MWIMBA Injili anayekuja kwa kasi Bongo, Elizabeth
Ngaiza, Jumamosi iliyopita alijikuta katika wakati mgumu kufuatia watu
wasiojulikana kumuweka chini ya ulinzi kwa dakika kadhaa wakitaka awape
pesa ndani ya gari aina ya Toyota Vitz (pichani juu).

Mwimba Injili anayekuja kwa kasi Bongo, Elizabeth Ngaiza.
Kwa mujibu wa Elizabeth mwenyewe, tukio hilo lilijiri Babarara ya
Kilwa, Dar maeneo ya Mivinjeni akitokea Temeke kwenda Posta Mpya
kusambaza albamu yake iitwayo Sema Nao Bwana.
“Nilipofika maeneo ya Mivinjeni majira ya mchana, nikasimamishwa na watu waliokuwa wamesimama pembeni ya barabara, nikajua wananifahamu maana mimi ni mwimba Injili, wakaomba kuingia kwenye gari, nikasema sawa, walipoingia wakasema niko chini ya ulinzi mpaka nitoe pesa.
“Nilishtuka sana, mmoja alikuwa na kisu cha kukunja, mwingine hakuwa
na silaha. Niliwaambia sina pesa, wakasema watanifanyia kitu kibaya.
Ilibidi niwape elfu ishirini, wakashuka,” alisema Eliza huku akikiri
kutotoa taarifa polisi zaidi ya kusali na kumshukuru Mungu wake.
Comments