NUKUU MUHIMU KUTOKA KWA WATUMISHI WA MUNGU.(Sehemu ya 3)

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze na kutiwa moyo na kukua kiimani kupitia Nukuu hizi za watumishi mbalimbali kutoka kwenye mafundisho yao au mahojiano. Na utaniambia wewe binafsi umependa Nukuu namba ngapi kati ya hizi Nukuu 11.


1.Huwezi kuomba kwa muda mrefu kama hujui faida na mbinu za kuomba kwa muda mrefu.
Unaweza kuzijua faida za kuomba kwa muda mrefu lakini usipozijua mbinu za kuomba huko hutaweza kuomba inavyotakiwa.
Unaweza kuzijua mbinu za kuomba kwa muda mrefu, Lakini usipozijua faida za kuomba hivyo hutapata msukumo ndani yako wa kutumia hizo mbinu ili kuomba ipasavyo-By Mwl. Christopher Mwakasege.

2. Usiishi kwa sababu tu unaishi bali ishi kwa sababu KRISTO anaishi ndani yako-By Peter M Mabula.

3.   Kila mtu aliyeokoka ni jiwe moja au tofali ambalo linapaswa kuunganishwa na mengine na kufanywa kuwa Jengo la MUNGU au Kanisa. Ni rahisi kuiba tofali lililotupwa mchangani, kuliko tofali lililounganishwa na wengine katika Jengo. Shetani ni rahisi kumuiba mtu ambaye hajiungi na Kanisa (1 PETRO 2:5)-By Askofu Zakaria Kakobe.

4.  Dunia inakuambia '' Mimi nitakutenga '', shetani anakuambia ''Nitakuangamiza'', Mwili wako unakuambia ''Nitakusaliti'' Lakini Uko salama kwa sababu MUNGU mwenyewe anakuambia '' Sitakupungukia kabisa, Wala sitakuacha kabisa(Waebrania 13:5)- By John Flavel.

5. Ili ushinde ulimwengu ni lazima ujue siri hii kuwa Mtu  ni ROHO anayo NAFSI anaishi katika MWILI. Kabla ya anguko la Adamu, MUNGU alitawala ulimwengu kupitia roho ya mwanadamu, Lakini baada ya anguko shetani alianza kutawala ulimwengu kupitia mwili wa mwanadamu. Ijue kweli ili ikuweke huru-By Mtume Moses Kingu.

6.  Miaka mingi imepita toka niwe Mkristo. Ndugu zangu , marafiki na wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinilaumu daima kuwa nilikuwa naisaliti nchi yangu na kwamba sikuwa mtiifu kwa wazazi wangu na tena nimekufuru kwa vile sasa nilikuwa naamini Miungu watatu. Hii yote ilitokana  na kutokuielewa vizuri imani ya Kikristo na mafundisho ya Biblia ambayo waislamu wengi wanaogopa kuyasoma. Biblia  imeandika wazi wazi kuwa Wakristo sharti wawatii viongozi(1  Petro 2:13-14), Wawahesimu wazazi wao(Kutoka 20:12) na kumwamini MUNGU mmoja wa kweli(Mathayo 22:37)- By Masoud Ahmed Khan.


7.   Maisha ya mtu ni matunda ya mtiririko wa maamuzi ya mtu mwenyewe binafsi, lakini yanaweza pia yakawa   yamechanganyika na maamuzi ya watu wengine yaliyogusa maisha yake. Kufanya uamuzi ni uamuzi wako, MUNGU hawezi kukulazimisha kufanya uamuzi, ila atakujengea mazingira ya kukusaidia ufanye maamuzi vizuri na mazuri. Usilaumu mazingira yaliyokufanya uamue ulichoamua, ikiwa hupendi matokeo ya uamuzi  huo. Lakini ukubali kuwajibika na matokeo ua maamuzi yako, Ndio maana unahitaji msaada wa MUNGU juu ya jambo hili la maamuzi-By Mwl. Christopher Mwakasege.

8.   Kuna Watu BWANA YESU Kila Siku Anagonga Hodi Kwenye Milango Ya Mioyo Yao Ili Awaokoe Wasiende Jehanamu, Lakini Watu Hao Wameshupaza Shingo Zao Ambazo Karibia Zinavunjika Na Wokovu Hawajaupata. Ndugu Ukiisikia Sauti Ya BWANA YESU Usishupaze Shingo Bali Mpokee- By Peter M Mabula.

9. Ipe Biblia nafasi ili ifanye kazi ile inayotaka kufanya. Iache Biblia iseme yenyewe. Sio kazi yetu kuifanya Biblia iseme au ifanye jambo fulani , bali kazi yetu ni kuielewa na kuitii-By Don Fleming.

10. Uharibifu mmojawapo wanaoufanya wasichana ni kutokuwa makini na mtu anayemwomba uchumba, Wasichana wengi wamepiga simu na kuandika kuwa Hakuna kijana aliyewahi kuwataka uchumba. Wakati ambapo wengi wao wamewakataa wachumba zaidi  ya wanne, Sasa umri wao umekwenda  na hakuna tena mtu mwingine aliyekuja tena kuwataka uchumba- By Mwinjiliti Kenneth Onyeme.

11. Huwezi kufanikiwa katika maoisha yako zaidi ya MTAZAMO ulionao juu ya maisha na mambo mbalimbali yanayokuzunguka katika maisha- By Mchungaji Goodluck Kyara.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu Yako Peter M Mabula.
Maisha ya ushindi Ministry.
Mabula1986@gmail.com.

0714252292
Askofu Zakaria Kakobe.

Comments