VIZUIZI KUMI(10) VINAVYOZUIA MAOMBI YAKO USIPOKEE ULICHOOMBA KUTOKA KWA MUNGU.(2)

BWANA YESU asifiwe.
Karibu tujifunze vizuizi vitano vya mwisho ambavo vinaweza kuzuia maombi yako.
 Maombi ni muhimu sana, BWANA YESU nasema  ''Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na BABA yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao-Mathayo 18:19-29.
Baana ya kuzungumzia vizuizi 5 vya kwanza vya maombi yako , na sasa tunamalizia sehemu ya mwisho yaani vizuizi vitano vilivyobaki.

6. KUTOKUOMBA IPASAVYO: Yakobo 4:2  '' Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! ''
-Kuna watu hata hawana muda wa kuomba lakini hutaka na kutamani sana MUNGU awape mahitaji yao.
-Kutokuomba ipasavyo ni moja ya kizuizi cha kupokea baraka kutoka kwa MUNGU.

7.  KUTOKUWA WASIKIVU: Isaya 28:23 ''Tegeni masikio, sikieni sauti yangu, sikilizeni mkasikie neno langu. ''
-Watu wengi humuomba MUNGU kuhusu baraka fulani na BWANA nae kabla ya kuwapa husema nao ili watengeneze vitu fulani katika maisha yao hata kuruhusu baraka iwajie lakini watu walio wengi huwa si wasikivu na kupelekea kutokua watii na hayo yakitokea hupelekea kutokujibiwa maombi yao.
-Hebu mfano wewe jigeuze yule mama wa Salepta wakati wa Nabii Eliya ambaye alitaka BWANA ambariki chakula, lakini jibu la MUNGU likawa yule mama ampe Eliya Chakula, alipotii alibarikiwa hata isiwepo sehemu ya kubaki. Leo ni wangapi ambao wangemuomba MUNGU harafu MUNGU akasema nao neno gumu kama hilo la mama wa Salepta lakini bado wao wakatii? Huo ni mfano tu lakini MUNGU husema na sisi waombaji kwa namna nyingi, ni vizuri kuwa wasikivu na watii. Kumb 28:1-7 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, MUNGU wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, MUNGU wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, MUNGU wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.  Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.   ''
-Baraka hizi zitakuja kwa sababu ya kuitii sauti ya MUNGU.
-Kuitii sauti ya MUNGU ni muhimu sana. 
-Kama huitii sauti ya MUNGU hata ungeombaje huwezi kupokea.

8. UBAYA NA UDHALIMU: Mika 3:4 '' Ndipo watakapomwomba BWANA, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao.   '' 
-Mitindo ya maisha inaweza kusababisha mtu asijibiwe maombi yake.
-Matendo na usemi mbaya unaweza kuwa kikwazo cha kupokea kutoka kwa MUNGU hata kama unaomba sana maana maovu hayo yatauficha uso wa MUNGU. Zaburi 34:15-16 ''Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.  ''

9. KUOMBA VIBAYA: Yakobo 4:3 '' Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.  '' 
-Kuomba vibaya ina maana nyingi sana. Kuna watu huomba kwa lengo la kushindana na watu wengine.
-Wengine hawaombi bali wanalalamika tu mbele za MUNGU, Mfano wanandoa wengi huwalaumu wenzi wao kwa kuwaona kwamba wao ndio chanzo  cha kila aina ya tatizo kwenye ndoa kumbe tatizo wakati mwingine linaweza likawa la mlalamikaji. Wengi hufikia hata kuomba sasa kumbe hapo ni kulalamika tu kwa MUNGU maana tatizo ni la muombaji. Unaweza ukasema '' BABA wa mbinguni finyanga moyo wa mke/mme wangu '' kumbe alitakiwa aombe kwanza yeye atengenezwe moyo wake maana yeye ndio tatizo.
-Wengine huomba kwa kutaka kubalikiwa kama mtu fulani ambaye wanamfahamu. Ndugu fulani ni fulani na wewe ni wewe, omba  uwe kama wewe sio kama alivyomtu fulani.
-Kuomba vibaya ina maana nyingi sana.

10.   KUTOKUOMBA KWA IMANI: Waebrania 11:6 ''Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.   ''
-Usimwendee MUNGU kwa kujaribu.
-Hata kama unaumwa kiasi gani na ugonjwa gani kama umeamua kumwomba MUNGU basi omba kwa imani.
-Wengi huenda kwa YESU kwa kujaribu tu ndio maana hata hawapokei walichokiomba.
Naamini umejifunza kitu kizuri.
 Warumi 8:26-27 ''Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU. ''
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.

Comments