HUWEZI KUMILIKI BILA KUFANYA VITA

Na Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima, ufufuo na uzima.
Mungu ametuahidi ahadi nyingi kwenye Biblia lakini hatuwezi kuzipata bila kupigana vita, kwenye kila ahadi anayotoa Mungu lazima kuwepo na vita.
Mungu anataka tushindane na ametugawia nguvu ya kupigana, Mungu huwa anakupa vinavyomilikiwa na watu ili upigane na kuvimiliki. Watu wengi katika kanisa leo wamesahu hilo, wanaamini kwamba Mungu akisema amekupa tayari umeshapata kumbe kuna vita ya kupigana.
Ndio sababu watu wengi walioahidiwa vitu na Mungu hawajaviona vikitokea mpaka Leo, kwasababu waliokaa wakaridhika wakaacha kufanya vita. Mungu anapokuahidi jambo inatakiwa ujue ufanyeje ili kupokea ahadi ya Bwana katika maisha yako.
Imeandikwa: Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; (KUT. 13:17 SUV)
Mungu aliwaongoza njia isiyokua na vita kali, lakini njia inayooitwa haina vita ndio ile ile waliopigana na Waamaleki, pamoja na mataifa mengine. Ilifika kipindi ikabidi Mungu asimamishe jua ili Israel wapigane vita.
Mungu akataka hata watoto waliozaliwa katika nchi ya ahadi wajifunze kupigana vita, ndio sababu akawaacha mataifa matano katika nchi hiyo ili wapigane nao vita.
Imeandikwa: Basi haya ndiyo mataifa ambao BWANA aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani; (AMU. 3:1 SUV)
Hii ndio sababu wakati mwingine Mungu anaruhusu magumu au changamoto ili ujifunze kupigana vita. Ndio sababu Mungu anaitwa "Bwana wa vita"
Paulo alimwambia mwanae wa kiroho Timotheo kuwa amepigana vita.
Imeandikwa: Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; (2 TIM. 4:7 SUV)
Huwezi kumiliki pasipo kufanya vita.
Mungu na akupe Neema ya kufanya vita ili umiliki kila ulichoahidiwa na Bwana kwa jina la Yesu.

Comments