MUNGU ANATAKA KABLA YA YOTE KWANZA TOBA YA KWELI.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze habari za uzima wa roho zetu.
Neno la MUNGU ni chakula za roho zetu hivyo kwa vyovyote vile kama tunataka tuwe hai kiroho lazima tu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
MUNGU yuko hai na Neno lake liko hai vilevile.

Kama kuna jambo gumu kwa watu wengi basi ni toba ya kweli yaani kutubu na kuacha dhambi hiyo.
Siku zote na miaka yote MUNGU anataka sana watu wake watubu na kugeuka yaani watubu na kuacha dhambi hizo. Maana yake kama unafanya uzinzi na kutubu kila siku  na baadae unarudi tena kwenye uzinzi hapo bado haikusaidii, tena hujatubu, huko ni kumjaribu MUNGU na Biblia iko wazi kabisa kwamba ''Usimjaribu BWANA MUNGU  wako-Luka 4:12) 
-MUNGU hajaribiwi kwa uovu, unatenda dhambi ukijisemea ''si nitatubu''.Ndugu hata wote walio matesoni kuzimu leo walijisemea hivyo hivyo unavyojisemea wewe lakini walijikuta huko bila kutubu toba la kweli.
 Kama kuna mahubiri MUNGU anataka watumishi wake wahubiri kila iitwapo leo basi nikuhubiri ili watu watubu na kumpokea YESU KRISTO na majina yao yataandikwa kwenye kitabu cha uzima.
-Kutubu ni muhimu sana.
-Hakuna dhambi inayojisamehe yenyewe ndugu zangu.
-Hakuna kusamehewa kwa njia ya  sms tu ya kuambiwa ''umesamehewa dhambi zako''
-Hakuna kusamehewa kwa njia ya kutoa pesa za kitubio, kitubio cha pesa ni ushetani.
-Hakuna kutubu baada ya kufa.
-Hakuna maombi ya mtu awaye yeyote yanayoweza kumbadilishia makazi marehemu yeyote.
MUNGU anataka wewe mwenyewe mwenye dhambi uchukue maamuzi, Wachungaji kazi yao ni kuwapatanisha wanadamu na MUNGU aliye hai kupitia YESU KRISTO. Ni jukumu lako  kuongozwa kwa maombi na jina lako litaandikwa tena kwenye kitabu cha uzima mbinguni.

Kuna mambo makuu matatu nataka niyazungumzie katika ujumbe wa leo.

=Jambo la kwanza ni kwamba Yohana mbatizaji alipoanza tu kuhubiri, Jambo la kwanza alisema '' Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.- Mathayo 3:2 ''
-Unaweza ukajiuliza, Kama Yohana mbatizaji angekuwa baadhi ya wahubiri wa leo angeanza huduma yake kwa mahubiri yasemayo ''Njoni kwangu ili mbarikiwe kwa baraka kubwa kubwa za nyumba na magari''
Lakini MUNGU anataka kwanza toba, Lengo la BWANA YESU ni watu wampokee na kutubu ili wapate nafasi ya uzima wa milele. ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi -Yohana 14:6''
Yohana alimtii ROHO MTAKATIFU ndio maana alihubiri toba.


=Jambo la pili ni kwamba BWANA YESU alipoanza huduma yake hapa Duniani alianza na jambo hilo hilo, Mathayo 4:17 Biblia inasema '' Tokea wakati huo YESU alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. '' 
-YESU anaanza kuwahubiri watu kwa kuwaambia watubu maana ufalme wa MUNGU umekaribia. Na Katika Marko Biblia inasema ''   Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, YESU akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya MUNGU, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.-Marko 1:14-15''
-BWANA YESU anaanza tu huduma kwa kusema ''Tubuni na kuiamini injili kwa maana Ufalme wa MUNGU umekaribia''
-Toba ni jambo kuu ambalo MUNGU analihitaji kwako na kwangu ndugu, sio kwamba injili za mafaniko ni mbaya hapana ila muhimu kuliko yote ni Toba na jambo la toba ndilo linalotakiwa lipewe nafasi ya kwanza  kuliko yote.

=Jambo la Tatu ambalo nataka nizungumzie ni Mitume walipoanza tu kuhubiri injili, moja ya maneno ya kwanza kusemwa na wao ni hili hapa '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; apate kumtuma KRISTO YESU mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na MUNGU kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu-Matendo 3:19-21''
-Hata mitume walianza na mafundisho ya toba.
Toba ni muhimu sana maana baraka bila kutubu hakuwezi kumwepusha mtu na jehanamu, lakini toba ya kweli ndiyo inayoweza kumwepusha.
-Ndugu zangu ni wakati wa kutubu, Na toba zote tunatubu kwa MUNGU kupitia YESU KRISTO pekee, hakuna njia nyingine ya kutubu. Warumi 10:9-10 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. ''
-Wachawi tubuni
-Waongo tubuni.
-Wazinzi na waasherati tubuni.
-Wambea tubuni.
-Wasengenyaji tubuni. 
-Mama na baba tubuni.
Vijana na wazee tubuni.
Watoto na mabinti tubuni.
Ni saa ya kutubu.
Ndugu, tubu dhambi zako zote maana nimetaja 1% tu ya dhambi.
MUNGU hasa anataka kwanza toba ya kweli, Kujificha na kutenda wema machoni pa watu hakutakusaidia ndugu. Mkimbilie BWANA YESU ili akuokoe.

''Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. -Mithali 11:2.

Wanyenyekevu ni wale wanaokubali kumpokea BWANA YESU na kutubu
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu Yako Peter M Mabula.
Maisha ya ushindi Ministry.
Mabula1986@gmail.com.
0714252292

Comments