MAISHA YA WANAFUNZI WA KWELI WA YESU KRISTO.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tule chakula cha uzima.

Wateule wa YESU kwa jina jingine huitwa Wanafunzi wa YESU(Matendo 11:26,  …. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.).

Wanafunzi wa YESU lazima wawe wamejifunza kwa YESU kupitia Neno lake Biblia, Tena wakidumu katika neno lake na kulishika na kulitii (Yohana 8:31-32,  Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;  tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.).

Wanafunzi wa YESU ni wale walioivaa nira yake(Mathayo 11:29-30,  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.).

Hizo ni sifa za wanafunzi wa YESU lakini zipo tabia pia za wanafunzi wa YESU na yapo maisha pia ambayo wanatakiwa kuishi wanafunzi wa YESU.

-Tabia njema ni jambo la muhimu sana kwa kila mwanafunzi wa YESU.
-Mwana wa MUNGU ni Yule tu anayemheshimu MUNGU.
-Tabia mbaya inaweza kuwa kikwazo  cha watu wengine kuokolewa. Ziko nyingi ila Leo nazungumzia maisha ya wanafunzi wa YESU.


MAISHA  YA WANAFUNZI WA  KWELI WA YESU KRISTO.


   1.Huushinda ulimwengu (1 Yohana 5:4, Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na MUNGU huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.   ). 
Kuushinda ulimwengu ni kushinda dhambi, kushinda mambo ya kidunia yaliyo machukizo kwa MUNGU na kuwashinda mawakala wa shetani wote.

    2.  Hujitenga na anasa za dunia(1 Yohana 2:15-17, Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia.  Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.  )

    3.   Hawaendi katika njia ya wasio haki na wala hawakai barazani pa wenye mizaha( Zaburi 1:1-3 , Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.  Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.). Shauri la wasio haki ni kwenye mambo au vikao vya watu wanaopanga mabaya, ni kwenye ajenda za kupinga Wokovu. Njia ya wakosaji ni kwenye mambo yote ya dhambi, baraza la wenye mizaha ni kwa wanaokejeli injili na ukombozi wa Mwanadamu kupitia YESU KRISTO.

   4.  Ni waombaji(Waefeso 6:18,  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;).
 Maombi ni maisha, maombi ni mkono mrefu zaidi wa kupokea kutoka kwa MUNGU. 
Maombi huwaweka huru watu, maombi ni maisha ya waenda mbinguni

 5.  Humtumikia MUNGU(Yoshua 24:14-15, Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.). Ni heri kumtumikia BWANA MUNGU. Wanafunzi wa kweli wa YESU KRISTO humtumika MUNGU tu. Hujiepusha na miungu na sanamu zote, hujepusha na usoma nyota, unajimu, mizimu na kila machukizo.

       6.  Huongozwa na  ROHO MTAKATIFU(Warumi 8:14, Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.). Wanafunzi wa YESU huongozwa na ROHO MTAKATIFU. 
ROHO hutukumbusha, hutufariji, hutufundisha, hutuonya, hutuelekeza na hutufunulia tusiyoyajua na hata mafumbo ya MUNGU.  ROHO MTAKATIFU ni muhimu kuliko vyote kwa mteule wa MUNGU.

 7.  Huishi maisha matakatifu(Wakolosai 1:21-22, Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, WATAKATIFU, wasio na mawaa wala lawama;)

Manafunzi anaambiwa hivi  ‘’katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.- Tito 2:7-8’’
Ndugu yangu, hakikisha unakuwa mwanafunzi wa kweli wa YESU kwa kumtii MUNGU. 
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments