MFALME WA WAFALME

Na Frank Philip
Mara nyingi huwa najiuliza maana ya kuwa mfalme ni nini. Kwanini rais wa nchi ni tofauti na mfalme? Angalia hapa, wote ni watawala ila kwa majina yao tu unaanza kupata picha tofauti kwa habari ya mamlaka zao au hata mfumo wa maisha yao.
Nimewahi kutembelea nchi mbali mbali ambazo ni falme, yaani kiongozi mkuu wa nchi sio rais ila ni mfalme. Katika nchi moja nilimfananisha ndugu mmoja na picha ya mfalme kwa sababu walifanana sana. Nilidhani yule ndugu angeona ni kawaida au hata kufurahi kufanana na mfalme, badala yake alinikemea vikali na kuniambia "picha ya mfalme huwezi kuinenea maneno tu, wala kuinyoshea vidole, tena sio vizuri kumtaja mfalme hovyo, hii inaweza kunisababishia matatizo". Kwa mara ya kwanza nikaanza kusikia UTISHO wa mfalme wa nchi hiyo. Jambo la msingi ninalotaka kusema ni hali ya kuwa na HOFU ya mfalme hata kama hayupo kwa jinsi ya mwili au muonekano wa macho ya damu na nyama.
Nikasikia simulizi za hawa wafalme mbali mbali, nikajifunza kwamba NENO la mfale ni kama SHERIA, hakuna mtu ananyanyua kinywa kusema kinyume na mfalme au kupingana na amri ya mfalme, labda awe amechoka kuishi. Katika kutafakari kwangu nikaanza kutizama UFALME wa Mungu wetu. Yeye ni Mfalme, na ana amri zake na maagizo ambayo ANAPENDA tuyafuate. Sifa za wafalme wote ni kupenda KUSIKILIZWA na KUHESHIMIWA. Nikazidi kujiuliza, hivi Mungu anasikilizwa na kuheshimiwa maishani mwangu kama Mfalme? Kwa mara ya kwanza baada ya kuona mambo makuu sana ya Mfalme ambaye ni juu ya wafalme wote, na ni BWANA wa mabwana, ndipo nikawa na hofu zaidi na hata mara nyingi kushindwa kuita hovyo jina ja Yesu. Nikajikuta naita BWANA kwa urahisi kuliko kuita Yesu. Nikaanza kuona kwa mara ya kwanza ni kwanini kuna amri inasema "usilitaje BURE jina la Bwana Mungu wako, kwa maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure"! Nikaona tena kwa wazi sababu ya kupewa amri hii, yaani huwezi kutaja jina la MFALME mkuu sana kwa mzaha tu; Anahitaji heshima yake ambayo Yohana mbatizaji alipoiona, japo kwa mbali alisema, "sistahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake".
Petro akijua ukuu na heshima ya BWANA, akakataa kunawishwa miguu yake hadi BWANA aliposisitiza; na ilipofika mahali pa kuuwawa msalabani kwa sababu ya imani yake kwa BWANA, Petro alisema, "sawa nakubali kufa kwa ajili ya BWANA wangu, sitamkana tena kama mwanzo, ila SISTAHILI kusulubiwa kichwa juu kama BWANA, nisulubisheni kichwa-chini-miguu-juu", Petro akafa kichwa chake kikielekea ardhi kwa maaana alimheshimu sana BWANA. Je! Umeona jambo hili katika mwili wa Kristo, kwamba mambo ya BWANA sio kitu tena cha kuangalia? Ona jinsi ambavyo wengi wanafanya mambo yasiyopaswa ikwa sababu ya HOFU ya WANADAMU tu na wala sio hofu ya Mungu, wao wameogopa "wauao mwili tu" na kumdharau "Yeye awezaye kuua mwili na kisha kutupa roho yake motoni"! Angalia heshima unayompa bosi wako kazini hata unamkosea Mungu kwa ajili yake, na mara nyingi unakubali amri zote tu hata kama utafarakana na familia yako, kwa sababu hutaki kumkorofisha bosi! Je! Ni yupi mkuu kati ya bosi wako na Mungu wako? Je! Hilo nalo ni jambo dogo?
Kama umeweza kuona UKUU wa Mungu wako, na HESHIMA yake kama BWANA na Mfalme, mpe heshima yake, hata kama humwoni kwa jinsi ya mwilini, jua yupo, na anakuona. Ukitaka kujifunza itupasavyo kumheshimu Mungu jifunze kwa adhabu ya Musa mtumwa wa Mungu, "hakumstahi BWANA mbele ya wana wa Israel", Musa akaadhibiwa asiingie nchi ya ahadi baada ya kufanya kazi ngumu usiku na mchana ya kusafiri jangwani na kundi la watu wakaidi na wasumbufu sana. Musa hakutenda dhambi ila kushindwa "kumstahi BWANA" mbele za watu!
Frank Philip.

Comments