KUMILIKI PASIPO MIPAKA

Na Mtume na Nabii Josephat Mwingira.Efatha Ministry.
Mipaka.unaendelea kuangalia TABIA YA WANA WA MUNGU, leo tutaanza kutazama Tabia 10 ambazo unatakiwa kuwa nazo, fuatilia moja baada ya nyingine, ROHO MTAKATIFU Akakusaidie. Katika suala la Kumiliki pasipo Mipaka kuna mambo 10 muhimu ya kufanya yafuatayo:-

(i) Tafakari Kitabu au Neno la MUNGU
Jijengee TABIA ya Kutafakari Neno la MUNGU Asubuhi, Mchana na Jioni ili ujue MUNGU Anasema nini. Tabia hii itakufanya uweze KUELEWA Neno la MUNGU na Mafundisho yake kama inavyosisitizwa katika Biblia ya kuwa;

“Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na Mwanga wa njia yangu”. Zaburi 119: 105

Ukifahamu Neno la MUNGU, utajua unakokwenda, Njia ya kupita na kitu cha kufanya bali usipokuwa na Neno HUTAJUA haya yote. Kabla ya hujafanya jambo lolote ni Vizuri utafakari juu ya jambo unalotaka kufanya kulingana na linavyosema Neno la MUNGU.

(ii) Amuru au Sema Neno
Uwe na tabia ya KUTAMKA au KUSEMA Neno ili jambo litendeke. Tunasoma katika Biblia “Ee BWANA sema neno moja tu na Roho yangu itapona”.

Kumbuka kisa cha yule Akida aliyekuwa na mtumishi mgonjwa aliyemwendea Bwana YESU na kusema; 

“Yule Akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.” Mathayo 8:8b


Tabia ya Wana wa MUNGU ni ile ya kusema Neno ili liweze kufanya Kazi, kwa sababu MUNGU hafanyi jambo bila mtu kusema Neno.
Anasema;
“Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia Watumishi wake Manabii siri zake.” Amosi 3:7


Hata nyakati zetu sisi, MUNGU anataka kusikia UMESEMA nini, ili halitakaa litendeke jambo lolote hadi kwanza Umesema neno. Tabia ya kusema neno IKIUMBIKA ndani ya mtu, inaruhusu Utendaji wa MUNGU kuthibitika. Usinung’unike na Kulalamika bali TAMKA neno, kwa sababu hiyo ni TABIA YA MAMLAKA.
Mfano:

Siku moja Musa alishindana na Kora, dathani, Abiramu na wengine katika Kusanyiko, wakibishana na kukaidi maagizo yake. Mwisho Musa akaamua KUSEMA neno, tunasoma;


“Kama watu hawa wakifa kifo cha siku zote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua kwamba watu hawa wamemdharau BWANA.” Hesabu 16:29-30

Musa alipomaliza kutamka hayo maneno ardhi ilipasuka ikawameza wote, na mahema yao na vitu vyao vyote, ardhi ikajifunika tena. Umati ule ukamgeukia Musa na kusema Musa umeua watu. Hawakusema MUNGU Ameuwa watu kwa sababu Hawakumwona au Kumsikia MUNGU akisema. Walimsikia Musa akitamka na IKAWA.
(Itaendelea....)

MUNGU akubariki sana.

Comments