Kardinali Pengo; Fedha za waamini zisitumike kwa maslahi binafsi


ASKOFU

ASKOFU Mkuu Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka waamini wa jimbo hilo, kuwa wazi endapo wataona fedha wanazotoa kwa lengo fulani zimetumika kwa matumizi binafsi ya viongozi.

Amesema kunung’unika pembeni hakuna faida badala yake wanatakiwa kuwafuata viongozi wao na kuwaeleza ukweli ili waweze kubadilika na kutumia fedha watakazo kuwa wanapewa kwa lengo lililokuwa limekusudiwa.

Kardinali Pengo ametoa mwito huo hivi karibuni wakati akitoa mahubiri katika Misa ya Shukrani ya Mavuno ya jimbo hilo iliyofanyika katika Viwanja vya Msimbazi na kuhudhuriwa na Maaskofu Wasaidizi wa jimbo hilo Askofu Eusebius Nzigilwa na Askofu Titus Mdoe, mapadri, watawa pamoja na waamini wa jimbo hilo.
“Ninawashukuru sana kwa kujitoa kwenu katika Misa hii ya Shukrani ya kumtolea Mungu mavuno ya kutegemeza jimbo letu, lakini mnatakiwa kutuombea sisi mnaotukabidhi fedha hizi ili tuweze kuzitumia kama inavyotakiwa. Mkiona  tunazitumia tofauti kwa matumizi yetu binafsi msisite kutuambia,” amesema Kardinali Pengo.
Aidha amewasisitiza waamini kuwaombea viongozi wao ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Mtuombee mimi pamoja na maaskofu wasaidizi kwani ndio tunakabidhiwa fedha hizi,” amesema.
Katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Misa ya Shukrani ya Mavuno kwa ajili ya kulitegemeza jimbo hufanyika kila mwaka ikiwashirikisha waamini wa jimbo hilo na kila Parokia hutoa kiasi kadhaa cha fedha kulingana na malengo na uwezo wa parokia husika. Lengo lao  ni kuendeleza shughuli mbalimbali za uinjilishaji ndani  ya jimbo hilo.

Ripoti za Parokia kwa mwaka huu zimebaini kuwa, Parokia ya Mtakatifu Josefu imefanikiwa kutoa  shilingi milioni 135 na elfu 54, huku Parokia ya Mtakatifu Petro ikitoa shilingi milioni 105 na laki tano ikifuatiwa na Parokia ya Chang’ombe iliyotoa shilingi milioni 72 na laki tatu.

Katika mavuno hayo, kila parokia ilitoa ripoti ya kiasi cha fedha iliyotoa mwaka jana pamoja na kiasi cha fedha ilichotoa mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo ameendelea kuwashukuru waamini wa jimbo hilo na majimbo mengine pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa sala zao ambazo zimemuwezesha kuendelea kuimarika zaidi kiafya.

“Asanteni sana kwa sala zenu kwani kama mnavyoona ninajaribu kusimama bila fimbo ya kunisaidia, endeleeni kuniombea ili Mungu anijalie nguvu zaidi ya kuendelea kutimiza wajibu wangu,” amesema.

Comments