TABIA YA WASHINDWAO

Na Frank Philip
(Mambo ya Nyakati 28:1-5, 16, 22, 23): “1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, kama Daudi babaye; 2bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, akawafanyizia mabaali sanamu za kusubu. 3Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli. 4Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. 5 Kwa hiyo BWANA, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.”
“16 Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie. 17Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.”
“22 Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi BWANA, huyo mfalme Ahazi. 23Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.”
Bila shaka hakuna mwanadamu asiyekosea iwe ni kwa makusudi, au kwa bahati mbaya. Niliposoma habari za mfalme Ahazi, nikaona tofauti yake na mfalme Daudi na watumishi wengine wa Mungu kama mfalme Ahabu, nabii Musa, Jushua, nk. Ahazi alipofanya MAKOSA, na akajikuta anaingia matatani kwa sababu ya makosa yake, HAKUMTAFUTA BWANA, ila ALIAMUA kuitolea miungu mingine dhabihu KWA MAKUSUDI.
Nimejaribu kuangalia mfano wa Ahazi na kuona kama bado kuna watu wenye moyo kama wa Ahazi katika kizazi hiki, nikaona wapo wengi sana juu ya nchi. Tabia ya Ahazi nimeiita tabia ya washindwao kwa sababu zifuatazo: kwanza, Ahazi alianza huduma yake au kazi yake kama mfalme kwa kuweka madhabahu za mabaali na wala si za Mungu wake (Mst.1-5). Pili, Mungu alipomrudi kama arudivyo awapendao, Ahazi hakujua marudia ya BWANA, akazidi kufanya machukizo tu. Tatu, baada ya kupata changamoto, Ahazi alienda kutafuta msaada wa wanadamu wala sio kwa Mungu wake! (Mst. 16). Nne, Ahazi akaona kwamba miungu ni bora kuliko Mungu wake AKAAMUA kuitolea sadaka! Kwa sababu alisema “miungu ya Washamu imewasaidia kunyume naye”. Ahazi hakujua kwamba vita ni vya BWANA!, Alidhani yeye ndio anapigana kwa hiyo hakumtafuta BWANA katika vita vyake, akashindwa siku zote.
Jiulize swali hili, unapoumizwa na mtu wa karibu, unafanya nini? Je! Unamrudia BWANA au unaazimia KUZIDI kumtolea ibilisi sadaka kwa mwili wako, fedha zako, nk? Je! Ni mara ngapi umetafuta msaada wa wanadamu na wala hukumwita BWANA kukupigania? Ni mara ngapi umejifariji na kuhalalisha uovu wako, eti, kwa sababu ya mtu mwingine kakukosea?
Jua jambo hili, kama Mungu alivyoufanya moyo wa FARAO kuwa mgumu ili aweze kuwafundisha Israel na dunia yote mambo Muhimu ya Ufalme wa Mungu na nguvu zake, vivyo hivyo, hiyo hali yako ngumu unayoshughulika nayo inaweza kudumu sana hadi utakapojua kwamba MUNGU ni BWANA. Na utakapo DHAMIRIA kumrudia kwa moyo wako wote, na kumtolea dhabihu zinazompendeza yeye na sio kwa miungu mingine, ndipo utakapoona kuvuka hatua nyingine.
Nimejifunza jambo hili maishani mwangu, mambo mengi tunayokutana nayo ambayo tunayaita “majaribu” au “vita” au “shida” au “mateso”, nk. yametengenezwa kutufanya imara kiimani na sio kutuangamiza. Ukiona mtu anapata shida katika ndoa yake, kazini, shuleni, nk., na akaamua KUMTENDA dhambi Mungu kwa sababu ya CHANGAMOTO zake, huyo amefeli mara mbili. Kwanza, amefeli kumjua Mungu wake, na pili amefeli mtihani muhimu wa kumwinua hatua zingine za mafanikio kimwili na kiroho. Mtume Paulo akijua jambo hili, anatufundisha kazi ya DHIKI maishani mwetu, yaani tufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu lakini pia anasema, “mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini” (Warumi 5:3,4). Kama hujajua, mitihani migumu zaidi na mizuri hupitia watu wa karibu sana kuliko watu mwa mbali, ili BWANA aujue moyo wako; na mara nyingi madarasa ya namna hii hufanyika jangwani (wakati wa kupungukiwa).
Mungu atuimarishe na kuifundisha mioyo yenu kumrudia BWANA na kumtafuta yeye peke yake katika changamoto zetu, ili tukiisha kushinda tukapate kuvuka hatua zingine za imani na mafanilio yetu ya rohoni na mwilini, na kutambua kwamba “bila BWANA sisi sio kitu”.
Frank Philip.

Comments