NINAJUA UNATAKA FEDHA, DHAHABU, MKE, MUME, WATOTO, KAZI/AJIRA, NYUMBA, GARI, N.K, LAKINI MIMI NINAKUPA YESU.


Na Godfrey Miyonjo
“Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uatwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mutu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na petro, akamkazia macho, pamoja na Yohana, akasema Tutazame sisi. Akawaangalia, akitarajia kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, MIMI SINA FEDHA WALA DHAHABU, LAKINI NILICHONACHO NDICHO NIKUPACHO. KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, SIMAMA UENDE” MATENDO 3:1-6.
BWANA YESU KRISTO wa Nazareti asifiwee.
Ninasikia kusema na watu walio na uhitaji na vitu mbalimbali katika maisha yao ya kilasiku.
Watu wanaohitaji fedha, ajira, mke, mume,watoto, nyumba, gari, chakula, N.K.
Inawezekana kuwa uhitaji wako ni wa siku nyingi, na watu wengi wamesimama ili kukusaidia kama ilivyokuwa kwa Yule kiwete.
Wapo waliokutabiria kuwa BWANA atatenda wakakupa na muda kuwa utaona matokeo, lakini haukuona matokeo yoyote.
Imefika mahali umekata tama, hata ukaona kuwa Mungu huwa hawasaidii wanadamu.
Ukaona kuwa umedanganywa, na ukawaza kugeukia miungu na kutafuta habari zako huko.
Ninataka nikwambie kuwa Mungu siyo mwanadamu hata aseme uongo, ahadi za Mungu wetu ni za kweli kabisa.
Hayo yote unayoyahitaji ni mambo mema na yanampa Mungu utukufu, Pia ni sehemu ya ahadi zake kwa watu wake.
Lakini ingekuwa heri kama ungemhitaji YESU kwanza kuliko hayo mengine.
Ukimpata YESU hayo mengine yote yatakujilia kwa wakati wa BWANA.
Usiwe kama Yule kiwete aliyekuwa anahitaji sadaka ya fedha na dhahabu kila siku asihitaji kutembea.
Hakujua kuwa angepata kutembea angekuwa na uwezo wa kujitafutia yeye mwenyewe fedha, dhahabu na vitu vingine vingi, pamoja na kuepukana na adha ya kubebwabebwa na kuwekwa mlangoni.
Hali hii aliyokuwanayo Yule kiwete ipo pia kwa wapendwa wengi hii leo,
Wengi wamekuwa ni wenye kutangatanga huku na kule kwa mitume na manabii wakitafuta miujiza juu ya uhitaji walionao.
Ewe Rafiki uliyepata neema ya kuusoma ujumbe huu, chukua hatua ya kujenga kwanza imani yako juu ya Mwamba imara (Yesu Kristo) ili uepukane na adha ya kubebwabebwa ukipelekwa huku na kule kwa mitume na manabii kutafuta miujiza.

Ndugu yakupasa ujue kuwa imeandikwa “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia” AYUBU 22:21.
Mahitaji yako yote YESU atakutimizia ikiwa tu, kama utaamua kumhitaji kwanza Yeye kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yako.
Ninasemaaaa…………………………………………….!
MKIYAJUA HAYO HERI NINYI MKIYATENDA.
Asomaye na afahamu
Wenu katika imani
Godfrey Miyonjo (Mtu wa milki ya Mungu).

Comments