DUNIA NA MAMBO YALIYOMO YASIKUFANYE UMWACHE MUNGU MUUMBA WAKO.



BWANA YESU atukuzwe.
karibu tujifunze.
Dunia ya leo ina mambo mengi, na mengi hayo hayana mpango wa kuhakikisha wanadamu wanampendeza muumba wao.
Wengi wa Wenye hekima ya kidunia hawana akili ya kuwaza uzima wa milele.
Wengi wa Wenye elimu ya kidunia hata hawajui kwamba ipo siku wataondoka na elimu zao.
Matajiri wengi wa dunia hii wala hawajui kwamba wakifa wataacha hapa mali zao na wataenda huko waendako wakiwa mikono mitupu.

1 Yohana 2: 15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

Dunia sio rafiki kabisa wa mwanadamu ila wanadamu hawalijui hilo.
shetani anaitwa mungu wa dunia hii maana yake watu wengi badala ya kutawaliwa na MUNGU aliye hai wao wamekubali kabisa kuwa chini ya himaya ya mungu wa dunia hii yaani shetani.
Wanadamu mchana na usiku wako tayari kumpendeza shetani badala ya MUNGU aliye hai. 2 kor 4:3-4 '' Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU.''

Wanadamu wengi hawajui kama wameumba na MUNGU maana kama wangejua kwamba wameumbwa na MUNGU wa mbinguni basi wangemtii.
MUNGU BABA anauliza  ''Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? -Malaki 3:7''

Sio mara zote shetani anawashawishi wanadamu ili wamwache MUNGU bali wao wenyewe wanadamu kwa sababu ya tamaa ya vitu vinavyoonekana hujikuta wakijipendekeza kwa shetani ambaye naye huwatumia vile atakavyo.

''Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.  atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili MWANA wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. 1Yohana 3:4,8''
Biblia inasema atendaye dhambi ni wa shetani. je watu wa shetani ni wangapi? maana mtenda dhambi ni wa shetani. 

Hata wateule kabisa wa BWANA YESU leo wapo ambao kwa sababu ya tamaa ya vitu vinavyoonekana wamejikuta wamemkimbia MWOKOZI wao.
Hawamhitaji YESU sasa kwa sababu ya dunia na vitu vyake.Yohana 3:19-21 ''Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU. ''

Elimu za wanadamu badala ya kuwasaidia ili wamtumikie MUNGU lakini wao elimu hizo ndizo chanzo cha kumkufuru MUNGU.

Ndugu zangu, dunia itapita na mambo yake yote.
Hata kuwa na sauti nzuri tu kumewafanya wengi kumtumikia shetani wakiwa mawakala wake kwa njia ya miziki ya kidunia.
Kuna watu kuwa na maumbo mazuri tu kumefanya wamtumikie shetani.
Kuna watu kuwa na sura nzuri tu kumewafanya kumtumikia shetani.
Kuna watu kuzaliwa tu kwenye familia za kitajiri kumewafanya wawe walevi na wazinzi na kumchukiza MUNGU aliye hai.
Kuna watu kumiliki magari kwao tu imekuwa tatizo na sasa ni kiguu na njia kila siku kwenye kufanya dhambi.
Dunia inapotosha watu sana, vinavyoonekana vimewakosesha sana uzima wanadamu. ''tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. -2 Kor 4:18''

BWANA YESU kila siku anawahitaji wanadamu lakini hata hawana habari nae.
BWANA YESU anawaambia wanadamu kila leo kwamba aliwafia ili wawe na uzima wa milele lakini wanadamu wengi hawataki.
Mchungaji akikufatilia na kukupigia siku kwamba uje kanisani kujifunza neno, unaanza kumkwepa na kumsema vibaya na kusema ''hiki kizee kimekosa kazi''
Ndugu yangu hizo ni huruma za MUNGU na anakuvuta tu kwa njia za kibinadamu. lengo la MUNGU na mchungaji ni usiende motoni.
Siku ile kuna watu watalia sio kwa sababu ya kutenda dhambi kwao bali watalia wakikumbuka jinsi walivyokutana na ujumbe wa MUNGU na kuudharau, watalia jinsi walivyoijua kweli lakini wakaidharau.
Ndugu yangu, dunia itapita, wewe na mimi tutaondoka lakini ni ole wake yule anayemkataa BWANA YESU leo, ole wake yule anayekataa kuishi maisha ya wokovu leo. Kumkataa YESU ni kukataa uzima wa milele na kujifanya ni wa YESU kumbe matendo yako ni ya shetani nayo ni hasara kwako.
MUNGU hata leo anakuhitaji, ukiisikia sauti ya MUNGU usifanye moyo wako kuwa mgumu.
Mambo yaliyomo dunia yamewafanya wanadamu wengi kupotea.
Utajiri na elimu, biashara na fani vimewafanya watu wengi kupotea.
Ndugu yangu siku ile hutaondoka na elimu yako wala utajiri wako bali utaondoka mikono mitupu.
Mimi nakuonya na kukuomba kwa upendo mwingi sana mpokee BWANA YESU na uishi ukimpendeza MUNGU. Kumbuka hakuna uzima nje ya BWANA YESU.
YESU KRISTO anakupenda sana na yuko tayari kukupokea leo na jina lako litaandikwa mbinguni kwenye kitabu cha uzima.

Wagalatia 5:18-21 ''Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments