SEMA HIVI MIMI NI HODARI.


SAM_1691
Na Daud  Lubeleje.
UTANGULIZI:
Bwana Yesu asifiwe. Atukuzwe Mungu aliyenipa kibali hiki tena kukuletea somo hili lenye kichwa kinachosema “SEMA HIVI MIMI NI HODARI”. Unapoendelea kujifunza somo hili ni maombi yangu Roho Mtakatifu akupe kudaka na kuelewa kile amekusudia kwako.
Ukisoma katika Warumi 5:6, 8 Neno la Mungu linasema “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili waovu……..kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi”. Katika mistari hii tunajua kwamba “Tulipokuwa tungali wenye dhambi ndio wakati tulipokuwa hatuna nguvu” na asiye na nguvu kwa maana nyingine ni mtu aliye DHAIFU. Mtu aliye dhaifu ni Yule asiyeweza kufanya mambo mpaka kwa msaada wa mwingine au mpaka asaidiwe. Kwahiyo Dhambi inamfanya mtu kuwa dhaifu wa kufanya mambo, inamwondolea ule ujasiri wa kusema MIMI NI HODARI NA SHUJAA       . Sasa hebu daka pointi hii;
POINTI: Dhambi inaondoa ujasiri na uhodari wa kufanya mambo na badala yake inaweka udhaifu wa kuona kuwa mambo hayawezekani.
Maandiko yanaendelea kusema kwa sababu hatuna nguvu na dhaifu kwa sababu ya dhambi, Mungu alimtoa Kristo Yesu aliyekufa msalabani kwa ajili yetu kuondoa huo udhaifu na kuweka NGUVU. Tumeona Neno la Mungu linasema “…..Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8). Kristo alipokufa msalabani alichukua udhaifu wetu na kutupa nguvu, Hiyo nguvu inatupa ujasiri wa kusimama na kusema MIMI NI HODARI. Ngoja nataka tuone mstari huu katika Mathayo 8:17 Neno la Mungu linasema “…….Mwenyewe (Yesu Kristo) aliutwaa udhaifu wetu………”. Sasa unaweza kuona faida ya kuokoka na kumpa Yesu maisha yako kwamba ile hofu ya dhambi inayoleta udhaifu kwa kuona mambo hayawezekani, Kristo anaondoa na kukupa ujasiri na sasa unaweza sema mimi ni hodari. Si jambo la ajabu kukuta mtu anayemjua Mungu akisema NAYAWEZA MAMBO YOTE KATIKA YEYE ANITIAYE NGUVU (Wafilipi 4:13) kwa sababu anajua kuwa udhaifu wake, Kristo Yesu alichukua pale msalabani na akampa ujasiri wa kutamka kwamba  yeye ni HODARI na anaweza mambo yote. Sasa daka pointi hii tena
Pointi: Kwa sababu Kristo Yesu alichukua udhaifu wetu, tunaweza sema kwa ujasiri tunaweza mambo yote na sisi ni HODARI ndani ya Kristo.
Ukisoma katika Yoeli 3:10 Neno la Mungu linasema “…..aliye dhaifu na aseme mimi ni HODARI”. Anayekwambia useme hivyo ni Kristo aliyechukua udhaifu wako na sasa anabadilisha kusema kwako kuwe MIMI NI HODARI. Wewe ambaye ulikuwa ukijinenea vibaya na kujiona ni dhaifu badilisha sasa usemi wako, acha kusema ile mimi siwezi, na sema mimi ni hodari na ninaweza ndani ya Kristo.
KWANINI USEME MIMI NI HODARI
Ziko faida kadha wa kadha za kusema mimi ni hodari. Huenda umefundishwa kwenye semina mbalimbali au Mchungaji wako amefundisha kanisani kwenu, ila nataka uone faida hizi ambazo ulikuwa huenda hujazifahamu;
Fungua biblia yako na usome kwa sauti kabisa mstari huu katika Isaya 53:12, Neno la Mungu linasema “……naye (Yesu Kristo) atagawanya nyara pamoja na walio hodari…..”. Nataka urudie tena ili udake vizuri ATAGAWANYA NYARA PAMOJA NA WALIO HODARI. Hii ni faida mojawapo katika nyingi za wewe kuwa hodari. Ukitaka upate mgawo wa nyara ambazo Kristo anagawa BASI AMUA KUWA HODARI. Hizo nyara ni zipi?, Nataka nikwambie kuwa ukisoma katika Waefeso 4:8 inasema “…Alipopaa juu aliteka mateka….”, Mateka ni nyara baada ya ushindi wa vita. Hizo nyara ni Baraka ambazo wewe unahitaji kwa maisha yako na ili upate badilisha usemi wako anza kusema mimi ni HODARI, naweza kufanya biashara, naweza kwenda kusoma, naweza peleka mtoto shule, naweza kufanya hiki na kile n.k, Utaona Mungu anafungua milango kwa ajili yako, UTAPATA MGAWO WA NYARA. Daka pointi hii
POINTI: Hakuna namna unaweza pata mgawo wa nyara (Baraka) za Kristo Yesu kama hujaamua kuwa hodari, walio hodari ndio wanagawana nyara na Kristo, Hivyo badilisha namna ya kusema kwako, Sema hivi mimi ni hodari!!!.
Faida nyingine tunaipata katika Yoshua 1:7 na inasema “Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, …….UPATE KUFANIKIWA SANA KILA UENDAKO”. Umeona?, Huwezi kufanikiwa kila uendako kama tu hujaamua kujivika uhodari na ushujaa mwingi. Ngoja nikupe sababu
“Aliye hodari anatangulia kuuona ushindi kabla hajaingia vitani, anaanza kutabiri juu ya kufanikiwa kwake hata kama mazingira hayako upande wake”
Walio hodari huongea maneno kama haya “Bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, …..Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, name nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako….” (1 Samweli 17:45-46). Huwezi kusema maneno ya waliokata tamaa ukitegemea ushindi na mafanikio. BADILISHA LEO USEMI WAKO SEMA HIVI MIMI NI HODARI!!!.
Faida nyingine tunaona katika Danieli 11:32 ambayo inasema “….lakini watu wamjuaoMungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu”. Ngoja nirudie sehemu hii tena WATAKUWA HODARI NA KUTENDA MAMBO MAKUU. Unataka kutenda mambo makuu basi amua kuvaa uhodari leo na uanze kusema kama Neno la Mungu. Daka pointi hii tena;
POINTI: Ukitaka kutenda mambo makuu, sema kama mtu aliye hodari na ujasiri mwingi
HITIMISHO
Mungu akubariki sana wewe uliyesoma somo hili. Tunaweza kuwasiliana zaidi kwa maombi, ushauri, maoni na maswali kupitia mawasiliano haya
Mwl Lubeleje D
VIJANA NA UTUMISHI
0764771298, 0652034083 & vijanautumishi@gmail.com

Comments