YAONDOENI HAYA: ASKOFU ZAKARIA KAKOBE.


Na Askofu Zakaria Kakobe.
     L
eo tena, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo tunajifunza YOHANA 2:12-25.  Kichwa cha somo letu la leo, ni “YAONDOENI HAYA”.  Hata hivyo, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii. Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinne:-
(1)MAKAO MAKUU YA HUDUMA YA YESU (Mst. 12-13);
(2)YAONDOENI HAYA (Mst.14-17);
(3)KUTAMBUA MAMBO YA MUNGU KWA JINSI YA ROHONI (Mst. 18-22);
(4)KUMWAMINI YESU BAADA YA KUZIONA ISHARA (Mst. 23-25).

(1)      MAKAO MAKUU YA HUDUMA YA YESU (Mst. 12-13)
            Katika mistari hii, tunajifunza juu ya Makao Makuu ya Huduma ya Yesu Kristo.  Makao Makuu ya Huduma ya Yesu Kristo, yalikuwa KAPERNAUMU, karibu mwendo wa siku moja kutoka KANA, mji wa Galilaya.  Kwa msingi huu, KAPERNAUMU uliitwa MJINI KWAKE.   Baada ya huduma yoyote aliyoifanya, wakati wowote wa mapumziko, alirudi Kapernaumu na kupanga safari nyingine ya Injili (Mst. 12; MATHAYO 4:13; 8:5; 9:1; MARKO 1:21; 2:1).  Kanisa la Kwanza pia lilikuwa na Makao Makuu, Yerusalemu (MATENDO 8:1, 14, 25).  Hatimaye baada ya Injili kuanza kupelekwa kwa Mataifa, Yerusalemu ilibaki kuwa Makao Makuu ya huduma kwa Wayahudi; na ANTIOKIA ikawa Makao Mkuu ya Huduma kwa mataifa (MATENDO 11:25-26; 13:1).  Kwa misingi hii, ni Ki-Biblia kuwa na Makao Makuu ya Kanisa.  Makao Makuu ya Kanisa la FULL GOSPEL BIBLE FELLOWSHIP, ni DAR ES SALAAM.  Wajibu wa Makao Makuu kwa matawi yaliyoko mikoani ni kama wajibu wa baba au mama kwa watoto wake au wajibu wa shina kwa matawi.  Kama Makao Makuu, tunapaswa kufahamu wajibu wetu wa kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kazi ya Mungu.  Sadaka zetu za kila siku pamoja na mafungu yetu ya kumi ya mapato yetu, siyo tu kwamba yanatumika katika kuboresha kazi ya Mungu Makao Makuu, lakini sadaka hizi zinatumika kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na matawi yaliyoko katika mikoa yote.  Tunapaswa kuwa waombaji wakubwa pia, tukijua kwamba Shetani atafanya kila mbinu kuhakikisha huduma ya Makao Makuu inavurugwa kwa njia moja au nyingine.  Tunapaswa kuombea kwa bidii kazi ya Mungu mikoani tukijua matunda yanayopatikana huko, ni matunda yetu pia.  Vivyo hivyo, wote walioko Makao Makuu na mikoani kote, ni wajibu wetu kila siku kuomba kwa bidii kwa ajili ya MWANGALIZI MKUU WA KANISA LA FULL GOSPEL BIBLE FELLOWSHIP, TANZANIA; tukijua kwamba Shetani analenga kumpiga yeye ili kondoo wote watawanyike (MATHAYO 26:31; 1 WAFALME 22:31-33), na pia ni muhimu kuomba kwa ajili ya Kanisa lote kwa ujumla.  Wajibu mwingine wa Makao Makuu, ni kuwa kielelezo kwa wote waaminio katika matawi yote mikoani (1 WATHESALONIKE 1:7-8).  Ni wajibu wa kila mmoja Makao Makuu, kuwa KIELELEZO kwa ndugu zetu mikoani katika utii, unyenyekevu kwa viongozi wetu, usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi (2 WAKORINTHO 7:14-15; 1 TIMOTHEO 4:12).  JAMBO JINGINE TUNALOJIFUNZA HAPA NI KWAMBA, WANAFUNZI WA YESU hawakukubali kumwacha Yesu.  Popote alipokwenda, wao nao walitaka kwenda naye (Mst. 12).  Yesu Kristo ilibidi wakti mwingine “kuwalazimisha kutengana naye (MATHAYO 14:22).  Hii ndiyo siri ya wao kutumiwa sana na Mungu na kuwa msaada kwa wengi katika Kanisa la Kwanza.  Sisi nasi tukitaka kutumiwa hivyo hatupaswi kumwacha Yesu.  Tuhudhurie katika kila Ibada ya Kanisa Kuu, Jumatatu, Jumatano, Jumapili na pia Jumamosi katika Makanisa ya Nyumbani, na kuambatana na Yesu kaatika neno lake kila mahali linapotupeleka.  Tunaona hapa pia, kwamba, hawakukaa huko siku nyingi naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu kwenye Pasaka ya Wayahudi.  Yesu anatufundisha hapa kutoa nafasi kwa mambo makubwa na kuyaacha madogo.  Mtu akisema, “Leo sitakuja katika ibada ila nimeonelea vema nifanye maombi nyumbani kwangu”, mtu huyu hafuati mfano wa Yesu wa kuacha madogo na kutoa nafasi kwa mambo makubwa.  Ibada ni jambo kubwa kuliko kuomba binafsi, kufuatilia watoto wachanga, kusoma neno mwenyewe nyumbani n.k.  Pasaka ya Wayahudi, inaitwa hivyo, kutokana na jinsi ilishikwa na Wayahudi peke yao kwa namna ile ya mwanzo.  Leo Pasaka wetu ni Yesu, huyu tunamshika wote.

(2)      YAONDOENI HAYA (Mst. 14-17)
             Baada tu ya Yesu kuingia Yerusalemu, alianza kulisafisha hekalu.  Wakati wa Pasaka ya Wayahudi, wanyama wengi sana walihitajika kuchinjwa kwa ajili ya sadaka mbalimbali za kuteketezwa.  Waandishi wa Karne ya Kwanza wanasema kwamba walichinjwa wanyama kufikia 256,500 kila Pasaka ya Wayahudi.  Wanayma hawa waliuzwa sokoni ili kila mtu aje anunue, na makuhani katika tama yao ya fedha walisogeza soko hilo na kulifanya liwe ndani ya hekalu.  Makuhani walitoza kodi ya mauzo kwa kila mnyama.  Wenye kuvunja fehda, kazi yao ilikuwa kubadili fedha za wageni ili kuwapa shekeli ambayo ndiyo ilikuwa fedha pekee ya kutolea kodi ya hekalu.  Fedha nyingine za wageni zilikuwa na picha za miungu, hivyo hazikufaa kutoa kodi ya hekalu.  Wavunja fedha walitumia kipindi hiki kuwadhulumu wau , kwa kibali cha makuhani waliowapa rushwa.  Soko hili la fedha pia lilifanyika hekaluni, kinyume na kawaida.  Ndiwa pia waliuzwa hekaluni kwa wale waliowahitaji kwa kuwatoa kama sadaka ya kuteketezwa (WALAWI 1;14).  Katika mazingira haya, Yesu alitwaa kikoto cha kambaa (fimbo yenye michirizi mingi ya kamba ubavuni mwake).  Kikoto hiki kilikuwa ni alama ya mamlaka ya kifalme, na siyo fimbo ya kawaida ya kupiga watu.  Kwa kawaida ilikuwa ni desturi ya Wafalme waliompeneza Mungu kutumia Mamlaka waliyo nayo kusafisha kila namna ya dhambi na uchafu wote katika hekalu kabla ya Pasaka.  Hivi ndivyo walivyofanya Hezekia na Yosia (2 NYAKATI 30:1, 13-15; 2 WAFALME 22:3; 23:4-24).  Ikiwa sisi pia tunataka kuuona uwepo wa Mungu katika makusanyiko ya ibada zetu au mikutano yetu ya Injili, lazima tuzingatie maneno ya Yesu, “YAONDOENI HAYA”.  Kila kilicho uchafu, kilicho dhambi na kisicholeta ushuhuda wa wokovu wetu, hatuna budi kukiondoa katika Kanisa.  Uasherati, kucheza “disco” katika Kanisa, kuvaa kama mataifa, uasi kwa viongozi na uasi wa Neno la Mungu, masengenyo, sanamu za aina zote, “maji ya baraka” kufukiza uvumba, kipaimara, ubatizo wa watoto wadogo, urafiki wa wanawake na wanaume (hakuna girlfriend au boyfriend katika wokovu), mizaha, bahati nasibu n.k; vyote hivi vinapaswa kuondolewa.  Wivu wa nyumba ya Mungu ulimla Yesu, sisi nasi tuige mfano wake na wivu huo utufanye tutamani Kanisa liwe safi na tena liongezeke kila siku.  Kwa nini masinasgogi ya sanamu yawe na watu wengi zaidi kuliko Makanisa ya Mungu?  Wivu wa Nyumba ya Mungu, ututafune!  Vivyo hivyo tunajifunza kuwa, mtu mwenye mamlaka ya Mungu, maneno yake hufuatwa bila kutumia nguvu za kimwili.  Mtu mmoja tu Yesu aliwafukuza maelfu ya watu na mifugo yao!  Ikiwa watu tunaowaongoza hawayafuati maneno yetu basi tumepungukiwa mamlaka ya Mungu.  Tumwendee Mungu kwa maombi!

(3)      KUTAMBUA MAMBO YA MUNGU KWA JINSI YA ROHONI (Mst. 18-22)
            Tutafanya makosa makubwa, tukidhani kwamba kila neno la Mungu, linatafsiriwa kwa akili tu.  Tukifanya hivi, hatuwezi kuielewa Biblia.  Mambo ya Roho wa Mungu yaani Biblia, inatambulika kwa jinsi ya rohoni.  Mtu ambaye hajaokoka, hawezi kamwe kuielewa Biblia!  (1 WAKORINTHO 2:14-15).  Watu hawa walitaka Yesu awape ishara ya kuthibitisha mamlaka yake, akawaambia LIVUNJENI HEKALU HILI nami katika SIKU TATU nitalisimamisha.  Wao walidhani jingo lao la hekalu.  Kumbe alimaanisha “Usulubisheni mwili huu msalabani na kuniua, katika siku tatu nitafufuka”.  Vivyo hivyo tukitafsiri kwa akili “Mwana wa Mungu” na kusema Mungu hazai kwa jinsi ya mwili, hatuwezi kuifahamu Biblia, na mengine ya jinsi hiyo.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
            Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!


Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe  tembelea sehemu zifuatazo.
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments