WAISRAELI WOTE ULAYA WATAKIWA KURUDI NYUMBANI ISRAEL

 Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu 

Waziri Mkuu wa Israel amewataka Wayahudi wote wanaoishi Ulaya kurejea Israel, kwa kuwa nyumbani kuna nafasi ya kila Myahudi. 
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameweka msimamo huo wazi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi yao, ambapo juzi Myahudi mmoja aliuwawa nchini Denmark, tukio ambalo limekuja siku chache baada ya shambulio la namna hiyo nchini Ufaransa.

 Akizungumza kwenye baraza la usalama na baraza la mawaziri, Bwana Netanyahu alieleza kwamba kwa kadri ambavyo Wayahudi wamekuwa wahanga kwenye mashambulizi mbalimbali, ni vema wakarejea nyumbani ambakokuna usalama zaidi, ambapo wanaweza kulindwa. "Wayahudi wanastahili kulindwa kwenye taifa lolote, lakini kwa kadri mambo yalivyo, tunawaambia kaka zetu na dada zetu walioko nje, Israel ni nyumbani kwenu". Amenukuliwa Benjami Netanyahu. 
 
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akiwasili kwenye mkutano wa kila wiki na baraza la mawaziri. 

Matokeo ya mkutano huo ilikuwa ni kukubaliana kupitisha bajeti kiasi cha dola milioni 46 ambazo ni takriban zaidi ya shilingi bilioni 80 za Kitanzania kwa ajili ya kuwezesha mpango wa Wayahudi hao kurudi nyumbani, Israel. 

 Kufuatia tamko hilo, mataifa kadhaa yalionyeshwa kutopendezwa, Ufaransa ikiwa ni taifa mojawapo, ambapo Waziri Mkuu wa taifa hilo, Manuel Valls amepinga na kusema kuwa, "Ufaransa bila Wayahudi siyo Ufaransa tena." Wayahudi waishio Ufaransa wamekuwa wakirejea Israel kufuatia mashambulizi mbalimbali, jambo ambalo limeonekana kuwagutusha viongozi nchini humo, kwa mwaka 2014 pekee, Wayahudi takribani 7000 wamereja Israel, kiwango ambacho kimeongezeka zaidi ya mara mbili kulinganisha na mwaka 2013. 

Tukio la kuondoka Ufaransa lilishika kasi mwaka 2012, mara baada ya mtu mmoja aliyefahamika kama Mohammed Merah kushambulia shule ya Kiyahudi Jijini Touluse, ambapo watoto 3 na rabbi mmoja waliuwawa. Mwezi Januari pia kumekuwa na shambulizi nchini humo, ambapo watu 17 waliuwawa na kundi linalodai kuwa na uhusiano na vikundi cha al-Qaida na Islamic State.

 Kwa upande wa Denmark, Waziri Mkuu Helle Thorning-Schmidt ameeleza masikitiko yake kutokana na shambulio ambalo lilipelekea mauti ya mtengenezaji mmoja wa filamu pamoja na mwanajumuiya ya wayahudi kwenye nchi za Scandinavia, shambulizi ambalo limefanywa Jumamosi karibu na Sinagogi kuu Copenhagen. 
 
Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning-Schmidt "Kwao ni Denmark, wao ni sehemu ya jamii yetu yenye nguvu", ananukuliwa mwanamama Helle.

 Kwa upande wake rabbi mkuu wa Copenhagen, Jair Melchior amechukizwa na tamko hilo la Netanyahu na kusema kwamba kama ni hivyo basi nafuu wangeenda kuishi kwenye kisiwa kilichojitenga kama ni kuhofia ugaidi. "Watu kutoka Denmark wanahamia Israel kwasababu wanaipenda Israel, kwasababu ya Uyahudi lakinisio kutokana na ugaidi. Kama namna pekee ya kushighulika na ugaidi ni kwa kukimbia kimbia, basi sote na tukimbilie kwenye kisiwa kilichojitenga."

Comments