USIONE SHAKA MOYONI MWAKO WAKATI UOMBAPO,ILI UPOKEE MAJIBU YAKO.


20141122_152926
Na Mtumishi Gasper Madumla. Akihubiri katika moja ya mahubiri ya mwaka 2014.
Bwana Yesu asifiwe…
Yeyote aombaye kwa MUNGU BABA,kwa jina la Yesu Kristo,basi hatakiwi kuwa na shaka ndani ya moyo wake kwa kile akiombacho,bali aamini amepokea hata kama mazingira ya kupokea yanakataa. La ! Kama mtu anaomba kwa mungu mwingine wa kibinadamu yaani sio Mungu mkuu,basi hata akiona shaka moyoni mwake ni sawa kabisa.
Maana hakuna atakachokipokea kwa huyo mungu zaidi ya kudanganywa na mapepo. Kuomba kwa imani pasipo kuona shaka moyoni ni kanuni ya kipekee ya mwombaji,Bwana Yesu alilijua hili na anasema hivi :
” Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. ” Marko 11:23
● Siri kubwa ya kujibiwa maombi yako ni kutokuwa na shaka ndani ya moyo wako.
Waamini wengi wanaomba sana,lakini wanamashaka mioyoni mwao,ndio maana hawapokei sawa sawa na kile walichokiomba.

Bwana Yesu anatufundisha namna ya kupambana na mlima kwa kuung’oa kwa kutumia kinywa,yaani maombi. Tafsiri nyepesi ya neno mlima,inaweza kuwa ni magumu yote unayoyapitia,mfano magonjwa yanaweza yakawa ni mlima kwako.Mateso yote ni mlima kwako,kila kifungo cha nguvu ya giza ni mlima kwako,N.K  Katika magumu hayo yote,yanaweza kuondolewa kwa kinywa chako kupitia jina lenye uweza,jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Maana imeandikwa;
” Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ” Matendo 4:12
Uwezo uliopo ndani ya jina hili la Kristo Yesu,limepita sayansi ya mwanadamu maana kwa jina hilo kila aina ya mlima lazima ushushwe. Nguvu iliyopo ndani ya jina la Yesu Kristo haipimiki.Sikia ,
nguvu ya mabomu na hata milipuko yote inapimika lakini nguvu iliyopo katika jina Yesu Kristo haipimiki na Uweza wake Yesu Kristo bado unafanya kazi hata sasa,yeye aombaye kwa jina hilo hatakiwi kuona shaka ndani ya moyo wake hata kidogo.

● Mashaka,hofu,woga huletwa na shetani.
“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. ” 2 Timotheo 1:7
Shetani amewafunga watu katika hili eneo,sababu anajua akikuletea hofu basi hakika utakuwa na mashaka kwa kile ukiombacho. Mlima wowote hauwezi kuondolewa na mtu mwenye kuona shaka moyoni mwake,kwa maana siri ya ushindi ni kuamini kwa moyo wote.
Ngoja nikupe mfano kidogo;
~ Kulikuwa na wanamaombi sehemu fulani huko kijijini. Nao walikutana kwa maombi ya kuleta mvua,kisha wakaomba kwa mzigo ili mvua ije siku ya kesho yake ili wapate maji ya kutosha pale kijijini. Wakamaliza maombi yale na wakaambiana wakutane siku hiyo ya mvua yaani kesho yake.
child-praying-300x147Siku hiyo ilipofika,mtoto mmoja aliyekuwepo katika yale maombi akaja na mwamvuli,wale watu walipomuona yule mtoto wakamshangaa kwa nini kabeba mwamvuli.
Yule mtoto akawaambia ” Jana tuliomba mvua inyeshe leo,hivyo nimekuja na mwamvuli ili nisilowe ” ….
Mtoto huyu ndie alikuwa na imani,wala hakuona shaka moyoni mwake maana aliamini ya kwamba mvua itanyesha tu kwa sababu aliomba. Ila wale wakubwa ingawa waliomba lakini hawakukumbuka kabisa kama waliomba mvua,wala hawakubeba chochote. Wakubwa hawa waliona shaka mioyoni mwao,hawakuwa na imani timilifu.
Ndivyo tulivyo wengi tuombao kwa jina lake Yesu Kristo,kwamba tunaomba lakini tunafanana na wale wakubwa wenye mashaka mioyoni mwao.
● Kuomba sio ishu,ishu ni kutokuwa na shaka moyoni mwako.
Laiti kama usingekuwa na shaka moyoni mwako kwa kile ukiombacho mpaka sasa,basi hakika kingekuwa chako.
Yesu Kristo Yeye,tunaposoma habari zake zote,hakuwahi kuona shaka moyoni mwake alipoomba au alipomuombea mgonjwa. Maana mara nyingi alimwambia mgonjwa inuka uende zako imani yako imekuponya~ maneno haya hayawezi kutolewa na mtu mwenye kuona shaka moyoni mwake.

Sasa unisikilize mpendwa;
~ Moyo wa mwanadamu unaweza kuona mambo mawili tu pindi mtu aombapo;
( i ) Unaweza kuona shaka~ Hali ya kutokuamini.
( ii ) Unaweza kutokuona shaka ~ Hali ya kuamini na kusonga mbele kwa ushindi.

Hakili ya mtu kamwe haioni imani bali moyo wake. Na ndio maana tunasoma ” Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki,…” Warumi 10:10.
Mkristo safi aliyeokoka,inampasa aombe pasipo kuona shaka,ili aweze kung’oa kila aina ya milima katika maisha yake.Hakuna mlima usioweza kung’olewa kwa mtu wa Mungu mwenye kuomba pasipo shaka..Unatakiwa uombe kisha unapokea pale pale katika moyo wako ya kwamba yamekuwa yako tangu saa ile. Na hakika yanakuwa yako katika ulimwengu wa kiroho kwanza.
Biblia inaposema yeyote atakayeuambia mlima huu ng’oka utupwe baharini… ( Marko 11:23 ) . Biblia haimaanishi kila mtu atasema tu hivyo basi halafu mambo yakajiseti yenyewe,bali inamaanisha kila atakaye amini katika Kristo Yesu,ndiye atakayesema juu ya mlima na kupokea pasipo shaka moyoni mwake.
Ukifanya maombi,wewe amini na itakuwa hivyo. Naomba niombe na wewe mpendwa katika jina la Yesu Kristo,kupitia namba yangu hii;
0655-11 11 49.

UBARIKIWE.

Comments