NI KWELI UMEFANYA SIRI ILI WANADAMU WASIJUE, NA MUNGU JE?

BWANA YESU atukuzwe sana ndugu.
Karibu tujifunze jambo muhimu.  
Mithali 15:3 ''Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.''
Kama macho ya MUNGU yako kila mahali yakichunguza kila jambo alifanyalo mwanadamu je kuna siri kwa MUNGU.
 
Ni Kweli Umefanya Siri Ili Wanadamu Wasijue, Na MUNGU Je?. 
Kuna vitu vingi ambavyo baadhi ya watu huvitenda sirini. Huona ni amani kutenda maana taa ya ROHO MTAKATIFU ilishazima ndani yao siku nyingi, hata hawaogopi tena kufanya dhambi hiyo ila wanaogopa tu wanadamu wanaowazunguka wasijue. Watu hawa wakati mwingine ni washirika kabisa wa makanisa na kila ibada wanahudhuria, wanajifunza neno ila wao ni wasikiaji tu wa neno na sio watendaji wa kukitendea kile walichokisikia kanisani. BWANA anawavumilia kwa muda labda watashituka na kutubu lakini wameshupaza shingo zao. Watu hawa ni magugu yaliyo katika shamba moja na ngano, BWANA maana ndio mwenye shamba amesema tu kwamba ''Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.-Mathayo 13:30''
 Magugu ni watenda dhambi na ngano ni wateule.
Je wewe ni nani? Gugu au ngano?

-Ndugu yangu,Unaweza Kujificha Kwa Wanadamu Wote Na Inawezekana Kabisa Kila Mtu Akiulizwa Ataje Watakatifu 3 Tu Anaowajua Atakutaja Wewe Kama Wa Kwanza Wao. 
-Ni Kweli Wanadamu Wanajua Kwamba Wewe Ni Mwema Sana Hata Kama Kiuhalisia Wewe Ni Muovu Sana. 

Huwezi Kujificha Kwa MUNGU(Mithali 15:3). 
-Kama Huwezi Kujificha Unasubiri Nini Kutubu? 
MUNGU Hukuona Kokote Ulipo(Zaburi 139:7-8,12 ''Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. ).
Ndugu yangu, hakuna pa kuukimbia uso wa MUNGU, Hata gizani MUNGU huona kama tu anavyoona kwenye mwanga.
 -Kama BWANA Hukuona Popote Ulipo Je Unasubiri Nini Kutubu? BWANA YESU Anasema Hakuna Neno La Siri Ambalo Halitafunuliwa(Luka 8:17 '' Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. ). 
Hakuna neno la siri ambalo halitawekwa wazi.
Hata ungejificha kwa kufanya uzinzi ipo siku kila kitu kitakuwa wazi yawezekana ukimwi utakuumbua, yawezekana mimba itakuumbua na siku ya hukumu ndio kila kitu kitakuwa wazi kama hukutubu.
-Ndugu Yangu Kama Kila Ukifanyacho Kitakuwa Wazi Je Unaficha Nini? 
-Na Je Utatubu Lini? Maana Ukitubu Kwa MUNGU Katika KRISTO Dhambi Zako Zinafutwa Na Utakuwa Umesamehewa(Isaya 55:6-7 ''Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. ). 
Ndugu yangu, Hata Gizani MUNGU Anakuona(Ayubu 34:21-22 ''Kwani macho yake ya juu ya njia za mtu, Naye huiona miendo yake yote. Hapana weusi, wala hilo giza tupu, Wawezapo kujificha watendao udhalimu. ). 

-Kama Popote MUNGU Anakuona Unasubiri Nini Kugeuka Na Kutubu?. 
Hakuna Mahali Pa Siri Kwa MUNGU Huona Kila Mahali(Yeremia 23:24 '' Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema BWANA. ). 
-Je Uko Gesti Gani Hata MUNGU Asikuone? 
-Unaiba Wapi Ambako MUNGU Hatakuona? 
-Uongo Wote BWANA Anaona.
Ni dhambi gani ya siri ambayo unadhani MUNGU hatakuona?
Ndugu yangu hakuna dhambi ya siri ambayo MUNGU hatakuona. Dawa ni kutubu tu na BWANA YESU yuko tayari kukusamehe na kuliandika jina lako kwenye kitabu cha uzima. hakika hakuna siri kwa MUNGU. 
Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292

Comments