SOMO: MUNGU WA DUNIA

NA MCHUNGAJI KIONGOZI: JOSEPHAT GWAJIMA,UFUFUO NA UZIMA.

“Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;
 ambao ndani yao Mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” 2  Wakorintho 4:3
Sio kila asemaye Mungu anamaanisha Mungu wa mbinguni. Yule muovu, shetani naye pia anaitwa Mungu, lakini ni Mungu wa dunia. Mungu wa dunia hii ana majina mengi sana.
Mungu ni kama cheo kama ilivyo kwa rais. Cheo chake ni rais wa Tanzania lakini jina lake ni Jakaya Mrisho Kikwete. Mungu tunayemwabudu ni Mungu wa mbingu na nchi, Mungu mwenyezi, Mungu Yehova.
“Nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.” Kutoka 6: 3
Mungu wa dunia hii ndio huyohuyo biblia imamtaja kama mkuu wa ulimwengu.
“Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.” Yohana12:31
Mungu huyo sio Mungu wetu sisi. Mungu wetu sisi ni Mungu wa mbingu na nchi ambaye wana wa Israeli walimwita Yehova. Mahali anapotaka kujionyesha mwenye nguvu alitokea kama Jehoiva Eligibo; Jehova Mikadeshi, Mungu atakasaye; Jehova Rohi Mungu aongozaye; Jehova Rafa Mungu aponyae, Jehova Nisi bendera yetu. 

Kwenye agano jipya  aliamua kuvaa mwili akazaliwa na tukauona utukufu wake. Alikuja kama neno akavaa mwili akazaliwa akaitwa Yesu. Lakini Neno alikuwepo tangu mwanzo na ndiye Mungu.
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.  Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.  Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.  Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.  Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yohana 1:1
Yesu Kristo maana yake Yehova amashia yaani “Mungu yule yule.” Leo kuna mabishano makubwa kuhusu Yesu juu ya uMungu wake. Ukisema Yesu ni nabii hakuna ubishi hapo, ukisema ni mtume hakuna anayeongea lakini unaposema tu kuwa Yesu Kristo ni Mungu panatokea kutoelewana na dunia inatikisika.
Yesu naye alimwita Mungu wa dunia mkuu wa ulimwengu, jina jingine anaitwa mwovu maana yake ni mbaya ana uovu ndani yake. Unatakiwa ufike mahali uone sio kila mtu anayesema Mungu atatusaidia anamaanisha Yesu kristo, wengine wanakuwa wakimaanisha mungu wa dunia hii. Ndio maana ya lile andiko linasema ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikra zao. Kwa hiyo wao wana mungu wa dunia hii ndani yao lakini sisi tuna Mungu wa Mbingu na nchi. Shetani amekuwa mmiliki wa dunia hii baada ya Adamu kukosa. Kwenye dunia ni kambi ya shetani. Lakini nataka ujue Mungu aliye ndani yetu ni mkuu sana ndio maana sisi tuliombeba tunao uwezo wa kuishi duniani. Yaani tumeweka kambi ndani ya kambi ya adui.

“Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.” Yohana14:30
“kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.” Yohana  16:11
“Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.” 1 Yohana 4:4
Kuna nguzo nne ambazo shetani anazitumia kuiendesha dunia, Nguzo hizi ni:
1.   Siasa
2.   Uchumi
3.   Dini
4.   Jeshi
Hizi ni sehemu ambazo mungu wa dunia hii amezikamata na anaziendesha kama aonavyo vyema yeye. Ndio maana leo unapotaka kuingia kwenye siasa lazima uchafuliwe kwanza kwa wizi na mambo mengine ndipo ufanikiwe. Lakini Mungu akaaye ndani yetu atazuka katika uso wa nchi na kuziangusha tawala zote za ufalme wa mungu wa dunia hii. Hapo ndipo hata wewe uliyeokoka utaweza kuingia kwenye siasa na utakatifu wako.
“Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.” 1 Yohana 5:19
Andiko hili linamaanisha dunia yote inaongozwa na yule mwovu ambaye ni mkuu wa ulimwengu au mungu wa ulimwengu. Watu wa dunia hii kadri wanavyoongezeka kifedha, heshima na umaarufu ndivyo wanavyozidi kuwa wabaya. Lakini wao huona ni kawaida kwa kuwa wamepofushwa fikra zao.
“Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?  Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa.  Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;  bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi;  bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.  Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.  Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;  bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu;  tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko;  mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.  Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi;  kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.” 1 Wakorintho 1:20-31
Kuna watu wana hekima sana; lakini ni hekima ya dunia hii. Wanaweza kuongea maneno mpaka ukadhani ni Mungu wa mbingu na nchi anaongea kupitia wao kumbe ni mkuu wa ulimwengu/mungu wa dunia hii. Kuna watu wanatumia hekima ya dunia hii kutawala dunia.
 
Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika;  bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;  ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;  lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.  Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.  Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.  Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.  Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.  Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.  Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.  Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.” 1 Wakorintho 2:6-16
Lakini ipo hekima ya kiMungu pia ambayo Yakobo anaielezea namna ilivyo.
Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.  Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani. Yakobo3:15
Hekima hizi mbili zinakinzana wakati wote hapa duniani. Haina maana kuwa tunapowatambua wenye hekima ya dunia hii basi tuwatenge. Hapana, bali tunaungana na watu hawa lakini kwa malengo. Tunaungana na watu ili kuwabadilisha wao wawe sehemu yetu na sio sisi kuwa sehemu yao. Ni vizuri unapoenda sehemu katikati ya watu wanaomtumikia mungu wa dunia hii uwe makini wasikubadilishe wewe kuwa sehemu yao. Mungu wa dunia hii ni mungu wa uongo naye hupofusha fikra za watu. Atajaribu kukupofusha wewe pia.
“Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.  Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.” Luka 4:1-5
Shetani  alimpandisha Yesu na kumwonyesha miliki za dunia na fahari kwa dakika moja akamwambia mimi (ibilisi) humpa yeyote nipendavyo ila uniabudu. Kumbe basi kila aliyefanikiwa kwenye nguzo za dunia amepata kwa Bwana Mungu Yehova ama kwa ibilisi mkuu wa dunia hii baada ya kuabudu. Shetani aliuchukua utawala wa dunia kutoka kwa Adamu na kuigeuza dunia kuwa kama ilivyo leo. Adamu akija leo ataona dunia ni tofauti na alivyoiacha kwasababu ya uharibifu mkuu uliofanywa na mungu wa dunia hii. Ulimwengu uko chini ya yule mwovu asiyewaacha wafungwa wake waende zao ndio maana anaweza kutoa mali na vyote vilivyomo kwa yule atakayemwabudu.
“Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Warumi 12:2
“Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele. Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza.  Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.  Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.  Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.” 1Yohana 2:15
Dunia na tamaa zake vitapita bali yeye alishikaye neno la Mungu atadumu milele. Mungu anayetupenda ametuweka kwenye dunia ambayo mkuu wake ni ibilisi na kutupatia nguvu na mamlaka ya kumtiisha. Ndio maana Yesu alipoanza kuwafundisha watu jinsi ya kuomba aliwaambia waombe wakisema, “baba yetu uliye mbinguni” sio marekani wala ulaya bali mbinguni. “Jina lako litukuzwe” kwa maana jina lake limetukuka. “Ufalme wako uje” ili kabla kanisa halijanyakuliwa ufalme wake uje.
Mungu alimwacha shetani aujenge utawala wake hapa duniani ili amtume Yesu kama nuru auokoe ulimwengu ndio maana imeandikwa; “na ile nuru yangaa gizani nalo giza halikuweza kuishinda.” Kwa sababu hiyo Yesu Kristo alidhihirishwa ili kuudhihirisha uweza wake. Ni hakika kabisa kuwa watakaoingia mbinguni ni wengi zaidi ya watakaoingia kwenye moto wa jehanamu. Ndio maana leo kazi yetu mimi na wewe ni kuwapunguza wale wanaoelekea jehanamu ili waingie mbinguni.
“Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;  na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.” Yohana 17:9
Haya ni maneno ya Yesu, anajua ulimwengu una shetani na mawakala wake. Anasema ulimwengu umewachukia kwa sababu ukiwa wa Mungu wewe sio wa ulimwengu huu. Kama ambavyo Yesu alichukiwa wewe pia utachukiwa kwa sababu kama ambavyo alivyokuwa sio wa ulimwengu huu ndivyo na wewe ulivyo. Uko hapa kwa kazi maalum utakapoimaliza unarudi kwa baba. Lakini shetani ameshika watu wa Mungu kwenye ulevi, ukahaba, wizi na uharibifu wa kila aina.
Shetani anazo taarifa juu ya kila mtu anayezaliwa ulimwenguni kwa kuwa yeye ndiye mkuu wa ulimwengu huu. Anajua makusudi ya kila mtu pia, hivyo anaanza kuharibu lile kusudi tangu siku unayozaliwa. Kuna watu wamekuwa wagonjwa tangu siku waliyozaliwa. Lakini bado Mungu wetu anao mpango wa kukutoa hapo ambapo yule muovu amekuweka. Ndio maana ya maarifa kama haya, unapoelewa nini kinaendelea kwenye maisha yako na nini ufanye ili urudi kwenye kusudi lako la asili.
Mtu una matatizo kwasababu shetani amekuwekea matatizo kwasababu anajua utakuwa nani baadaye anajua Mungu wa mbingu na nchi ameweka kipawa cha aina gani ndani yako, mkuu wa dunia hii anakuzuia ili usije fikia pale unapotakiwa kufika. Shetaani hapambani na wewe kwasababu ulivyo anapambana na wewe kwasababu ya kitu ambacho Mungu ameweka ndani yako, elimu inatusaidia kuendeleza kile kilichowekwa na Mungu ndani yako.
“Imeandikwa kabla haujatungwa katika tumbo la mama yako nalikujua” wachawi wanahitaji kile ulichonacho ndani yako ili waendeleze ufalme wa mkuu wa ulimwengu kwenye siasa, uchumi, jeshi, dini”

MAOMBI.
Mkono wa mungu wa ulimwengu ulionyooshwa kwenye maisha yangu ninauvunja kwa jina la Yesu, leo nina rudi kwenye kusudi langu kwa jina la Yesu.
Kwa damu ya Yesu ninaangusha nguzo za mkuu wa ulimwengu. Wale wote mliokaa kwenye nguzo za kisiasa, dini, jeshi na uchumi chini ya mkuu wa ulimwengu ninawaangusha wote kwa jina la Yesu. Ewe mkuu wa ulimwengu nakufunga leo kwa jina la Yesu, ninaangusha fikra zako ulizoziweka kwenye maisha yangu kwa jina la Yesu Kristo. Kila hekima ya mkuu wa ulimwengu ninaiharibu kwa jina la Yesu. Kwa mamlaka ya Jina la Yesu Kristo ninazikamata nguzo zote za mkuu wa ulimwengu kwa jina la Yesu, ninafuta kila upofu wa mkuu wa ulimwengu kwenye macho yangu, akili yangu, moyo wangu kwa damu ya mwanakondoo. Ninakunyanganya kazi yangu, afya yangu uliyoigusa kwa mkono wako ewe mkuu wa ulimwengu kwa jina la Yesu Kristo.
Mashetani, majini, mapepo, mizimu, wagang, wasoma nyota na wengine wote watumishi wa mkuu wa ulimwengu ninawasambaratisha, nawafyeka kwa jina la Yesu.
Ninaamuru nyota ya safari, kupendwa, kuhubiri, biashara inayotumiwa na watu wa dunia hii irudi kwa jina la Yesu. Amina.


Comments