YAPO MATATU YA MSINGI YANAYOSIMAMISHA KANISA KUWA HAI.

Bwana Yesu asifiwe…
Kanisa halihitaji mambo mengi ili liwe hai kiroho,bali yapo machache ya msingi yenye kulisimamisha kanisa la Bwana. Kupitia mambo hayo matatu tu,basi mambo mengine huzaliwa. Waamini wa leo wamechoka kuendeshwa kwa ibada zisizo hai,wanataka waongozwe na ibada za Roho mtakatifu. Mambo haya matatu ni nguzo katika kanisa la Bwana,ushindi upatikana katika haya matatu,tuyangalie mambo haya kwa ufupi;
01.Maongozi ya Roho mtakatifu.
Kati ya jambo kuu la msingi wa kanisa ni kuwepo kwa maongozi ya Roho mtakatifu.Kanisa pasipo Roho mtakatifu basi hilo si kanisa. Kanisa la kweli ni lile lenye kuongozwa na Roho mtakatifu katika kila kitu,Jambo hili ndilo tunaloliona katika kanisa la kwanza la akina Petro. Kanisa la mitume lile la awali kabisa,halikufanya jambo lolote lile pasipo kuongozwa na Roho wa Bwana. Biblia inasema;
Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. ” Luka 24:49
gasper 2
Na mtumishi wa Mungu Gasper Madumla.
Mitume na wanafunzi wa Bwana Yesu,wanaambiwa wasitoke humo Jerusalem,na wasije wakafanya jambo lolote lile mpaka wavikwe uwezo utokao juu- neno ” Uwezo utokao juu ” ni nguvu za Roho mtakatifu,ambao ni maongozi ya Roho wa Bwana. Hii inaonesha kuwa tegemeo lao lote lilikuwa ni kuongozwa na Roho mtakatifu,kwa kupitia huyo Roho mtakatifu tunaona uhai wa kanisa,tunaona ishara na miujiza ikitendeka,tunaona kanisa likitembea na Yesu maana yu hai,ndipo sasa wanatufundisha sisi wa kanisa la leo kwamba kanisa pasipo Roho mtakatifu basi kanisa hilo si kanisa lililo hai.
Tazama hapa tena,mkazo wa kanisa ni ule ule,mitume wanaambiwa hivi;
” Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. ” Matendo 1:4-5
Hivyo,kanisa lililo hai linatambulikana kwa kuongozwa na kusimamiwa na Roho mtakatifu pekee,na wala sio kuongozwa na kusimamiwa na mwanadamu awaye yote. Mwanadamu huwa chini ya uongozi wa Roho mtakatifu,lakini mwenye kuleta uhai wa kanisa ni Roho mtakatifu.

02.Neno la Mungu.
Kanisa lolote lile lenye uhai ni lile lenye kuhubiri neno la kweli pasipo kupunguza wala kuongeza. Dhambi  inastahili kukemewa kabisa katika kanisa kama vile neno la Mungu lisilokumbatia dhambi. Kanisa lolote likikaa katika neno la Mungu basi kanisa hilo ni sawa na kukaa ndani ya Yesu Kristo,biblia ;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” Wakolosai 3:16
Kukaa ndani ya Yesu ni kulijaza neno lake na kulishika,nasi tukikaa ndani yake naye hukaa ndani yetu. Neno la Mungu ni taa ya njia yetu,kwa neno kanisa uwa hai. Ukihitaji kulijua kanisa la kweli ni lile lenye kuhubiri na kufundisha kweli yote. Kanisa la kweli haliwezi kuongozwa na litrujia ya mwanadamu,bali kwa neno la Mungu aliye hai.
Yapo makanisa leo,hayafundishi ile kweli,makanisa ya namna hii hujaa maongozi ya kibinadamu,mbwembwe na hisia za kibinadamu .NK
Mfano mdogo tu ni huu;
Kanisa la kweli haliwezi kutegemea mafuta,chumvi au vitambaa kama ulizi kwa waamini wake. Ulizi wa kweli ni kwa kupitia jina la Yesu Kristo tu,hakuna kingine kinachoweza kumlinda mtu isipokuwa kwa jina hilo.Mtu hatakaswi kwa ibada ya vitambaa,wala mafuta bali hutakaswa kwa neno la Mungu tu. Imeandikwa; ” Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. ” Yoh.17:17,
Yesu anasema tena kwamba ulinzi wa kweli upo katika jina lake tu,na wala ulinzi haupo katika maji,vitambaa,mafuta,mchanga,chumvi kama wengine wafanyavyo leo N.K;
” Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. ” Yoh.17:12
Msingi wa neno la Mungu ndio msingi wa kanisa la Kristo Yesu,Hivyo Neno la Mungu hulifanya kanisa kuwa hai.

03.Maombi.
Maombi ni ibada inayokimbiwa makanisani,sababu shida kubwa ya kanisa ni maombi. Ikumbukwe ya kwamba majibu yetu yamefichwa katika maombi. Ukitaka majibu yako,basi omba kwa jina la Yesu Kristo ( Yoh.14:14 )
Maombi ni nguzo kubwa sana katika kanisa,nguzo hii huifanya kanisa kuwa hai. Kanisa lililoegama katika muhimili wa kudumu katika maombi huku likiwa na muongozo wa Roho mtakatifu na neno kwa wingi,basi ujue hakuna pepo,mchawi,wala majini yatakayofanya kazi humo,maana ni lazima maroho hayo yatalambwa kama vile ngo’mbe alambavyo majani.
Biblia inaweka wazi jambo hili;
” Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. ” Mathayo 16:18
Bwana Yesu anamuonesha Petro kwamba kanisa la kweli ni lile lisiloshindwa na milango ya kuzimu,kwa lugha nyingine alikuwa akimwambia kanisa la kweli ni lile linalodumu katika kweli likiomba,sababu yule aliye katika kweli ( neno) akidumu katika kuomba,kamwe hawezi kushindwa na nguvu za malango ya kuzimu.
* Kanisa lisipoomba,kupigwa na adui ni lazima,yafaa nini kuwa mkristo pasipo kuomba! Wachawi,au mapepo katika kanisa hawaogopi chochote kile isipokuwa wanaogopa na kukimbia panapo maombi katika Roho. Maombi katika Roho yana nguvu ya ajabu isiyoweza kuelezeka hapa.


Mambo hayo matatu ni muhimu sana katika kanisa la Kristo Yesu. Na ikiwa waamini watafuata hayo,basi ushindi ni lazima.

Kwa huduma ya maombi na maombezi,nipigie kwa namba yangu hii
0655-11 11 49.

UBARIKIWE.

Comments