UUACHE MWAKA HUU NAO

Na Frank Philip
“Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate” (Luka 13:6-9).
Kila mwisho wa mwaka, hii misitari kwenye Luka 13 hunirudia kwa nguvu na kunifanya kutafakari juu ya KIASI na AINA ya matunda yanipasayo kuzaa kwa MUDA uliopangwa na BABA, (sio kwa muda niliopanga).
Kusudi la Mtini ni kuzaa TINI japo upo kati ya shamba la MIZABIBU. Hii inanionesha kwamba, kila mtu anajambo (wito) analoPASWA kufanya, mahali MAALUMU na kwa WAKATI maalumu bila kujali wengine wanafanya nini hapo pembeni. Yamkini huu mtini ulijaribu kwa miaka mitatu KUIGA kuzaa zabibu kwa sababu ulidhani unapaswa kuzaa zabibu kwakuwa umepandwa kati ya mizabibu! Mtini haukufanikiwa kitu!
Angalia jambo hili, pamoja na mipango mingi tupangayo katika maisha yetu, na matamanio ya moyo ya kila namna, je! Umewahi kujiuliza UMEITIWA kufanya nini kati ya shsamba la mizabibu? Je! Kusudi la Yesu kutuacha duniani si KUZAA matunda? Naye akiisha kujiita MZABIBU alituita sisi MATAWI ya mzabibu, na akasema KILA tawi lisilo zaa HUKATWA, na tawi lizaalo HUSAFISHWA ili lizae zaidi. Kumbuka sio kwa MUDA wako ila kwa muda wa mwenye SHAMBA ambaye ni BABA.
Unapoenda kuomba mambo mengi na unapotamani KUFANIKIWA kwenye mwaka mpya, usisahau kanuni moja ya muhimu, MAJIBU ya maombi yako yanategemea KUZAA kwako matunda, na kuzaa kwako matunda kunategemea kukaa kwako NDANI ya Yesu na KUSHIKA Neno lake (Yohana 15:1-16). Angalia hapa, “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni” (Yohana 15:16).
Ukisoma Mathayo 15:21-28, utagundua huduma sio huduma hadi ufanye sawa na ulichoagizwa, ndio maana siku ile ya hukumu wapo watu watahesabu “mambo waliyofanya kwenye huduma zao” na BWANA atasema “sikuwajua, ondokeni kwangu mtendao udhalimu”. Angalia Mwanamke Mkaanani anamlilia BWANA (Mathayo 15:21-28), anamwambia “binti yangu amepagawa sana na pepo, nisaidie”, BWANA anakaa kimya tu, anakwenda zake. Mama anakuja akipiga makelele na kumfuata BWANA kwa nyuma, hadi wanafunzi wake wanaona kero, “wakamwendea BWANA, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu”, na BWANA akawajibu akisema, “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” (specific people, place and time), wanafunzi nao wakakaa kimya. Mama akazidi kulia na kuomba na kusujudu mbele za BWANA, ndipo BWANA akamjibu baada ya muda huu wote na kusema, “si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”. Angalia jambo hili, watu wengi ni MITINI ila kwa sababu wako kwenye shamba la MIZABIBU wanakazana tu kuzaa zabibu, hata wakishindwa kuzaa zabibu, basi watajigeuza ili kufanana na mizabibu! Kama BWANA alijua MAHALI na WAKATI wa kufanya jambo, na akasema “sifanyi jambo ila li le nililoliona BABA akifanya”, na akaita MAPENZI ya BABA yake ni “chakula chake”, na kuweka NIA ya “kufanya mapenzi ya BABA yake ili ayatimize”; Kelele za huyu mama Mkaanani hazikumsumbua sana, alitazama MAPENZI ya BABA kutizama kufanya kama alivyotumwa! Jua jambo hili, hata mimi na wewe kuna mapenzi ya Mungu ambayo yamefichwa kwenye WITO wa kila mmoja, imetupasa kuyajua na KUYAFANYA ili kuyamaliza.
Nakupa shauri, huu ni mwaka mwingine tena, angalia shoka liko shinani, na mkasi uko kupunguza matawi yasiyozaa. Katika mambo yako ya MUHIMU ya kuomba na kutamani ni kufanya MAPENZI ya Mungu kwa mwaka mpya, ndipo utafanikiwa na kusitawi sana (Kumbukumbu la Torati 28:1-14). Jitahidi kusikia kwa BIDII sauti ya BWANA Mungu wako (soma neno kwa bidii na tafakari usiku na mchana), na kutizama kufanya YOTE akuagizayo kufanya (tenda sawa na hilo Neno), ndipo UTAZAA matunda SAHIHI kwa MAHALI na WAKATI sahihi.
Frank Philip.

Comments