MIMI, NINYI NI NURU YA ULIMWENGU.

BWANA YESU atukuzwe  ndugu zangu.
Karibuni tujifunze habari za nuru ya uzima.
MUNGU anawapenda sana wateule wake. Na MUNGU huwatumia watu wake katika kulitimiza kusudi lake la wokovu kwa watu wote.
 ili MUNGU atutumie lazima tuwe Nuru iliyozaliwa kiroho na nuru yake MUNGU mwenyewe. MUNGU ni nuru na anatutaka sisi wateule wake kuwa nuru ulimwenguni.
Nuru kazi yake ni kuangaza ili watu wengine wapate kuona matendo yetu mema.
Kwa watumishi wa kweli wa MUNGU iko hivi   ''Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema-Wafilipi 2:13'' 
Ndugu zangu, ili MUNGU atutumie katika kazi yake ya kuwaokoa watu lazima tuwe katika utii wa kumtii YESU pia lazima tuenende nuruni kama yeye BWANA wetu alivyo nuruni.
Nuru ya MUNGU ni muhimu sana na tunatakiwa tuangaze kama nuru sahihi ya ulimwengu.
Matendo yetu ni nuru inayowamlikia watu wapate kuona jinsi ipasavyo kuishi. Ndugu zangu, MUNGU ni nuru na anatutaka sisi wateule wake tuwe nuru ulimwenguni.  

Tunatakiwa tuwe nuru kwa sababu zifuatazo:

     1.  MUNGU Ni Nuru(1 Yohana 1:5-7 '' Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;  bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
-MUNGU Anaangaza Kupitia Neno Lake. 
-MUNGU anaangaza kupitia matendo yake makuu.

    2. YESU KRISTO Ni Nuru ya ulimwengu (Yohana 8:12,  Basi YESU akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
-YESU ni nuru, ukiifuata nuru hii hutaingia gizani kamwe.
-YESU Alikuja Duniani Kututoa Gizani Ili Atupeleke Kwenye Nuru Yake Ya Ajabu. 
 -Ndugu Mpokee YESU Aliye Nuru Ya Uzima.

     3.  ROHO MTAKATIFU ni nuru (Warumi 8:14, Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.
-ROHO MTAKATIFU ndio ROHO wa MUNGU.
-MUNGU ni nuru na ROHO wake vilevile ni nuru maana haiwezekani MUNGU awe nuru harafu ROHO wa MUNGU asiwe nuru, haiwezekani, Hivyo wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU hao ndio wana wa MUNGU.
-ROHO MTAKATIFU Ni Nuru Anaangaza Mioyoni Mwetu Na Kutufanya Tutende Matendo Ya Nuruni.


      4.  Sii wateule  Ni Nuru Ya Ulimwengu (Mathayo 5:14-16, Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze BABA yenu aliye mbinguni. )
-Wateule ni nuru tunamlikia Watu Ili Wapate Kuona Matendo Yenu Mema
-Nuru Kazi Yake Ni Kuangaza Ili Wengine Wapate Kuona.

- Matendo yetu mema ndio sababu kuu ya MUNGU BABA kutukuzwa.

Ndugu hakikisha unakuwa nuru ya ulimwengu.
Kama unafanya dhambi kwa siri acha mara moja, na kama unafanya wema machoni kwa watu ili utazamwe na wao na waseme hakika wewe ni nuru ya ulimwengu ndugu yangu hiyo ni kazi bure na ni kazi ya hasara kuu maana unaweza kuukosa uzima wa milele.




Ndugu zangu Tuenende Nuruni Kama Ambavyo BWANA Wetu Ni Wa Nuruni(1 Yohana 1:7,
bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. ). 

Pia tukumbuke kwamba  Hukumu Ni Kwa Wale Walioikataa Nuru Hii Ya Uzima Yohana 3:19-21''  Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa NURU imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko NURU; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye NURU, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye NURU, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.   ''
Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292

Comments