AGANO JIPYA NA LA MILELE KATIKA DAMU YA YESU KRISTO.



BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze moja ya vitu muhimu sana kuvijua kwa kila mtu.
Agano maana yake ni patano au mapatano.
Agano hutokea baada ya pande mbili kuhusika.

Naomba unielewa kwamba sizungumzii agano jipya yaani vitabu 27 vya Biblia na wala sizungumzii agano la kale yaani vitabu 39 vya Biblia. Wapo watu hata hudanganywa kwamba agano la kale yaani vitabu 39 havihusiki kwa sasa na badala yake wameamua kuchukua tu Zaburi na Mithali na kuunganisha kwenye Mafundisho yao. Haiko hivyo agano hili ninalozungumzia sio maandiko bali Agano la MUNGU kwa wanadamu. Vitabu vya agano jipya na agano la kale vyote lazima vitumike katika makanisa yote.

Katika historia ya wanadamu MUNGU alifanya maagano mawili makubwa na wanadamu. Agano la kwanza ni lile ambalo MUNGU alifanya na wana wa Israeli mlima Sinai Kutoka 24:4-8 ‘’ Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng'ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. ‘’
Agano likafanyika na muhuri wa damu ukawekwa. Agano maana yake upande mmoja ukienda tofauti na makubaliano maana yake agano linavunjika. Waisraeli walipewa amri 10 pamoja na sheria na taratibu za kuishi ambazo jumla yake ni 613.

Jukumu lao lilikuwa ni kutenda sawasawa na MUNGU alivyowaamuru lakini Waisraeli walivunjwa agano au patano. MUNGU akasema hivi Waamuzi 2:2,20 ‘’ nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? , Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; ‘’
-Baada ya Waisraeli kuvunja agano ambalo MUNGU BABA aliagana nao, MUNGU aliadhimia kufanya agano jingine au agano jipya na wanadamu wote. Mwanzo MUNGU alifanya agano na waisraeli peke yao kwa lengo la wao kulishika na ili mataifa mengine yote yajifunze kwa waisraeli na kufuata sheria za MUNGU aliye hai maana wakati huo taifa waliokuwa wanamwabudu MUNGU aliye hai walikuwa waisraeli peke yao. Waisraeli kwanza walivunja agano kwa kufanya dhambi pili waisraeli hawakuwafundisha mataifa mengine kuhusu MUNGU muumbaji ambaye ni wao tu waliokuwa wanamwabudu na kumjua kwa wakati huo.

Mpango wa kuleta agano jingine la milele ukaanza. Miaka zaidi ya 600 kabla ya BWANA YESU kuja duniani, ROHO wa MUNGU kupitia Nabii Yeremia akasema ‘’ Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema BWANA. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena. - Yeremia 31:31-33’’.

Manabii wengi walitabiri juu ya kujwa Kwa bwana YESU ambaye kupitia yeye ndipo uzima utapatikana, uzima wa miili mpaka uzima wa milele. Miaka zaidi ya 500 ROHO wa MUNGU alisema kupitia Nabii Mika kwamba YESU yuko tangu milele yaani hana mwanzo, jambo jingine ni kwamba YESU atazaliwa kutokea Bethlehemu, Mika 5:2 ‘’ Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.’’.

Nabii Danieli yeye aliona makubwa zaidi yaani aliona mamlaka ya YESU ni mamlaka isiyoweza kuangamiza na tena aliona hadi kufa na kufufuka kwa YESU, Pia aliona kwamba YESU pekee ndiye atakayekuwa mwokozi wa wanadamu wote, kila taifa na kila kabila Daniel 7:13-14 ‘’ Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo MZEE WA SIKU, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. ‘’

Agano hili jipya na la milele lilikuwa linakuja, ni agano la kipekee na mfanya agano hilo ni MUNGU mwenyewe.

Kabla ya kuja BWANA YESU Manabii walisema kwamba atakuja kwanza atakayetengeneza njia ya BWANA na kunyoosha mapito yaani Yohana Mbatizaji ambaye ndiye aliyetabiriwa katika kitabu cha Isaya. Lakini katika Malaki anazungumziwa kwamba atakuja katika roho ya Eliya. Ni miujiza ya MUNGU hakika Malaki 4:5 ‘’ Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya. ‘’

BWANA YESU akaja kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu wote watakaompokea.

Malaika alisema yafuatayo. Mathayo 1:21 ‘’ Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. ‘’

Wokovu ukafika na BWANA wa uzima YESU KRISTO yuko tayari kuokoa wanadamu wote wataomwendea.

Katika kuweka muhuri wa agano la milele BWANA YESU alisema hivi ‘’ kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi-Mathayo 26:28’’

-Ndugu yangu Wokovu huu ni kwa ajili yangu na yako pia.
Kuna kazi nyingi sana za damu ya YESU katika agano la milele.

-Kwa Damu ya YESU tunamshinda shetani(Ufunuo12:11)
-Kwa Damu ya YESU tunahesabiwa haki(Warumi 5:9)
-Tunasafishwa roho zetu kwa Damu ya YESU(1 Yohana 1:7)
Kuna kazi nyingi za damu ya YESU na hata uzima wa milele

tunaupata kupitia Damu ya YESU KRISTO.
Hakuna uzima wa milele kwingine kokote nje ya YESU KRISTO(Matendo 4:12 Pia unaweza kusoma  Yohana 14:6-7
YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na BABA; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. ).

Hili ndilo agano jipya na la milele ambalo liko katika damu ya YESU na ambalo kwa hili tunaupata uzima wa milele.
Kutoka kila taifa ukimwendea YESU ili akuokoe hakika atakuokoa na kukuponya pia, kukufungua pamoja na kukuacha huru mbali na uonevu wa shetani.
Waebrania 13:20 ‘’ Basi, MUNGU wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye BWANA wetu YESU, ‘’

 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments