MUME AKIMKOSEA MUNGU HALI MKEWE AKIJUA PASIPO KUREJEA KATIKA TOBA,BASI ADHABU YA KOSA HILO NI LA WOTE WAWILI.


ndoa 2
Na mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Karibu katika fundisho hili fupi sana siku ya leo ndugu mpendwa katika Kristo Yesu. Na siku ya leo nina neno fupi kwako wewe mwanandoa,au kwako wewe mtu unayejitayarisha kuingia katika ndoa.Ikumbukwe kwamba ndoa ndio taasisi ya kipekee ya Mungu inayowindwa sana na shetani tofauti kabisa na vile wanavyofikilia watu.Sababu kupitia ndoa ndipo utakatifu unapoanzia,kupitia ndoa ndipo watumishi wa Mungu wanapotokea,na kupitia ndoa ndipo taifa huzaliwa.
Kama tujuavyo wawili katika ndoa ni mwili mmoja kama vile neno lisemavyo (Mwanzo 2:24). Hivyo basi dhambi yoyote ile ya mmoja wapo katika ndoa huweza kuwa kisababisho cha mateso kwa mwingine ikiwa dhambi hiyo haijashughulikiwa.
Mara nyingi kuna makosa ndani ya ndoa. Makosa hayo yanaweza kusababishwa na mume au mke,kila kosa lina adhabu yake ikiwa halijatubiwa au kusawazishwa kwa uweza wa damu ya Yesu Kristo wa Nazareti.  Biblia inaweka wazi jambo hili,na hapa tunaanza kusoma;

Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?” Matendo 5 :1-3
Katika andiko hilo hapo juu,tunaona Anania akiuza kiwanja kwa siri hali mkewe akijua. Biblia haisemi kwamba kiwanja kile kiliuzwa na Anania pamoja na Safira,bali tunaelezwa kwamba Anania peke yake kama mume ndie aliyeuza kile kiwanja kwa siri.
Safira mkewe alihusika kwa kujua mauziano ya siri juu ya kiwanja,lakini Safira hakuuza chochote. Kwa lugha ya kileo tunaweza kumuita Safira alikuwa kama shahidi wa mauziano ya kiwanja yaliyofanyika kwa siri.Kosa la Anania ilikuwa sio kuuza kiwanja kile,bali kosa lake ni kumuambia uongo Roho mtakatifu na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja. Jambo hili lilikuwa likijulikana kwa Safira,naye Safira alikuwa na mawazo kama ya mumewe.
Kwa kosa hilo lililotoka kwake Anania hali mkewe akijua hayo yote,adhambu yao ikawa sawa sawa.Wote walikufa kwa sababu dhambi ya Anania ilikuwa ni dhambi ya Safira maana hawa wote ni mwili mmoja. Biblia hajadanganya kusema wiwili katika ndoa ni mwili mmoja.
Anania na Safira walikufa kimwili kutokana na kosa la kumwambia uongo Roho mtakatifu na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja.Kwa kosa kama hilo,siku ya leo tunakufa pia. Wapo watu wengi leo waliokufa hali wanatembea kwa sababu ya dhambi zao.(Waefeso 2:1)
Safira alijua mauziano hayo yote,na hata ile namna ya kumuambia Roho mtakatifu uongo,lakini alikuwa akiwaza kwamba siri yao haitafichuka,hawakujua kwamba Roho mtakatifu Yeye huchunguza hata mambo ya siri. Na hiki ndicho kinaua wanandoa katika kanisa, wakipatana kudanganya mbele za wachungaji au watumishi wa Mungu juu ya mali zao,au maisha yao katika utoaji,wakidhani kuwa wanamuambia uongo mwanadamu bali Mungu.
Leo wanandoa hufa kiroho kwanza,
Yapo mapigo katika ndoa yaliyosababishwa na dhambi ya mmoja wao,hali mwingine akijua dhambi hiyo bila kuitubia ipasavyo. Mfano mdogo tu,ni hivi;
Baba anaweza akawa ni muabudu sanamu,au miungu mingine hali mama anajua hilo pasipo kulishughulikia ipasavyo,na baadaye wanashtuka wakipitishwa katika mateso makubwa yaani mateso kama vile ndoa kukosa amani,kuwa na mafarakano kila siku na hata kushindwa kupata mtoto,N.K
Dawa ya mateso yote haya katika ndoa ni kurejea kwa Yesu,kuanza moja na Bwana. Kuanza kuishughulikia dhambi hiyo yote katika ukamilifu wake,maana dhambi ni maovu hivyo Bwana Mungu akikusamehe maovu yako yote,na atakuponya na magonjwa yako yote katika ndoa ( Zaburi 103 :3)

* Kwa msaada wa maombi,nipigie kwa namba yangu hii;
0655-11 11 49.

UBARIKIWE.

Comments