JE! UNAWAACHIA WANAO URITHI KIASI GANI?

Na Frank Philip

"Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA" (Mithali 19:14).
"Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; akatawala Yehoramu mwanawe mahali pake. Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, na Yehieli, na Zekaria, na Azaria, na Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli. Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, na za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza" (Mambo ya Nyakati 21:1-3).
Bila shaka imempasa kila mtu kuwa na kitu mkononi mwake kwa ajili ya wanawe akiwa hai au amekufa, hasa kama ni mtu anayemjua Mungu. Tafsiri ya MALI sio utajiri, bali ni VITU ambavyo vinaweza kutofautiana kwa wingi na thamani.
Kila mtu imempasa awe na kitu ambacho anajua hiki ni kwaajili ya watoto baada ya kufa. Wengine wamewekeza sana katika ELIMU bora za watoto wao, naam, hilo ni jambo jema sana, lakini ikiwezekana, mwombe Mungu ili uweze kuwa na vitu angalau kidogo kwa majina ya watoto wako, na uwape ungali hai. Hii ni njia mojawapo muhimu ya kuepusha migogoro ya kifamilia.
Kati ya wafalme wa Yuda au Israel ambao walimpenda sana Mungu na kwenda katika njia zake mmoja wao ni Yehoshefati, mfalme wa Yuda. Kama ilivyokuwa Daudi, mfalme wa Israel, alivyojiwekea mali nyingi ambazo alimpa Suleiman ili aweze kumjengea BWANA nyumba, Yehoshefati naye alifanya vivyo hivyo; Aliwapa mali nyingi wanawe.
Jiulize jambo hili, kama Yehoshefati alikufa na tunaambiwa ALIWAPA, je! marehemu aweza kugawa mali? Kwa fundisho hili, naweza kujifunza kwamba hawa watu waliomjua Mungu, walijua umuhimu wa kuandika MIRATHI kabla ya kufa. Utaona jambo hili pia kwa Ibrahimu, Yusufu, Isaka, na watumishi wengine wa Mungu waliokuwa mifano bora kwetu. Waligawa urithi kwa wanao kabla ay kufa! Kuandika mirathi ni jambo la hekima na la kuiga kwa watumishi wa Mungu waliotutangulia.
Angalia, kufa kupo kwa kila mtu, weka mambo ya nyumba yako vizuri. Usiseme kwa sababu nitakufa na umri umesogea basi sitafuti mali; huo ni mtazamo hasi. Jinunulie ardhi kwa ajili yako na wanao, bila shaka litakuwa jambo jema sana. Ukiisha kununua, andika majina yao bila upendeleao, huku ukiomba uongozi wa Roho Mtakatifu.
Frank Philip.

Comments