SABABU ZA KUKOSEKANA KWA FURAHA NA AMANI KATIKA NDOA.



Mungu alipanga kwamba mtu anapoingia katika ndoa awe anaonja uzuri wa mbinguni na sio uchungu. Lakini kinyume chake, ndoa nyingi zimekuwa ni jehanamu ndogo. Wanandoa wana majuto, maumivu, simanzi, majeraha na hofu. Pamoja na ugumu huu, liko tumaini kwa Mungu aliyeanzisha taasisi hii ya ndoa.
Kwa utafiti wangu mdogo na kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu napenda kukushirikisha sababu za kukosekana kwa furaha na amani katika ndoa nyingi za leo:

1.Makosa katika uchaguzi wa mwenzi wa maisha.
Matatizo ya ndoa nyingi yanatokana na uchaguzi mbaya. Mungu anasema, ‘nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako’ Kum 30:19. Kama mtu alifumba macho asiangalie matatizo yanayojulikana wazi ya mchumba wake, lazima avune alichopanda. Gal 6:7 ‘Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna’. Pengine ulijua wazi tabia mbaya za mchumba wako lakini ukazipuuzia kwa vile tu ni tajiri au ni maarufu au umechoka kusubiri.
Kama Adamu hangekuwa na subira, angeoa sokwemtu kwa vile ndiye alikuwa na sura inayokaribiana na mwanadamu. Isije ikawa umeoa au kuolewa na sokwemtu kutokana na kukosa subira au kushinikizwa na watu uoe au uolewe na mtu ambaye si chaguo lako la moyo.

2.Msingi mbovu katika kuanza maisha ya ndoa.
Kama mlianza kukutana kimwili kabla ya ndoa kufungwa, lazima kuta za ndoa yenu zipate nyufa. Msingi wa ndoa yenu ni dhambi na kukosa subira ndiyo maana mnaishi kwa hatia na kutoaminiana. Tendo hilo linathibitisha kwamba mlikuwa na uwezo mdogo katika kusubiri na kutawala tamaa za miili yenu. Pia mlikosa hofu ya Mungu.
Lakini pia inawezekana mlijiheshimu katika uchumba hadi ndoa lakini hamkuandaliwa vizuri kuwa mume na mke. Ndoa ni kiwanda cha kuzalisha watu kinachohitaji meneja mzuri. Lazima wanandoa wakae chini mapema na kupanga wanataka nyumba yao iwe ya aina gani. Mjenzi hawezi kuamua baadae kuibadilisha nyumba iwe ya gorofa wakati msingi aliouweka awali ni wa nyumba ya miti.
Wengine walifichana uhalisi wa maisha yao. Pengine mume hakutaka mwenzake ajue kiwango chake cha maisha wakati wakiwa wachumba. Jambo hili linasababisha kujikwaa wakati wa kuishi pamoja. Inashindikana kumpa mke zawadi nyingi kama wakati wa uchumba kwa vile sasa hakuna wa kukukopesha. Hivyo mke anakosa hata mafuta ya kupaka. Ingekuwa bora zaidi kama mwanaume angekuwa muwazi ili mwanamke apige gharama kama ataishi naye au la badala ya kushtukizwa maisha ambayo hakuyategemea wala hakujiandaa kuwa nayo.

3.Kutegemea ndugu na kushindwa kuambatana.
Kuna wana ndoa ambao hawana maamuzi binafsi katika masuala ya nyumba zao. Kwa nje wanaonekana kama mume na mke lakini katika uhalisia ni ‘remote control’ ya ndugu zao. Kwa maneno mengine, ni bendera fuata upepo. Hawajaweza kutekeleza maagizo makuu matatu ya Mungu ya kuacha, kuambatana na kuwa mwili mmoja. Mwa 2:24 ‘Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’. Haiwezekani kuwa mwili mmoja (kuunganishwa kimwili, kiroho na kimawazo) kabla ya kuwaacha wazazi na kuambatana. Kuacha wazazi sio kuwasahau bali ni kujitegemea katika kuiongoza nyumba yako. Si lazima mfumo wako wa kuongoza ufafanane na wa wazazi wako. Kuambatana ni kuwa marafiki wa karibu kuliko yeyote mwingine. Kuna msemo unaosema, ‘Out of sight, out of mind’, yaani, ukiwa humuoni mtu kwa karibu, anaondoka mawazoni mwako. Kadiri wanandoa wanavyokuwa mbali, ndivyo kila mmoja anavyomsahau mwenzake na wakati huohuo mwingine aliye karibu anaingia moyoni kuziba pengo lililopo. Hatimaye, mlango wa zinaa unakuwa wazi.

4.Kumsahau aliyeanzisha ndoa.
Watu wengine hawamshirikishi Mungu katika kupata mwenzi wa maisha isipokuwa wanataka tu Mungu aibariki ndoa yao. Mungu alianzisha ndoa kwa malengo ya kusaidiana katika kumtumikia. Kinyume chake wengi wanadhani ndoa ni kwa ajili ya kujifurahisha tu wao wenyewe. Na hii ndiyo sababu watu wengi wakioa au kuolewa wanaacha kufanya kazi ya Mungu na matokeo yake wanaishi katika laana. Kum 28:30a, 47 ‘Utaoa mke na mtu mwingine atalala naye...kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote’. Yeyote anayetaka Mungu aiponye na kuisimamia ndoa yake ajiulize kwanza swali hili: ‘Mungu ananufaika nini na ndoa yangu?’

5.Kuthamini pesa kuliko utu (ubinadamu).
Kuna wanandoa ambao wamejenga upendo wao katika mafanikio ya kimwili. Kwa hiyo, mwenzi ana thamani kama tu ana pesa. Msingi huu unasababisha ndoa iyumbe hali ya uchumi inapobadilika. Ndoa inatakiwa ithamini mpango wa Mungu na utu kuliko kitu kingine chochote. Vinginevyo, mtu atatafuta zaidi pesa kuliko kuwa na faragha na mwenzi wake. Matokeo yake ukaribu unapungua na upweke unajitokeza tena na maana ya ndoa inatoweka. Kumbuka Mungu anawaunganisha mume na mke ili kudhibiti upweke (Mwa2:18). Kuna watu wengi siku hizi ni ‘married singles’ badala ya kuwa ‘married couples’. Yaani, mtu anaonekana kwa nje kwamba ameoa au kuolewa lakini kwa ndani yuko peke yake.

6.Kuingia katika ndoa kabla ya kujua kwamba ndoa ni majukumu.
Wapo wanaoingia katika ndoa kichwakichwa bila maandalizi ya msingi ya maisha. Mungu hakumpa Adamu mke hadi pale alipohakikisha amempa bustani ya kulima na kuitunza (Mwa 2:15-17). Ni kweli kwamba Mungu hapendi mtu awe peke yake lakini alishughulikia upweke wa Adamu baada ya kumpa kwanza bustani na majukumu. Hawa naye aliumbwa ili kumkamilisha Adamu. Ndiyo maana Mungu alitoa ubavu wa Adamu akautumia kumuumba Hawa badala ya kumuumba moja kwa moja katika udongo kusudi kila mmoja amuhitaji mwenzake.

Lazima kila mmoja ajue majukumu yake katika ndoa. Pamoja na ukweli kwamba wanandoa wanapaswa kusaidiana lazima kila mmoja ajue majukumu yake. Wapo watu wanaosema kazi zote ni za mume ikiwa ni pamoja na kupika na kudeki na mke ni msaidizi anayesaidia tu pale inapobidi. Tatizo hili linatokana na kutafsiri neno msaidizi kwa lugha ya kiswahili badala ya lugha ya kiebrania iliyotumika katika kuandika Agano la Kale. Kumbuka hata Roho Mtakatifu anaitwa pia msaidizi lakini haina maana kwamba ni mdogo kwetu wala haina maana kwamba anatusaidia tu pale tukishindwa. Roho Mtakatifu ni msaidizi kwa maana ya ‘kuwa karibu kututia nguvu ya kutenda’. Mke anayejua vizuri wito wake anatakiwa awe mfariji au muwezeshaji. Ingawa mke aliumbwa baada ya Adamu, hadhi yake ni sawa na ya mume isipokuwa tu ana majukumu yake tofauti. Kama kuumbwa kabla kunasababisha mume awe wa maana zaidi kuliko mke, basi itabidi sokwe mtu naye awe wa maana zaidi kuliko mume kwa vile aliumbwa kabla ya Adamu. Hata hivyo tusisahau kwamba mfumo dume ulianzishwa na Mungu mwenyewe ingawa hauna maana ya kumnyanyasa mwanamke. Ndiyo maana Mungu alichagua kuitwa baba na sio mama. Huu sio udhalilishaji bali ni ugawaji wa majukumu kwa utukufu wake mwenyewe. Maumbile yenyewe yanaonyesha kwamba Mungu alikusudia tofauti ziwepo kwa ajili ya mume na mke kuhitajiana. Ingawa wote wana haki sawa, mamlaka ya mume ni zaidi ya mke. Hakuna ‘authority sharing’ yaani, kugawana madaraka. Ndio maana mke akaitwa msaidizi na sio msimamizi. Opposites attract-Mtu anavutiwa zaidi na kitu asicho nacho ili akamilike. Tofauti hizi za kimaumbile ni kwa ajili ya kukamilishana na sio kushindana. 

 
Hivyo tuufurahie na kuulinda uumbaji wa Mungu wetu bila kuukosoa.
MUNGU akubariki.
 By Melchiory Kasmiry.

Comments