VIZUIZI KUMI(10) VINAVYOZUIA MAOMBI YAKO USIPOKEE ULICHOOMBA KUTOKA KWA MUNGU.(1)

BWANA YESU asifiwe.
Karibu tujifunze ujumbe wa kutuvusha kutoka sehemu mbaya na kuingia sehemu nzuri.
Watu wengi hupenda sana kuombewa na hata kuomba pia.Hutamani wapokee kile walichoomba lakini muda mwingine hawapokei, Tatizo sio la MUNGU bali tatizo ni la wewe unayeomba.
Kwa leo nimekuandalia vizuizi 10 vya maombi ambavyo ukivitendea kazi maombi yako yatakuwa na matokeo mazuri sana,

''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.-1 Yohana 5:14-15.''
-Kumbe lazima kwanza tuombe sawa sawa na mapenzi au matakwa yake MUNGU.
Hayo matakwa yake ni yapi? 
Hebu ndugu ona  vizuizi hivi kumi vya maombi yako ndipo utajua matakwa au mapenzi ya  MUNGU hata akajibu maombi yako.

VIZUIZI KUMI(10) VYA MAOMBI.

       1. UCHUNGU NA KUTOKUSAMEHE: Mathayo 5:22-24 '' Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.   '' 
-Uchungu maana yake ni kukaa na jambo moyoni.
-Moyo ni kwa ajili ya ROHO MTAKATIFU na sio vinginevyo
-Sadaka sio bora kuliko msamaha, samehe kwanza ndipo na utoaji wako utakuletea baraka kuu.
-Usikubali kuwa na hasira kwa ajili ya watu.Mathayo 6:14-15 ''Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.  ''
-MUNGU hatakupa hicho ulichomuomba hadi usamehe kwanza.MUNGU ana kanuni zake lazima tuzifuate ndipo tutapokea baraka zetu baada ya maombi. Umelala na uchungu na umeamka na uchungu hiyo haina faida kwako hata moja hivyo achilia kwanza na MUNGU atakujibu hitaji lako. Kuna watu mioyoni mwao hakuna ROHO MTAKATIFU ila kuna watu tu waliowaweka moyoni ambao waliwaudhi. Ndugu ondoa watu moyoni mwako na muweke ROHO wa MUNGU.

         2.  DHAMBI ZA MAKUSUDI ZISIZOUNGAMWA: Zaburi 66:18 ''Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, BWANA asingesikia.   ''
-Kama unakusudia mabaya maana yake ni dhambi na hakika MUNGU atakusikia maombi yako. Tubu kwanza dhambi yako.
-Kama hujaungama MUNGU hatasikia maombi yako na hutapokea ulichoomba kwake.
-Ukichagua kumkimbia  MUNGU  kwa kufanya dhambi utakuwa umejitenga na MUNGU na kwa kujitenga na MUNGU hakika hutajibiwa hitaji lako.
-Tukiwaza maomvu mioyoni mwetu MUNGU hatasikia maombi yetu.

      3.   MIZOZO ISIYOTATULIWA NA MAOMBO YA NYUMBANI: 1 Petro 3:7 '' Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.   ''
-Mizozo ya kwenye familia yako inaweza kuzuia maombi yako.
-Hata kama ni muombaji kiasi gani lakini kama kila siku mnapigana au kutukanana na mwenzi wako wa ndoa hiyo inaweza kuzuia maombi yako. Tafuta wapi ulipoangukia ukatubu. Uanweza ukasema mbona mwaka unaisha MUNGU hata hajajibu ombi langu la mtoto kumbe tatizo ni mizozo isiyoisha kwenye familia yako.

        4.  DHAMIRI MBAYA:Wagalatia 6:3-4 '' Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake  ''
-Unaweza ukajiona ni kitu kumbe si kitu kwa sababu ya dhamiri yako mbaya. kila saa unawaza mabaya. Ndugu waza mema maana kuwaza mabaya kunaweza kukunajisi wewe.
-Usijifananishe na watu wengine. BWANA YESU alisema neno hili kati ya mtu mwenye dhamiri mbaya na asiye na dhamiri mbaya. Luka 18:10-14 '' Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee MUNGU, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee MUNGU, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. ''
-Dhamiri yako kama ni mbaya hakika hutajibiwa maombi yako.

       5.  KUTOKUMPA MUNGU NAFASI YA KWANZA: Malaki 1:6-10 ''Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni BABA yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni BWANA wenu, kicho changu ki wapi? BWANA wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani? Mnatoa chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu Nanyi mwasema, Sisi tumekutia unajisi kwa jinsi gani? Kwa sababu mwasema, Meza ya BWANA ni kitu cha kudharauliwa. Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema BWANA wa majeshi. Na sasa, nawasihi, ombeni fadhili za MUNGU, ili atupe neema; ikiwa jambo hili limetoka katika mikono yenu; je! Atawakubali nafsi zenu? Asema BWANA wa majeshi. Laiti angekuwapo kwenu mtu mmoja wa kuifunga milango; msije mkawasha moto bure madhabahuni pangu! Sina furaha kwenu, asema BWANA wa majeshi, wala sitakubali dhabihu yo yote mikononi mwenu. ''
-Watu wengi leo MUNGU ni ziada tu kwao.
-Watu wengi maombi kwao pia ni ziada tu, hutaka tu kuombewa.
-Ndugu zangu, MUNGU anataka atuongoze yeye na sio sisi tumuongoze MUNGU jambo ambalo halitawezekana.
-Ndugu, najua umekuwa makini sana kwenye mambo yako ya kidunia, ndugu maombi yako yanaweza kutokujibiwa kwa sababu MUNGU umemfanya kuwa ziada tu kwako. Watu wengi ukiwauliza kwanza '' kitu cha kwanza na cha muhimu maoishani mwako watasema ni MUNGU lakini matendo yao hata hayaonyeshi kwamba MUNGU ni wa kwanza katika maisha yao.''. Kuna watu wengi tumewaombea lakini walipopokea tu uponyaji wao hata BWANA  wakamsahau na hiyo inaonyesha kabisa kwamba wao hawakumhitaji MUNGU ila walihitaji tu uponyaji na baraka zake.
-MUNGU lazima awe nafasi ya kwanza maishani mwetu.

 Luka 14:26 '' Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.   ''
-Ndugu zangu BWANA hana maana kwamba tuwachukie wazazi au wake/waume zetu au watu wengine wowote bali MUNGU wetu anataka apewe kwanza yeye nafasi ya kwanza maana ndio nafasi yake milele yote. Maana kama baba yako atakukataza kuokoka na wewe ukakubali maana yake umemtii baba yako kuliko MUNGU lakini ukimtii MUNGU kwa kuokoka utamchukiza baba yako lakini kwa MUNGU wewe utaitwa heri maana umemtii mwenye uzima wako wa milele.
-Tukishindwa kumpa MUNGU nafasi ya kwanza ni madhara kwetu maana tutakuwa mbali naye tu.

  Ufunuo 3:16 ''Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.''
-MUNGU hawahitaji watu ambao wako uvuguvugu yaani nusu wako kwake MUNGU na nusu wako kwa shetani.
-Ndugu zangu kama kuna jambo la kwanza katika maisha yetu basi MUNGU aliyetuumba  awe wa kwanza.
-MUNGU akikuacha utaenda kwa nani?
-Leo watu wengi ni vuguvugu kitu ambacho ni hatari sana.
-Ndugu, BWANA MUNGU anahitaji zaidi muda wako na hapo ndipo utakuwa na sifa za kuomba na kujibiwa.
Somo ni zuri sana na sehemu ya mwisho itafuata kesho.
Usikose. 
Kumbuka vizuizi vitano ndio vimebaki, ni muhimu kuvujuia nakuomba tu ungana nami hapa kesho tumalizie kujifunza jambo hili muhimu. 
Kwa sasa naishia hapo, somo litaendelea .na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.


Comments