Umoja wa Wakristo wamtaka Waziri Mkuu.Kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi la Sivyo watazunguka Tz nzima kuwashawishi Wakristo kuipigia kura ya hapana Katiba Pendekezwa

Umoja
wa Wainjilisti wa Kikisto Tanzania (Uwakita), umemtaka Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda (pichani) kuuondoa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria
vinginevyo utazunguka nchi nzima kuwahamasisha waumini wake kuipigia
kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Wiki
hii, Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na
mambo mengine, kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la Sheria ya
Kiislamu, Sura ya 375.
Mapema
wiki iliyopita, Jukwaa la Wakristo Tanzania lilitoa hoja kutaka
Serikali kuondoa muswada wa sheria itakayosimamia kuanzishwa kwa
Mahakama ya Kadhi.
Hata
hivyo, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu nchini imesema
jukwaa hilo linaingilia madaraka ya Bunge na kutaka Serikali ionekane
inasema uongo.
Akisoma tamko hilo jana, Mwenyekiti wa Uwakita, Samson Bullegi alisema: “Tunalitaka
Bunge la Jamhuri ya Muungano lijiepushe na mijadala ya dini, hususan
suala hili la Mahakama ya Kadhi ambalo limekuwa likijirudiarudia kila
mwaka pamoja na kwamba lilishahitimishwa na Rais,” alisema.
Bullegi
alisema Uwakita unamtaka Pinda kuzingatia mambo matatu ambayo ni pamoja
na maoni ya Tume ya Kurekebisha Sheria iliyokuwa chini ya Profesa
Ibrahim Juma.
“Hakuna
malumbano kati ya Waislamu na Wakristo hapa wala Waislamu hawana
malumbano na Wakristo katika jambo hili naomba tueleweke hivyo.” alisema.
Makamu
wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec), Askofu Severin
Niwemugizi alisema anaunga mkono hoja za Uwakita za kushinikiza Serikali
kuondoa bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria akisema ni nzuri na
ndiyo wanayoisimamia tangu awali akisema hakuna msingi wa kuanzishwa kwa
Mahakama ya Kadhi kwa sababu jambo hilo halipo pia katika Katiba
Inayopendekezwa.
Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Leonard Mtaita amepinga
dhamira ya kuzunguka nchi nzima kwa madai kwamba taasisi yao haifanyi
kazi kwa maandamano, bali kuisukuma Serikali kusikiliza hoja zao.
Msemaji
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba
alisema kinachohitajika zaidi ni elimu ili kufahamu uendeshaji wa
mahakama hiyo. Alisema Serikali inatumia gharama kubwa kuendesha kesi,
lakini baadhi ya mahakimu hawana ujuzi katikakutatua kesi za kidini.
Comments