KUUSHINDA ULIMWENGU – V

Na Frank Philip.
“Kwa kuwa nitakapokwisha kuwatia katika nchi niliyowaapia baba zao, imiminikayo maziwa na asali; nao watakapokwisha kula na kushiba, na kuwanda; ndipo watakapoigeukia hiyo miungu mingine, na kuitumikia, na kunidharau mimi, na kulivunja agano langu” Kumbukumbu la Torati 31:20.
Katika mfululizo wa somo hili, tumeona kanuni za kuushinda ulimwengu ambazo ni kuwa ndani ya Kristo, kuwa mtendaji wa Neno, na Kujilinda. Pamoja na mambo mengine, tumeona pia umihimu wa unyeyekevu, kumtegemea Mungu na jinsi itupasavyo kuwatendea watu wengine ikiwemo na adui zetu.
Mara nyingi watu hufikiri adui zao ni Ibilisi na wanadamu bila kujua adui mkubwa kabisa kuliko hao wawili ni mtu mwenyewe. Yaani mwili wako unageuka kinyume na roho yako, unashindwa kutenda mapenzi ya Mungu kisha unaangamia. Hili jambo sio kwako na kwangu tu ila hata BWANA alifika mahali pa kusema “roho iradhi lakini mwili ni dhaifu”.
Katika somo hili, nakuletea jambo moja ambalo linaitwa MAFANIKIO ya kimwili. Mara nyingi utawasikia vijana/watu wakijifariji kwa maneno haya, “nikioa/olewa nitaweza kushinda zinaa”, “nikipata kazi nzuri nitatoa fungu la 10 bila shida”, “nikimaliza kujenga nyumba yangu nitaweza kusaidia wahitaji bila shida”, “nikipona kwenye hii shida nitamtumikia Mungu”, nk. Mara nyingi watu wamesahu kwamba KIPIMO cha WEMA wako au UAMINIFU wako sio katika WINGI na ZIADA ya mali zako, ila katika KUPUNGUKIWA kwako. Ndio maana ule mfano BWANA aliotufundisha kwa habari ya TALANTA, alisema, “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.” (Matayo 25:21). Watu wengi bado wamo katika shida zao na mateso katika hali za maisha yao, pamoja na kwamba wameokoka vizuri tu, kumbe! Hawakujua kwamba ili KUUSHINDA ULIMWENGU ni pamoja na kuwa MWAMINIFU na MWAJIBIKAJI katika kutii Neno hata katika KUPUNGUKIWA ndipo kunatokea KUONGEZWA na KUINULIWA. Hii kanuni ya “mwaminifu katika vichache anapewa vingi” sio ya dunia hii bali ni ya Mungu.
Angalia jambo hili, Wana wa Israel walipokuwa jangwani, kwenye upungufu mkubwa, yamkini walisema “tukifika mahali hii shida ya jangwani ikiisha, tutamshukuru Mungu na kumtumikia”. Kinyume chake, waligeuka na kuabudu sanamu. Ona sasa, hata leo bado jambo hili limo katikati yetu.
Ukitaka kuelewa jambo hili kwa wepesi, mfananishe Adamu wa kwanza na Adamu wa pili. Adamu wa kwanza alimkosea Mungu akiwa katika bustani ya Eden yenye kila kitu, na Adamu wa pili alipokuja, alifanikiwa kutenda mapenzi ya Mungu na hakutenda dhambi japo “ilikuwa afadhali ndege wa angani kwa maana wana viota, na mbweha kwa maana wana mashimo ya kuishi, Yeye alikuwa hana mahali pa kulaza kichwa chake”. Ukimwangalia BWANA kwenye maandiko, utaona picha ya mtu aliyekataliwa, dharauliwa na wenye mamlaka na asiyekuwa na cheo wala mali, ila alisimama katika kusudi la Mungu katika hali hiyo hadi akafika mahali pa kusema “Mimi nimeushida ulimwengu”.
Nikisema mambo hayo, jifunze neno hili, “mafunzo mazuri ya Mungu ni pale uwapo nyikani, na USHINDI uliotukuka ni ule wa JANGWANI, mahali pa kupungukiwa”. Fikiri tu, Mungu aliweza kuleta magari ya moto (kwa mfano wa lile lililo mchukua Eliya) kuwavusha taifa lake teule kutoka Misri ili wasiteseke njiani, lakini alichagua watembee kwa miguu wao na watoto wao na wake zao ikiwemo na wajawazito pamoja na mizigo yao kichwani. Tazama, hii njia mimi naiita “darasa jangwani”, iko shule Mungu anakupitisha katika KUPUNGUKIWA kwako, angalia usipitwe na shule hiyo wala kufeli mitihani yake maana hiyo ndio itakufanya uwe MSHINDI katika ULIMWENGU huu na ni SIRI ya KUONGEZEKA kwako.
Frank Philip.

Comments