KUUSHINDA ULIMWENGU - II

Na Frank Philip.
“Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui” (Luka 22: 31-34).
Katika hadithi ngumu za biblia, hii imo. Mara nyingi najiuliza, inakuwaje Petro, siku zote alikuwa msitari wa mbele hadi kuona kifo sio kitu, leo anamkana BWANA tena akiisha kuonywa mbele! Kuna mambo mawili ya kujifunza: unyenyekevu na kumtegemea Mungu.
Somo lililotangulia lenye kichwa “kuushinda ulimwengu”, kuna kanuni za kuushinda ulimwengu, ambazo ni kuwa ndani ya Kristo, kuwa mtendaji wa Neno, na Kujilinda. Yohana anasema “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi” (1 Yohana 5:18). BWANA alipoona hatua za Ibilisi dhidi ya wanafunzi wake, alimwombea Petro ili “imani yake isitindike”, huu ni ulinzi wa Mungu kwa njia maombi (kujilinda), lakini bado Petro alimkana BWANA baada ya masaa machache tu! Shida iko wapi? Je! Maombi ya BWANA yalikuwa bure tu? La! Hasha, Petro kweli alimkana BWANA, ila imani yake haikutindika.
Niliposoma habari za Petro nikajiuliza, hivi Petro alitakiwa kufanya nini cha zaidi ili asimkane Bwana Yesu? Kumbuka jambo hili, BWANA angeweza kufumba kinywa cha Petro ili asimkane, ila alichoomba sio KUSHIKA KINYWA cha PETRO, ila IMANI yake isitindike!
Ni rahisi sana kuhesabu MAKOSA ya watu, bila kujua KIASI cha imani yao. Imani hukaa moyoni, kwa maana imeandikwa, “kwa moyo mtu huamini hata kupata haki”, nani aonaye moyoni kwa mwingine? Sasa, tukijua kwamba “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani”, nikaona jambo hili, maneno ya Petro kumkana BWANA ilikuwa kosa, na chukizo, ila kwa kweli “Mungu akichunguza moyo” wa Petro anaona yuko tayari kufa kwa ajili ya BWANA. Ndipo nikaona maana ya neno hili alilosema Yohana kwamba, “msipende dunia na mambo yake” na “apendaye ulimwengu, kumpenda BABA hakumo ndani yake”. Kweli Petro alimkana BWANA, ila hapendi dhambi na haishi kwenye hiyo! Bado BWANA akijua huyu jamaa amenikana mara 3 hadharani, anarudi kwake na kumwambia “nitajenga kanisa langu juu yako, wala milango ya kuzimu haitaliweza”, ni Petro yule yule. BWANA aliona nini? Bila shaka aliona MOYO wa IMANI na KUMPENDA BWANA.
Fikiri nini kingetokea baada ya BWANA kumwambia Petro, “utanikana mara 3”, na Petro badala ya kusema “niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni”, akabadili kauli yake na kusema “BWANA nisaidie nisikukane”? Petro alipoambiwa yatakayotokea, alikaa kimya! Yakatokea kweli kama BWANA alivyosema, japo Petro alikuwa tayari kufa. Angalia jambo hili, kweli una ujasiri na imani yako, umevuka mengi ila haimaanishi kwa sababu uliweza jana na kesho utaweza tu! Kuushinda Ulimwengu hakuji kwa UZOEFU wa mambo ya jana, ila Neema ya Mungu ukijua kusimama katika zamu zako KUOMBA msaada wake kila iitwapo leo, na hii ndio maana halisi ya KUMTEGEMEA Mungu.
Frank Philip.

Comments