KUUSHINDA ULIMWENGU – III

Na Frank Philip.
“Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima” (2 Samweli 9:3-7).
Mara nyingi tafsiri ya kuushinda ulimwengu inaleta picha ya mtu mpiganaji, jemadari, mwenye juhudi na MKAMILIFU sana ashindaye kila siku, lakini hii sio picha sahihi. Kama umesoma somo la kwanza katika mfululizo huu, utaona mambo matatu (kuwa ndani ya Kristo, kuwa mtendaji wa Neno, na Kujilinda) ambayo ni siri ya kuushinda ulimwengu. Ukiangalia katika somo la II, utaona tena mambo mawili (unyenyekevu na kumtegemea Mungu) ambayo washindi wengi wana tabia hizo. Hakuna mahali mtu anashinda kwa sababu ni MKAMILIFU, kwa maana hatushindi kwa nguvu zetu wenyewe, ndio maana kwenye msingi wa somo hili kuna kanuni ambayo KWANZA inamtaka mtu akae ndani ya Yesu. Ukijua kwamba “vita ni vya BWANA” na maneno ya BWANA akisema, “Mimi ni mzabibu na ninyi ni matawi..kaeni ndani yangu nami ndani yenu,…. pasimo Mimi hamuwezi neno lolote”, utaelewa kwa urahisi sana somo hili.
Daudi alikuwa mshindi sana katika maisha yake, haimaanishi alikuwa hafanyi makosa, hapana, Daudi alikuwa mwanadamu kama ilivyo kwa mimi na wewe. Daudi alijua kumtegemea Mungu sana na mnyeyekevu. Zaidi sana, Daudi alikuwa MWEMA, hata kwa adui zake. Ngoja nikwambie jambo, kutenda wema sio mpaka uombwe, mtu mwema HUTAFUTA kutenda wema. Mara nyingi sana katika maisha yetu tumeacha kufanya wema kwa watu, eti, kwa sababu hawajatuomba au kutuuliza! Kuna mambo mawili ya kijifunza kwa habari ya UOVU ili uweze kuelewa maana ya kuwa mwema. Kwanza, kuna kulipiza kisasi kwa adui zetu, na pili, kuacha mabaya yampate mtu bila msaada. Daudi alijitahidi kushinda katika haya yote mawili.
Hebu fikiri tu, Mfalme Sauli alianza vita na Daudi kwa sababu ya wivu wake, kisa, Daudi anafanikiwa sana, watu wanampenda, nk., Sauli akakasirika akaanza vita na kutaka kumwangamiza Daudi. Angalia jambo hili, katika maisha ya KILA mtu, iwe ni kazini, shuleni, familia, nk., wapo watu wataamua kukuchukia tu na kuanza vita dhidi yako. Kila ukijiuliza umefanya nini huoni sababu. Sikiliza Neno la BWANA, hayo nayo hayana budi kutokea. Yamkini huyo jamaa ameibuka ili Mungu aweze kupima wema wako. Angalia usifanye vita juu yake, na kama ilivyokuwa Daudi kwa Sauli, tafuta nafasi ya kumtendea wema huyu adui yako, ili ajue kwamba yuko Mungu katikati ya wanadamu ambaye amesema “kisasi ni juu yangu” na “humlipa kila mtu sawa na matendo yake”. Ona tena, ukifanya matendo ya wema kwa adui yako, Mungu atalipa wema kwako kwa maana “kila apandacho mtu huvuna”; na adui yako akifanya vita juu yako, atapambana na Mungu wako kwa maana “vita ni vya BWANA”, Mungu atamlipa sawa na matendo yake maovu. Kazi yako ni “kuipisha ghadhabu ya Mungu”, usimsaidie Mungu kushughulika na adui zako, wala USIWAOMBEE mabaya, Mungu anajua kazi yake vyema. Ukifanikiwa hapo, utaanza kuona unakuwa mshindi kwa maana ushindi wetu unatoka kwa BWANA.
Angalia sifa hii ya Daudi, pamoja na kupata nafasi ya kumkata kichwa adui yake Sauli akiwa amelala, Daudi aliacha tu; na aliposikia Sauli amekufa, walioleta habari kwamba Sauli amekufa huku wanafurahi, Daudi aliwauwa! Yaani alikasirika hata mabaya yalipompata Sauli! Hakutaka afe tu, Daudi akaomboleza na kulia mbele za BWANA kumlilia Sauli kwa sababu amekufa! Ona jambo hili, baada ya kufa Sauli, Daudi anaona hakufanya wema wa kutosha kwa Sauli, sasa anatafuta mtu katika nyumba ya Sauli, ili afanye wema wa BWANA juu yake! Huyu ni Daudi mwana wa Yese, mtu mkuu sana na mshindi sana, ila alijua KANUNI za kuwa MSHINDI, akafanya kwa mkono ulio hodari, akashinda na kiti chake kingali imara, japo amepumzika na baba zake. Sikiliza, wewe unaweza kuoza na kuliwa na funza huko kaburini, lakini wema wako hautaoza kamwe; wema wako utapiga kelele japo wewe umekufa.
Liko jambo nimeliona juu ya nchi, nalo ni mzigo mzito na ujinga mkuu; kumchukia mtu kwa sababu ya kosa la mwingine! Yaani unakasirishwa na mtu mmoja sasa unaamua kuchukia familia nzima, au ukoo mzima au hata kabila zima na nchi pia, kwa sababu yuko mtu katika jamii hiyo amekukwaza! Daudi alijua kutofautisha baina ya mtu na mtu. Aliyekuwa adui yake ni Sauli, sio watu wote wa nyumba yake, ndio maana alizidi kuwa rafiki wa Yonathani, na hata sasa Yonathani ajapo kufa, bado Daudi anaona sababu ya kuzidi kutenda mema juu ya nyumba ya Yonathani mwana wa Daudi na kurudisha mali za adui yake Sauli zilizotekwa nyara au kuibiwa. Kumbuka, huyu ni Sauli ambaye alimnyang’anya Daudi mke, licha ya kutaka kumuua mara kadhaa tena kwa mkono wake mwenyewe. Daudi alikuwa na sababu elf za kumchukia Sauli lakini alichunga sana moyo wake asifanye jambo baya ila kurudisha wema tu, kwa njia hii ni sawa na kumpalia Sauli mkaa wa moto kichwani mwake.
Frank Philip.

Comments