UTAWEZAJE KUTULIA IKIWA MUNGU AMEKUPA AGIZO?


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze kuhusu maagizo ya MUNGU na umuhimu wake.
Yeremia 47:7 Biblia inasema ''Utawezaje kutulia, Ikiwa BWANA amekupa agizo? .........  ''
Ni swali hilo anauliza Yeremia Nabii, Yeremia alikuwa na uzoefu wa kuagizwa na BWANA MUNGU, alijua ya kwamba hawezi kutulia ikiwa MUNGU amempa agizo fulani la kutekeleza.
Agizo la MUNGU kwako ni muhimu sana maana agizo hilo linaweza likaambatana na baraka zako zote.
Mimi Peter nilijiunga facebook mwaka 2011 mwishoni, lengo langu mtandaoni lilikuwa kusoma vichekesho na kufurahi, pia nilitaka kuwa napost vichekesho pamoja na habari za mpira wa miguu. Nilipenda kubishana kuhusu soka, siku timu yangu ikishinda nilikuwa wa kwanza kuwa mtandaoni ili niwasanifu timu pinzani. Nilikuwa nimeokoka lakini wala sikuwa na muda hata dakika moja wa kutuma Neno la MUNGU, Nilijiepusha tu na post za matusi na ngono. baada ya mwaka mmoja yaani ilipofika mwaka 2012 hali ilibadilika, nilitamani kuwashirikisha upendo wa MUNGU watu ambao hawajaokoka ila nilikua kama najaribu tu na kuacha zaidi sana nilipenda sana kujadili siasa na michezo. Siku moja miezi ya mwishoni ya Mwaka 2012 nilianza kusikia hukumu moyoni mwangu kwamba kwanini sitaki kuwahubiria watu?  nilitoa hoja mara kwa mara kwenye maombi kwamba sina website wala blog kwa ajili ya kupost Neno la MUNGU. Msukumo ulipozidi nilianza kutafuta namba za bloggers wakristo ili wanitengenezee blog kwa lengo la injili, ajabu kila niliyempigia hakupatikana, nilikata tamaa na kuacha mpango huo lakini MUNGU kwa sababu ya agizo lake alilotaka nilitekeleze mimi alinipa ujumbe kwa njia ya ndoto jinsi ya kutengeneza Blog, nikatengeneza blog yangu ya Maisha ya ushindi. baada ya hapo nikawa sina udhuru tena lakini nikawa naogopa kupost maana watu wengi mambo ya MUNGU yaliyo sahihi hawayapendi, wanapenda uongo na uzushi tu. Nilijaribu kupost post mbili tofauti, moja ya Neno la MUNGU na nyingine ya kawaida tu. ile ya neno la MUNGU haikupata hata likes 5 lakini ile ya kawaida ilipata likes zaidi ya 70, nikaona hakika kupost Neno ni mzigo mzito sana. Lakini kila nikiingia kwenye maombi agizo la MUNGU likawa pale pale kwamba injili yake lazima imfikie kila mtu. Agizo la MUNGU nikaamua kulitii na injili ikaanza. baada ya miezi kadhaa nikawa napost neno na mpira pia lakini MUNGU akamtumia ndugu mmoja ambaye kwenye post yangu ya mpira aka-comment kwamba anashuhudiwa moyoni mwake kwamba mimi Peter sitakiwi kupost chochote zaidi ya Mambo ya MUNGU. Hakika siku hiyo niliogopa na kuamua kumtii MUNGU. Namshukuru MUNGU kwa mimi kufanikiwa kulitii agizo lake, vipingamizi ni vingi sana na matusi ni mengi sana maana injili ya mtandaoni ni ngumu zaidi, maana unaweza kukemea dhambi, mfano unakemea uzinzi na ndugu mmoja yuko gesti tayari kwa kufanya ujinga huo, ndugu kama huyo asipoogopa lazima akutukane tu, unamkemea mtu yuko kwenye gari tayari kwa kwenda kwa mganga wa kienyeji, mtu kama huyo asipoingiwa na hofu ya MUNGU lazima tu akutukane matusi makubwa makubwa. Wapinga kristo ndio wengi sana lakini  naamini BWANA amenipa roho ngumu maana kadili ninavyopingwa ndivyo ninavyoongeza zaidi kuandaa masomo.

-Nimesema kwamba agizo la MUNGU wakati mwingine huambatana na baraka zako, hivyo kulitii agizo la MUNGU ni kupokea baraka pia, mfano September 2014 nilifunga ndoa, Wakati nakaribia kufunga ndoa mazingira ya kiuchumi yalikuwa mabaya sana,  hakika nilikwama lakini MUNGU ni mwema sana, siku chache kabla ya kwenda Mwanza kufunga ndoa niliandika fecebook kwamba '' Natarajia kufunga ndoa tarehe 20 Sept 2014'' lakini neno hilo tu likasababisha marafiki ambao hata hatujawahi kuonana na wala hata wengine hata kuwasiliana tu hatujawahi lakini jumla yao walinichangia zaidi ya Laki 7, ulikuwa ni moja ya miujiza ya ajabu zaidi kuwahi kutokea maishani mwangu. nilifanikisha jukumu lililokuwa mbele yangu kwa msaada wa hao ndugu ambao hata sikuawaomba na hatujawahi kuonana, inaweza kuwa pesa ndogo kwako lakini kwangu mimi ulikuwa ni muujiza mkuu sana. Ninachojua ni MUNGU alinibariki kupitia ndugu wale ambao hata sikuwaomba pesa ila niliandika tu tukio..'' Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake. -Zaburi 112:1''



Ndugu zangu, MUNGU humtumia mtu yeyote ili kulitimiza kusudi lake, ndugu usije ukakwepa agizo la MUNGU hata siku moja. Maagizo ya MUNGU ni mengi lakini ikitokea MUNGU amekupa agizo hakikisha unalitekeleza.
-MUNGU alimtuma Yona kwenda Ninawi, Yona alitaka kutoroka lakini agizo la MUNGU lilikuwa pale pale.
-Musa alipoitwa na MUNGU na kupewa agizo la kuwatoa Waisraeli Misri Musa alitoa udhuru mara 5 lakini agizo la MUNGU likawa pale pale. Ndugu usije ukakwepa agizo la MUNGU maana agizo hilo linaweza kuambatana na baraka zako zote. Kama MUNGU amekupa agizo la kuwaombea watumishi omba, kama umepewa agizo la kuwaonya watu fulani hakikisha unawaonya, kama umepewa agizo la kumbariki ndugu fulani hakikisha unalitimiza agizo hilo maana huwezi kujua kwanini MUNGU amekuagiza wewe. Hata kama umepewa agizo la kuwaonya wakuu wa nchi, ndugu timiza agizo la MUNGU. '' Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza.-Mika 6:9''
-MUNGU haji mwenyewe kuwaonya watu ila anatumia watumishi wake watiifu, ndugu zangu hata sasa mwisho u karibu na nyakati hizi ni za hatari  lakini MUNGU anasema ''Tubuni kwa maana ufalme wa MUNGU umekaribia-Mathayo 3:2'' Hilo ndilo agizo ambalo mimi binafsi nimeambiwa nimwambie kila mtu mwaka 2015.

Ndugu yangu, kutii maagizo ya MUNGU ni kumtii MUNGU.
Yeremia 1:6-10 ''  Ndipo niliposema, Aa, BWANA MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.''
-Yeremia alitaka kukwepa maagizo ya MUNGU kwa kusema yeye ni mtoto lakini agizo la MUNGU lilikuwa pale pale. Ndugu yangu , kama MUNGU amekuagiza kutenda kazi yake usitoe udhuru, usiseme kwamba wewe hujui Biblia na wala usiseme kwamba wewe umeokoka tu hivi karibuni, Timiza agizo la MUNGU maana agizo hilo linaambatana na baraka zako. Watu wengi wamekwepa maagizo ya MUNGU, Ndugu kama kuna agizo umelikwepa hakikisha unarudi na kutubu kisha kutenda agizo hilo. BWANA YESU kila siku anaagiza wateule wake kushuhudia injili na hakika kanisa au waliookoka hawatakiwi kukwepa kuwashuhudia wengine injili. Kaka yawezekana kabisa mkeo hata bado hajaokoka japokuwa wewe umeokoka,  na hata wewe dada yawezekana kabisa mmeo bado hata hajaokoka na ni lazima aokoke kwanza ndipo MUNGU atawaunganisha katika utakatifu wake lakini kwa sababu ya kutokushuhudia kumbe unazuia hata baraka zako mwenyewe. Fanya agizo la MUNGU la kuwashuhudia wengine habari njema za ufalme wa MUNGU.

USITULIE IKIWA MUNGU BABA  AMEKUPA AGIZO.
USITULIE IKIWA BWANA YESU AMEKUPA AGIZO.
USITULIE IKIWA ROHO MTAKATIFU AMEKUPA AGIZO.
Hakikisha tu umeagizwa na MUNGU, Wengine hujiagiza na kudanganya watu hao hawajui walitendalo.
Maombolezo 3:37 ''Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa BWANA hakuliagiza?''
-Natamani niendelee sana lakini kwa leo inatosha na naamini kuna kitu umejifunza, siku moja somo hili litaliweka kwenye kitabu likiwa na ufafanuzi mzuri zaidi.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments