SIKU YA MWISHO WA DUNIA ITAZAA SIKU YA KWANZA YA MAISHA YA MILELE.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mauti ya kwanza ni lazima kwa watu wote, Lakini pia mauti ya pili ni lazima kwa watenda dhambi. Ufunuo 20: 6 '' Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa MUNGU na wa KRISTO .......'' 
Mauti ya pili inawahusu tu watenda dhambi, mauti ya pili itaanza baada ya hukumu. Mauti ya kwanza ni kifo cha kawaida ambacho kila mwanadamu lazima atakufa lakini mauti ya pili  inawahusu wasio na KRISTO na itakuja baada ya ufufuo.Ni heri kumpokea YESU leo maana ''Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU.-Warumi 8:1  ''
Biblia Imezungumzia Mara Nyingi Zaidi Kuja Kwa BWANA YESU Mara Ya Pili Kuliko Mara Ya Kwanza. Kuna Maana Yake Jambo Hili Ndio Maana Maandiko Yakawa Hivyo. Ujio Wa BWANA YESU Mara Ya Pili Una Maana Kubwa Sana Kwa Kila Mwanadamu Duniani, Kuna Watu Ujio Huo Utawapa Uzima Wa Milele Na Kuna Ambao Ujio Huo Utamaanisha Mwanzo Wa Jehanamu. Mtahayo 13:37-43 '' Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni MWANA WA ADAMU; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;  yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. MWANA WA ADAMU atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa BABA yao. Mwenye masikio, na asikie.   ''

 Ndugu Zangu, Anayeweza Kukuepusha Na Jehanamu Ni BWANA YESU Pekee, Mpokee Leo Na Jina Lako Litaandikwa Kwenye Kitabu Cha Uzima, Kisha Anza Kuukulia Wokovu Kwa Mafundisho Kanisani. BWANA YESU anasema  ''Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. -Ufunuo 3:20
-Mlango unaozungumzwa hapo ni moyo. Ndugu fungua moyo wako na umpokee mkombozi pekee wa ulimwengu. BWANA YESU anaendelea kusema ''Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. - Yohana 10:28''

 Baada Ya Kumpokea YESU KRISTO Kuwa BWANA Na Mwokozi Wako Na Kuanza Kuishi Ndani Yake, Toa Ushuhuda Juu Ya YESU Aliekuokoa Kwa Wengine, Soma Kwa Bidii Biblia Ili Uwe Mzima Kiroho Na Ili Uweze Kuwasaidia Wengine Kiroho. MUNGU Anatarajia Hayo Kwako uzae matunda kwa kuwaleta watu wengine kwake. Hakuna uzima nje na YESU KRISTO, Biblia inasema ''Amwaminiye Mwana(YESU) yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya MUNGU  inamkalia.-Yohana 3:36''

-Ndugu yangu tambua neno hili kwamba Siku ya mwisho wa dunia itakuwa tu ni mwanzo wa maisha ya milele, wengine mbinguni na wengine jehanamu.

Watu Wengi leo Wakipata Msiba Wa kufiwa Na Wapendwa Wao Huwaambia Marehemu Hao Kwamba "Tangulia Ipo Siku Tutakutana Mbinguni Kwa BABA". Ndugu, Yawezekana Kabisa Aliyekufa Ameenda Mbinguni Maana Aliishi Maisha Ya Wokovu Sahihi Ndani Ya BWANA YESU, Lakini Wewe Ni Mdhambi Mkubwa, Taarifa Ni Kwamba Wenye Dhambi Hawataenda Mbinguni. Na Kama Wewe Umeokoka Na Ndugu Huyo Hakumcha MUNGU Hadi Kifo Kikamkuta, Tambua Kwamba Mmetengana Nae Milele, Hata Kama Ulimpenda Sana Lakini Ukweli Ndio Huo. Wewe Mteule Kama Kweli Unaupendo Basi Mshuhudie Sasa Ili Ampokee YESU Kabla Ya Kifo.  Biblia inasema ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye(MUNGU) ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. -1 Yohana 1:9'' Kumbuka Wokovu Ni Sasa, Kama Mnapendana Okokeni Kwa Kumpokea BWANA YESU Na Liishini Neno La MUNGU Ndipo Hakika Wote Hata Mkiondoka Duniani Mtaenda Mbinguni, Lakini Kama Wote Ni Watenda Dhambi Hakika Hamtakutana Mbinguni Kwa BABA Bali Kuzimu Ni Kisha Jehanamu. 
Kuokoka kutaleta mageuzi makubwa  maishani mwako, Biblia inasema  '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. -2 Kor 5:17''

YESU KRISTO Anaokoa, Ukiamini Leo Unaokoka Na Jina Lako Linaandikwa Kwenye Kitabu Cha Uzima Mbinguni. Jambo Jingine La Kujua Ni Hili Hakuna Uzima Wa Milele Nje Na YESU KRISTO.
YESU anakupenda ndugu, chukua hatua ya kumpokea kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yako, utafutiwa dhambi zako na utakuwa huru. Biblia inatoa uhakika huu '' Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.-Yohana 1:12-13'' 
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments