Ya Kutokusamehe Haijakupeleka Jehanamu, Anasema "Watendee Watu Yale Unayopenda Wewe Kutendewa" Wewe Unapenda Sana Kusamehewa Hivyo Samehe, Kutokusamehe Kutakuletea Presha Bure Mwisho Ufe Huku Ukimwacha Mtesi Wako Akinywa Supu Kwa Chapati. Ndugu Samehe, Neno La MUNGU Linasema "ukisamehe Na Wewe MUNGU Atakusamehe, Usiposamehe Na MUNGU Hatakusamehe Wewe.
Ndugu samehe na kusahau.  MUNGU anasema ''Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena. -Waebrania 8:12''
-Kusamehe na kusahau maana yake ni kwamba lile jambo ambalo umekosewa hata ukilikumbuka halikuumizi hapo umesamehe na kusahau. Kama kuna jambo ulikosewa na baada ya muda kupita kila ukilikumbuka unakosa raha au unaumia tambua kwamba hujasamehe tena hujasamehe na kusahau. ndugu tubu sana na mwambie MUNGU ''Nisamehe kwa kutokusameheme kwangu, nawasamehe wote walionikosea na niliwakosea, Damu ya YESU initakase kwenye hili na niwe huru sasa kwa jina la YESU KRISTO.'' Ndugu hakikisha unasamehe na kusahau.

''Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA. -Walawi 19:18''  
Dini Ni Mpango Wa Mwanadamu Kumtafuta Mungu, Na WOKOVU Ni Mpango Wa MUNGU Kumtafuta Mwanadamu. Je Kati Ya Dini Na Wokovu Unataka Nini?Najua unataka wokovu na wokovu ili uupate lazima kwanza usamehewe dhambi zako na BWANA na akikusamehe na wewe wasamehe wote na achilia na songa mbele na Wokovu. ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. -  1 Yohana 1:9''  
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani.
ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana
Ni mimi ndugu yako katika BWANA YESU.
Peter M Mabula
Maisha ya ushindi Ministry.
+255714252292

Mabula1986@gmail.com
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12


Comments