MAJINA SABA(7) YA HESHIMA YA WATEULE WA KRISTO.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tena tujifunze habari njema za MUNGU aliye hai.

Warumi 8:1-2 ‘’ Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU.  Kwa sababu sheria ya ROHO wa uzima ule ulio katika KRISTO YESU imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. ‘’

Leo tunazungumzia majina 7 ya heshima ya wateule wa MUNGU. Sio kwamba majina haya tu saba ndio yapo kwa ajili ya waenda mbinguni bali kuna majina mengi tu. Nimeandika majina saba kama tu yalivyoandikwa katika 1 Petro 2:9. Sio kwamba wakristo wote ni wateule wa KRISTO bali wale tu waliokombolewa kwa damu ya YESU na kuukulia wokovu kwa mafundisho katika makanisa sahihi ya kiroho.

1 Petro 2:9-10 ‘’ Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.  ‘’

Kutokana na maandiko hapo juu tunatambua kwamba Wateule wa MUNGU ni;

-Mzao mteule

-Makuhani wa kifalme.

-Taifa takatifu.

-Watu wa milki ya MUNGU.

-Watangaza fadhili za MUNGU.

-Tulioitwa na MUNGU kutoka gizani na kwenda kwenye uzima wake.

-Tuko kwenye nuru yake ya ajabu.

1.   MZAO MTEULE.

Wateule wa KRISTO wanaitwa mzao mteule kwa sababu wamezaliwa kiroho na MUNGU ‘’Yohana 1:13,  waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.’’  Pia Biblia inaendelea kusema kwamba bila kuzaliwa upya au kuzaliwa mara ya pili haiwezekani kuurithi ufalme wa MUNGU Hivyo hawa kuitwa mzao mteule ni haki yao kabisa maana Yohana 3:5-6 Inasema ‘’ YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa ROHO ni roho.  ‘’. MUNGU ametuita na kutukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa(1 Petro 1:3)

2.   MAKUHANI WA KIFALME.

Wateule wa MUNGU pia wanaitwa makuhani wa kifalme kwa sababu MUNGU mwenyewe anasema ‘’ nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.  -Kutoka 19:6’’

Moja ya sifa za kuhani wa JEHOVAH MUNGU wetu ni hizi;

-Uaminifu(1 Samweli 2:35)

-Wana sheria ya MUNGU(Yeremia 18:18)

-Wamehifadhi maarifa ya Kimungu(Malaki 2:7)

Hizo ni sifa za makuhani na makuhani wa kifalme ambao ni wateule wa BWANA YESU wana sifa hizo na zaidi,  Pia ni makuhani wa kifalme kwa sababu wamempokea MFALME wa wafalme yaani YESU KRISTO. Ufunuo 1:5-8 ‘’ tena zitokazo kwa YESU KRISTO, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa MUNGU, naye ni BABA yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema BWANA MUNGU, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi. ‘’

3.  TAIFA TAKATIFU.

Wateule ni taifa takatifu kwa sababu wanaishi maisha ya  utakatifu kama atakavyo MUNGU.   Wakolosai 1:21-22 ‘’  Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;  ‘

BWANA ni mtakatifu na aliyeungwa roho moja na BWANA lazima tu naye awe mtakatifu, 1 Kor 6:17 ‘’ Lakini yeye aliyeungwa na BWANA ni roho moja naye.  ‘’ Ni heshima kuu MUNGU Bamteupa sisi wateule wake. Waefeso 2:20 -22 ‘’  Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake MUNGU. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.  Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya MUNGU katika ROHO.  ‘’

4.   WATU WA MILKI YA MUNGU.

Wateule ni watu wa milki ya MUNGU kwa sababu Wanaliishi kusudi la MUNGU, Wameokoka Waefeso 2:8 ‘’ Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU.‘’ KRISTO ametuokoa na na yeye anamilki milele. Ufunuo 11:15 ‘’ Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa BWANA wetu na wa KRISTO wake, naye atamiliki hata milele na milele.   ‘’

5.   WATANGAZA FADHILI ZA MUNGU.

Wateule ni muhimu sana kwa MUNGU maana wanatangaza fadhili za MUNGU hapa duniani Zaburi 103:17 ‘’ Bali fadhili za BWANA zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana; ‘’ Watu wanamjua MUNGU wa kweli kupitia wateule wake. Zaburi 96:2-7 ‘’ Mwimbieni BWANA, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.  Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu.  Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA  utukufu na nguvu. ‘’. Tu wajumbe kwa ajili ya KRISTO(2 Kor 5:20-21)

6.    TULIOITWA NA MUNGU KUTOKA GIZANI NA KWENDA KWENYE UZIMA WAKE.

MUNGU mwenyewe ni nuru na anatutaka wateule wake tuwe nuruni siku zote 1 Yohana 1:5-7 ‘’ Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.  ‘’ Pia Biblia inaendelea kusema kwamba tumetoka gizani na sasa tuko nuruni kwenye uzima wa BWANA . 1 Yohana 3:13-14 ‘’ Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia.  Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.  ‘’

7.   TUKO KWENYE NURU YA AJABU.

Tuko kwenye nuru ya BWANA YESU, Waefeso 5:8 ‘’ Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika BWANA; enendeni kama watoto wa nuru,  ‘’

YESU ni nuru(Yohana 8:12) na ametufanya na sisi wateule wake kuwa Nuru ya ulimwengu. Mathayo 5:14-16 ‘’ Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.  Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze BABA  yenu aliye mbinguni.  ‘’

Naamini umejifunza mambo mazuri sana kukuhusu wewe mteule mwenzangu wa KRISTO na pia Yule ambaye bado hajampokea YESU kama BWANA na MWOKOZI wake siku ya kufanya hivyo ndugu naomba uifanye iwe leo maana zamani hizi ni za maovu mengi. Mimi mteule ‘’ Nimesulibiwa pamoja na KRISTO; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali KRISTO yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa MUNGU, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.   Wagalatia 2:20) 
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.

Comments