MADHARA YA KUMKANA YESU KRISTO.

BWANA YESU atukuzwe milele ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU aliye hai.
Leo tunazungumzia madhara ya kumkana YESU KRISTO.
 Yuda 1:1-4 Biblia inasema '(Yuda, mtumwa wa YESU KRISTO, ndugu yake Yakobo, kwa hao walioitwa, waliopendwa katika MUNGU Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya YESU KRISTO. Mwongezewe rehema na amani na upendano.  Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya MUNGU wetu kuwa ufisadi, nao HUMKANA yeye aliye peke yake MOLA, na BWANA wetu YESU KRISTO.)
Mtume Yuda ila sio Yuda Eskarioti aliyemkana YESU aliwaandikia Wanadamu wote  kwamba waishindanie Imani ya uzima wa milele ambayo ni moja tu. Katika kuwaonya alizungumzia pia kwamba kuna watu waliojiingiza kwa siri katika kundi la wateule ili kuibadili neema ya MUNGU kuwa ufisadi, na hao ndio makafiri, na humkana MUNGU BABA na BWANA YESU. Hao ni wa kujiepusha nao sana. 

-Ndugu yangu kuna watu hukana YESU, 
-Kuna watu humkana YESU kwa sababu ya kushika mafundisho ya viongozi wao wa dini yasiyotokana na Biblia. 
-Kuna watu hata kama wanaenda kanisani humkana YESU kwa sababu ya matendo yao na tabia zao, 
mimi sijui kama wewe ni mmoja wao wa wanaomkana YESU ndiposa ujumbe huu umekuja kwako leo ili kukusaidia kurudi kwenye kusudi la MUNGU la uzima wako ambao hauko kwingine ila kwa BWANA YESU.Kumkana YESU inaweza kuwa kwa kutamka au kwa matendo ya mwili na roho. Ndugu yangu, Kama unamkana YESU hakika unaikana mbingu.
Mtume Petro aliwaambia hivi Wayahudi waliomkana YESU na kumsaliti  '' MUNGU wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, MUNGU wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake YESU, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye MUNGU amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. ..............Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; apate kumtuma KRISTO YESU mliyewekewa tangu zamani; -Matendo 3:13-15''.
Mtume Petro aliwaomba watu hao watubu na kurejea kwa BWANA waliyemkana mwanzo, Ndugu yangu hakuna jinsi zaidi ya kurejea kwa BWANA YESU kama kweli unautaka uzima wa milele.

Kumkana YESU Ni 

1. Kumkataa ROHO MTAKATIFU Maana Asiye Na ROHO Wa KRISTO Huyo Sio Wake; Maana '' Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake.-Warumi 8:9''

2.  Ni Kutomtii YESU; Maana '' Bali MUNGU aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa KRISTO alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na MUNGU kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake-Warumi 5:8-10'' 

3.  Ni Kufanya Dhambi; Maana ''Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha KRISTO, ili kila mtu apokee ijara(malipo) ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya- 2 Kor 5:10''

4.  Ni Kushindwa Kulitangaza Neno Lake; Maana ''Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo BABA kwa jina langu awapeni.Yohana 15:16''

5.  Ni Kakataa au kuacha Wokovu; Maana ''Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima- 1Yohana 5:11-12'' 

6.  Kumkana YESU Ni Kukataa Kumwamini; Maana ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;-Yohana 1:12''

7.  Kumkana YESU Ni Kukataa Kuokoka; Maana ''kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.-Warumi 10:13''
8.  Ni Kukataa Kutubu; maana “Kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi”. (Matendo 10:43)
 
9.  Ni Kukataa Kuwa Chini Ya MUNGU Aliye Hai; Maana ''
Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia MUNGU, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya MUNGU, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.Warumi 1:28-32''

10. Ni Kukataa Kulikiri Au Kulitaja Jina Lake Kwa Kuwaogopa Au Kuwahofu Watu; Maana ''Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za BABA yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za BABA yangu aliye mbinguni.-Mathayo 10:32-33''

11. Kumkana YESU Ni Kumtumikia shetani; Maana ''Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;  wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.- 1 Timotheo 4:1-3''

12.  Kumkana YESU Ni Kukataa Uzima Wa Milele; Maana ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu-Warumi 10:9-10''
 
-Ndugu Yangu Mpendwa, Kama Ulimkana YESU Popote Tubu Na Anza Kumkiri Popote Uendako.
  -Wewe Unayemkana YESU na unaendelea kumkana bila kutubu na kuacha tabia hiyo Ipo Siku Na Yeye Atakukana. 
-Wewe Unayemkana YESU Ili Tu Uolewe Au Kuoa ipo siku atakukana,
-Wewe Unayemkana Ili Tu Upate Kazi ipo siku atakukana.
-Wewe Unayemkana YESU Kwa Kwenda Kwa Waganga Wa Kienyeji ipo siku atakukana.
- Wewe Unayemkana YESU Kwa Kwenda Kwa Wasoma Nyota ipo siku atakukana. 
Ipo Siku YESU KRISTO Atawakana, Ni Hasara Kuu Kukanwa Na YESU. 
-Wewe Unayemkana YESU Ili Tu Umpendezeshe Mmeo/mkeo Unakosea Sana, Tubu ndugu.
-Wewe Unayemkana YESU Kwa Kutaa Kuifanya Kazi Yake Ipo Siku Atakukana. 
Ndugu Geuka Na Anza Kumtii BWANA YESU Sasa.
Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.'' ila ni jina la YESU KRISTO tu.

 Kumpinga KRISTO Ni Kuchagua Jehanamu, Ni Kujipiga Chapa Ya Mnyama 666. Unaeendelea Kumkataa YESU Ipo Siku Utamtaka Ila Utakuwa Umechelewa. Mchague YESU Leo Ili Uandikwe Jina Lako Kwenye Kitabu Cha Uzima.

 Siku za karibuni  Kwenye Ndoto Niliwaona Wateule Wa BWANA YESU Wakiingia Mbinguni, Wengine Safari Yao Ya Mbinguni Ilikuwa Rahisi Na Wengine Safari Yao Ilikuwa Ngumu Sana Yaani Ni Kwa Neema. BWANA YESU Tusaidie Kukushika Wewe Siku Zote Za Maisha Yetu. Leo Nimeaamini Kile Alichokisema Mtume Petro Kwamba "Tukikuacha Wewe BWANA YESU Tuende Kwa Nani? Wewe Una Maneno Ya Uzima.''
 Ndugu Wa Kirohoni Tuliokombolewa, Tutafakarini Sana Yatupasayo. YESU Anatupenda Sana Na Ana Uzima Wetu Wa Milele. Mimi Na YESU Milele
 Yohana 14:6 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi''
Ndugu Zangu Dunia Itapita, Kila Mtu Ataondoka Duniani. Mojawapo Ya Maeneo Haya Mawili Kila Mwanadamu Huenda. -Kundi La Kwanza Wataondoka Na Kwenda Mbinguni, Hao Ni Wateule Wa MUNGU Waliotakaswa Kwa Damu Ya YESU KRISTO. Hawa Ni Waliookoka Wangali Wakiwa Hai Duniani, Walikubali Kumpokea BWANA YESU Kama BWANA Na MWOKOZI Wao, Wakaliishi Neno La MUNGU Na Kubaki Wokovuni Hadi Mwisho Wa Maisha Yao. 
-Kundi La Pili Wataondoka Duniani Na Kwenda Kuzimu Tayari Kwa Maandalizi Ya Jehanamu, Kuzimu Ni Mateso Ila Jehanamu Ni Mateso Zaidi. Watakaoenda Kuzimu Ni Ambao Hawakuokoka Kipindi Wanaishi Duniani Na Hawakuushika Wokovu Hadi Mwisho Wa Kuishi Kwao Duniani. Ndugu Yangu YESU Anakuita Leo, Ukiisikia Sauti Yake Kutoka Ndani Ya Ujumbe Huu Hakikisha Unaenda Kanisani Kuokoka. MUNGU Akupe Kuona Yaliyofichika Kwako Ya Uzima Wa Milele. Ndugu Kazana Kwa YESU Maana Usipoenda Mbinguni Basi Utaenda Kuzimu Ya Mateso.

 Ndugu Ukifa Muda Huu Unaenda Ama Mbinguni Ama Kuzimu. Mbinguni Wanaenda Waliotakaswa Kwa Damu Ya YESU KRISTO Na Kuzimu Wanaenda Watenda Dhambi Waliokataa Kumpokea BWANA YESU Walipokuwa Hai. Ndugu Yangu YESU KRISTO Ni Muhimu Kwako Kuliko Chochote Ukifanyacho.
 Yohana 11:25-26 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. ''
Watu Wengi Wameenda Jehanamu Huku Wakijua Kwamba MUNGU Ni Mmoja. Lakini Kilichowapeleka Huko Sio Kujua Kwamba MUNGU Ni Mmoja Bali Wako Huko Kwa Sababu Walimkataa BWANA YESU Aliye Njia Pekee Ya Kwenda Uzima Wa Milele Iliyoamriwa Na MUNGU. Kumkataa YESU Au Kumkana Ni Kukataa Uzima Wa Milele.

 Ndugu usiogope hao wanaokuita kafiri kwa sababu ya KRISTO maana
 -Heri Kuitwa Kafiri Kwa Sababu Umeyakataa Mafundisho Ya Mashetani Kuliko Kuitwa Mtakatifu Huku Unaabudu shetani.
-Heri Kuitwa Kafiri Huku Jina Lako Limeandikwa Kwenye Kitabu Cha Uzima Cha MUNGU Kuliko Yule Anayejiita Mtakatifu Huku Yuko Kwenye Gari Ya Kuelekea Jehanamu.

 Mtume Petro Alimkana YESU Ila Akatubu, Sijui Kwa Upande Wako Uliyemkana YESU Utatubu Lini? Wokovu Ni Sasa Tena Ni Sasa Hivi.

Kama Unaitumia Siku Ya Leo Kwa Mabaya Ni Kwa Kujiangamiza Wewe Mwenyewe, Na Kama Unaitumia Siku Hii Kwa Mema Ubarikiwe.
Ufunuo 1:7 ''Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. ''
 Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
0714252292

Comments