JE MTU UWEZA KULINDWA KWA KITAMBAA AU MAFUTA AU MAJI YALIYOOMBEWA NA MCHUNGAJI?


power of Jesus name
Na mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Siku moja nilipokuwa nimetulia Roho akasema nami kwa habari ya ulinzi wa kiroho kwa mwamini. Akaniuliza Je ni kweli ulinzi wa watu wangu upo katika kitu kiwayo chote hata kama kimeombewa na mtumishi?
Kwamba kitu hicho ndio kifanyike ulinzi kwa mwamini?
Kwa kweli sikuwa na jibu kipindi hicho,maana naliwaza nikawazua,nikafikiri kwamba inawezekana kulindwa na chochote kile kwa yule anaeamini.
Ndiposa Roho akanichukua mpaka katika maneno aliyoyasema Bwana Yesu,ambayo maneno hayo ndio asemayo leo. Akanipeleka mpaka katika kitabu cha Yohana,ile sura ya 17:12.
Imeandikwa;
” Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. ” Yoh.17:12
Maneno hayo ni maneno ya Bwana Yesu mwenyewe,yalikuwa ni maombi ya Bwana.
Swali hili ( Je mtu huweza kulindwa kwa kitambaa,au mafuta,au maji yaliyoombewa na mchungaji ) ni moja ya maswali muhimu na makini sana katika imani yako.
Si wengi wenye kujiuliza swali kama hilo,wengi huwa tunapokea au kufanya chochote  kile tunachokiamini kuwa ni kinga yetu.
Wengine hawapendi kulisikia jambo hili likihubiriwa sababu wanaona kana kwamba wao wanaohubiri wasije wakaharibu imani yao. Leo nami imenilazimu kuyaeleza haya mambo wazi wazi pasipo kumuonea mtu haya! kama vile alivyonionesha Roho wa Bwana.
Katika andiko lile lile alilolifunua Roho wa Bwana,ndilo nami naanzia papo hapo.
Bwana Yesu anatuambia wazi wazi kabisa ya kuwa ulinzi wa mtu upo katika jina lake tu. Biblia inasema Bwana Yesu alupokuwapo aliwalinda kwa JINA LAKE pekee,wala hazungumzii ulinzi wa kitu chochote kile.1393006272853
▪ Ulinzi wa kweli upo katika jina la Yesu Kristo.
Unapolitamka jina la Yesu Kristo kwa habari ya ulinzi,na damu yake uhusika.
Jibu la swali la hapo juu ni hili. ▪ Mtu hawezi kulindwa kwa kitambaa,wala maji wala chumvi,wala mafuta,wala hawezi kulindwa na kitu chochote kile hata kama kimeombewa na mchungaji. Ulinzi wa mwamini haupo katika kitu bali upo katika jina la Yesu Kristo tu.
Roho alinifunulia haya ili niwaambie ndugu zangu wenye kutembea na vitambaa vya upako kama kinga yao,na wale wenye kutegemea maji,au mafuta kama kinga kwao,kwamba vitu hivyo havina ulinzi wowote ule.
Vitu vya namna hiyo ni kama uganga wa kawaida kabisa. Maana ipo tofauti gani kwa yule mwenye kutembea na kitambaa kama kinga yake na yule mwenye kutembea na irizi kama kinga yake?
Utofauti wa hawa wawili upo wapi?
Tuangalie neno la Bwana linasemaje
” Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza;…” Yoh. 17:12
Yesu anazungumzia ulinzi kwa jina lake,wala hazungumzii ulinzi kwa mafuta,maji,kitambaa bali kwa jina lake. Na anazidi kusema kuwa jina lake lina kazi ya kutunza. Hii ikiwa ina maana kuwa,jina la Yesu lina ulinzi tosha na linautunzaji kwa wale wenye kumuamini.
Naomba unielewe kwamba;
Roho mtakatifu Yeye ni Mungu wa utaratibu na njia zake hazichunguziki. Roho mtakatifu anaweza kumuelekeza mtumishi wake,atumie mafuta katika ibada fulani kwa ajili ya kufungua nira za yule aliyefungwa ( Isaya 10:27 ) . Kwa habari ya jambo kama hilo sio mbaya,maana ni Roho mwenyewe yupo kazini saa ile ile katika ibada.
Lakini ubaya unakuja pale mtumishi anapotumia mafuta kwa kuyaombea au kitambaa kisha na kuwapa waamini waende navyo kama kinga yao,watembee navyo muda wote kama ulinzi wao.Hilo ndio tatizo kubwa sana,!!
Pameandikwa wapi,kwamba watu walindwe na vitambaa,au maji,au mafuta au chumvi,au mchanga ?
Mpendwa imefika wakati wa kugeuka kutoka katika kuvitumainia vitu viaribikavyo na kuanza kulitumainia jina la Yesu Kristo. Jina hili ndilo tulilopewa wanadamu litupasalo kuokolewa kwalo ( Matendo 4:12 ).Hatuna haja tena ya kutegemea kitu kingine ikiwa tumepewa jina la Yesu.
Wakati mmoja nalipokuwa naelekea Israeli, watu wengi wakristo waliniagiza vitu mbali mbali nije navyo. Wengine walinituma nije na mchanga wa Isareli,wengine walinitaka nibebe matope ya Israeli,wengne walihitaji mafuta ya upako. N.K,basi tu kila mmoja alikuwa na lake kulingana na kile anachokiamini.Lakini cha kushangaza hakuna hata mmoja wao aliyeniagiza nije na Yesu wa Nazareti,yaani nije na upako.
Ndipo sasa nikaangalia imani yao,nikagundua kwamba imani ya wakristo wengi siku ya leo imeegemea katika vitu na sio katika uweza wa jina la Yesu Kristo,hii ni shida kubwa katika kanisa la leo.
Unajua ni shetani ndio ameingia hata kwa baadhi ya wachungaji na kwa waamini kwa kubadilisha imani yao kwamba wasiliamini jina la Yesu Kristo na kugeukia vitu vilivyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu kwa kuvifanya ndio miungu yao.
Mpendwa,kataa kuvitumainia vitu hivyo kwa ulinzi bali litumainie jina la Bwana pamoja na damu yake kwa ulinzi tosha wa maisha yako. Hakuna awezaye kulinda maisha yako isipokuwa Yesu Kristo tu. Kwa jina lake sisi tunakuwa na uzima,kwa jina lake tunaishi na kwa jina lake tunakwenda kwa ushindi tele.
Ushauri wangu wa bure kwako;
Ikiwa mtu amekuamanisha kuvitumainia vitu vingine,umuulize amepata wapi imani ya namna hiyo? Maana hatukuagizwa kutembea na ulinzi wa namna nyingine iwayo yote isipokuwa jina la Yesu tu na damu yake.
Kwa huduma ya maombi na maombezi nipigie;
0655-11 11 49.
Mch. Gasper Madumla
Beroya bible fellowship church-Kimara
UBARIKIWE.
▪ Usikubali kutembea na kitambaa kama ulinzi wako. Kubali kutembea na Yesu kwa ulinzi wa kila kitu.Kamwe utukufu wa Bwana hauwezi kukaa katika kitambaa bali utukufu wa Bwana hukaa ndani yako.

Comments