MWENDEE ADUI KWA JINA LA YESU KRISTO UTASHINDA.





BWANA YESU asifiwe.
Karibu tujifunze.





1 Samweli 17:45-46 ''Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. ''

1-Nakujia kwa jina la BWANA MUNGU
2-BWANA atakuua mikononi mwangu.
3-Dunia nzima watajua kwamba yuko MUNGU katika wateule.
4-BWANA haokoi kwa upanga na mikuki ya kibinadamu.
5- Vita ni ya BWANA.

''Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike. [Kumbukumbu la Torati 31:8]''

Ndugu,Hakikisha unatumia vigezo hivyo vitatu ili kuwashinda maadui zako.
-Wafuate kwa jina la YESU KRISTO kupitia maombi.
-Nenda kwa imani kuu ukiamini kwamba BWANA atawaua maadui zako kupitia wewe mwenywe kwa maombi yako.''Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu. [Zaburi 143:8]''
-MUNGU atatukuzwa baada ya kukushindia. Mpe MUNGU utukufu wote.
''Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, MUNGU wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia. [Yoshua 23:10]''
-MUNGU haokoi kwa upanga na mikuki, MUNGU anaokoa kwa njia aitakayo yeye. unaweza kujiuliza ndani ya jiwe alilorusha Daudi kulikuwa na nini? Yawezekana kabisa kulikuwa na moto wa ROHO MTAKATIFU, Yawezekana kabisa kulikuwa na nguvu kubwa sana ya MUNGU maana Daudi alikiri kwamba anamfuata mfilisti yule kwa jina la BWANA MUNGU wa majeshi. Yawezekana kabisa ndani ya jiwe la Daudi kulikuwa na nyundo ya kuweza kuangusha ghorofa. Yawezekana hata kabla jiwe la Daudi halijamfikia Goliathi tayari malaika wa BWANA alikuwa kashampiga goliathi. Hatujui kulikuwa na nini lakini kama tukiamua vita yetu iwe vita ya BWANA hakika yeye ana njia maelfu ya kutusaidia.
Daudi alibeba mawe matano(1 Samweli 17:40) na kuna huduma tano za ROHO MTAKATIFU. Kwa huduma 5 za ROHO MTAKTIFU lazima kanisa lishinde, lazima shetani akimbie.Njia za MUNGU hazichunguziki.''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo(YESU), na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. [Ufunuo wa Yohana 12:11]''

Je adui yako ni nani?
Je uko tayari kumwendea kwa jina la YESU KRISTO?
Je MUNGU akikushindia uko tayari kumpa utukufu wote?
''Nafsi yangu, umngoje MUNGU peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. [Zaburi 62:5]''

Ndugu zangu Wateule wa BWANA YESU ni muhimu sana kumtegemea MUNGU katika vita tunavyokutananavyo. ukimtegemea MUNGU hakika atawaharibu watesi wako wachawi, majini, mizimu na watu wabaya maana MUNGU anataka kutukuzwa kupitia wewe na dunia nzima watajua kwamba MUNGU yuko.
''Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. [Mithali 3:5, 6]''
Usiwaogope maadui bali mwite BWANA YESU ili akushindie. yeye haji kukusaidia bali anakuja kukushindia tu.

Usiogope ukubwa wa adui yako bali kimbilia upande wenye nguvu ndipo utashinda. Mkimbilie BWANA YESU na utakaa salama.
Wateule wa MUNGU humtegemea MUNGU.

BWANA YESU anasema ''Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. [Yohana 15:5]''
-Ndugu pasipo YESU huwezi kufanya lolote.
-Pasipo YESU huwezi kushinda. Mwite yeye akushindie.

''BWANA ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina. [2 Timotheo 4:18]''

Haijalishi maadui zako ni wengi kiasi gani. yawezekana una maadui magonjwa, madeni, kuteswa katika ndoa yako. yawezekana adui yako ni kila ukichumbiwa unaachwa au yawezekana adui yako ni kuonewa kwa sababu tu ya ulemavu au unyonge. Ndugu yangu napenga kukutia moyo kwamba liko tumaini kwa BWANA YESU, uko msaada kwa MUNGU wa israeli. Kwake hakuna kushindwa wala kusitasita. kwake kuna uzima sasa kisha uzima wa milele.
''Hata twathubutu kusema, BWANA ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? [Waebrania 13:6]''

Jina la YESU ni mwisho wa wewe kuonewa na kunyanyaswa. kwa jina la YESU maadui wote hukimbia na wengine hufa kabisa. Ndugu mkimbilie BWANA YESU na utakaa salama.''Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; [Waefeso 3:20]''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments