TAMASHA LA CHRISTMAS, KULA PAMOJA NA YATIMA.

Alex Msama ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya tamasha la Christmas.

Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismasi inatarajia kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa kugawa vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa baadhi ya vituo vya kulelea yatima vya jijini Dar es Salaam.

 Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Jimmy Rwehumbiza hafla hiyo ya makabidhiano hayo inatarajia kufanyika Desemba 20 kwenye ofisi za Kampuni ya Msama Promotions zilizoko Kinondoni Block 41. 

Rwehumbiza alisema wamefikiria kukabidhi zawadi hizo ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo ambayo imejikita kusaidia jamii zenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu na wajane. “Tumeonelea kabla ya tamasha kufikisha mchango wetu kwa jamii, kwani sisi kama wadau wengine tunahitajika kusaidia kupitia kidogo tunachopata,” alisema Rwehumbiza.

 Wakati huohuo waimbaji watakaoimba kwenye Tamasha la Krismasi katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Songea wanatarajia kupigwa msasa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kupitia semina itakayofanyika Desemba 17 katika ofisi za Msama Promotions, Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Abihud Mang’era semina hiyo itahusisha baadhi ya watendaji wa Basata ambao watafikisha ujumbe wa serikali katika tasnia ya muziki. Mang’era alisema ni muhimu kwa waimbaji kuhudhuria semina hiyo ambayo ina lengo la kuwapa mwangaza waimbaji ambao watashiriki kutoa huduma ya neno la Mungu. “Ni muhimu kwa waimbaji kuhudhuria katika semina hiyo ambayo itaongozwa na watendaji wa Basata ambao watashirikiana na watendaji wa Msama Promotions,” alisema Mang’era. Mang’era alisema semina hiyo itawasaidia waimbaji kukumbuka masuala ya msingi pindi wawapo jukwaani ambako alisisitiza waimbaji kuhudhuria semina hiyo.

Comments