UNAFANYA NINI UKITENGWA?

Na Frank Philip.

Nimesikia habari ya watu kutengwa na familia, makanisa na hata wengine kufukuzwa nchi zao. Je! unafanya nini unapotengwa kwa KOSA liwe la kweli au la kusingiziwa?

Kuna namna mbili za kumtenga mtu: kwa kumwambia wazi wazi au kwa kujiepusha naye au kumkalia kimya tu.
Nimejifunza jambo hili, katika mambo mepesi kuambukiza kuna UCHUNGU au CHUKI! Yaani amekosewa mtu mwingine, kisha wewe unamsaidia mtu kumchukia adui yake! Ghafla tu unamkuta mtu anamkasirikia mtu na kumtenga, eti, kwa sababu "AMESIKIA" kwamba alimkosea mwingine! Je! ungekosewa wewe ingekuwaje?
Mojawapo ya sifa za KIONGOZI aliyekomaa ni kuweza KUTOFAUTISHA mambo BINAFSI na KAZI, hata kama hayo mambo binafsi yanamhusu. Naam, je! Si zaidi sana kwa ndugu zako waaminio? Je! Umchukie mtu, na kumtenga kwa sababu, eti, umesikia kafanya makosa? Je! Umkalie tu kimya halafu udhani kwa namna hiyo hujahukumu? Je! Atawezaje kurejeshwa kwa roho ya upole kama kweli ameghafilika? Ukimkalia kimya na kujiepusha naye yakufaa chochote? Je! Umsemapo mwenzako kwa sababu ya udhaifu wake, je! wewe umefikia ukamilifu wa Kristo hata uhukumu wengine?

Nimeona jambo hili, wakaapo wawili au zaidi wakimjadili mwingine kwa sababu ya udhaifu wake, kisha baada ya hapo wakajiwekea kusudio mioyoni mwao (japo hawajapanga) la kumkalia kimya tu, na kumyooshea vidole kila apitapo! Je! twaweza kuwa salama kwa namna hii?

Kama unadhani wewe ni kiongozi, mfano kwa jamii (kiroho & kimwili), jua kuwapa bega la kuegemea wale aliojeruhiwa na waliokataliwa, kuwapa mkono walioanguka ili wasimame tena wala sio kuwasema na kuwatenga huku ukijihesabia haki BURE.
Nawe uliyetengwa na jina lako kukanyagwa chini, usizimie roho wala kurudi nyuma.

 Kwa Mungu kuna msamaha. Kumbuka, imani ni jambo la kibinafsi. Wakiisha kukutenga na kukuacha peke yako, tafuta kujua siri hii, BWANA hakwenda kwa makundi ya watu maarufu na wakuu wa nchi, alijinyenyekesha na Mungu akamwinua sana, japo hakuwa na cheo wala kiti pamoja na wafalme wa dunia hii. Walipomhukumu aliwabariki, walipompiga aliwasamehe, naye alipozidi sana kunyenyekea na kufanya mapenzi ya BABA, ndipo alipokuwa mkuu sana, naam hata akakirimiwa Jina lipitalo majina yote. Basi mfuateni huyo maana kwake kuna USHINDI na FARAJA ya kweli.
Frank Philip.

Comments