YEYE ASIYE NA DHAMBI NA AWE WA KWANZA KUKUTUPIA JIWE. ( Yoh.8:7 )

Na Mtumishi Gasper Madumla.
“Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. ” Yoh.8:7-9
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa lugha nyingine Bwana Yesu anawaambia ikiwa kama watu hao hawana dhambi basi wawe wa kwanza kumuhukumu huyo mwanamke. Anawaambia watesi wako siku ya leo kwamba ikiwa kama hawana makosa basi wawe wa kwanza kukuhukumu wewe.
Ndiposa nikajifunza jambo moja kubwa hapo,kwamba;
Hata wenye kukuhukumu wewe,kumbe wao pia wanadhambi za kuhukumiwa,hivyo hawastahili kukuhukumu,pia nikajua kwamba;Usalama wako haupo kwa wanadamu bali usalama wako upo magotini pa Yesu. Ujapowakimbilia wanadamu kwa msaada,msaada wako kamwe hautapitikana kwao,sababu;
Wanadamu wamejaa kuhukumu wakosa hali wao ni wakosaji wakubwa.

Waandishi na mafarisayo hawakujua kwamba usalama wa mwanamke yule ulikuwa ni magotini pa Yesu. Mwanamke alipelekwa mahali ambapo ataiponya roho,nafsi na mwili wake,mwanamke huyu alishangazwa na maamuzi ya kupelekwa kwa Yesu.
Kimbilio lake lilikuwa ni kwa Yesu Kristo wa Nazareti,
ambaye kwake Bwana Yesu;
aliokoa maisha yake,
alisamehewa dhambi zake,
alianza maisha mapya,
alifundishwa msamaha,
alifundishwa toba halisi,
alifundishwa kuishinda dhambi N.K
Sikia;
Haya yote asingeyapata kama asingepelekwa kwa Bwana Yesu. Laiti labda angelipelekwa kwa mwanadamu mwenye moyo mzuri,angeliweza kumuokoa asipigwe mawe lakini asingeliweza kumpatia wokovu,wala asingelimpatia msamaha wa dhambi zake.
Sababu hakuna chini ya jua awezaye kusamehe dhambi za mwenye dhambi isipokuwa Yesu wa Nazareti anaweza,tena kwa jina lake linaweza mambo yote. Hata sisi wachungaji,kazi yetu ni kumpeleka mtu kwa Bwana Yesu ili asamehewe madhambi yake.
Kawaida ipo hivi;
Ukimkimbilia mwanadamu,mwanadamu atakumaliza,atakushambulia na isitoshe mwanadamu hana mbingu,mwenye mbingu ni mmoja tu ni Mungu kwa jina la Yesu Kristo aliye hai.
Utendapo dhambi,usimkimbilie mtu bali umkimbilie Mungu maana Yeye Mungu ana neema rehema na tele.
~ Je ni mara ngapi ufanyapo dhambi unamkimbilia Bwana Yesu kwa toba?
Sababu Yesu Kristo yupo hata leo,anakusubili umwendee kwa toba.
Siku ya leo tunajifunza jambo moja kubwa sana mahali hapa,ya kwamba kimbilio la kweli, tena lenye usalama wa maisha yako ni kwake Bwana Yesu tu.
Ni kweli umetenda dhambi nyingi. Lakini yupo Yesu Kristo wa Nazareti mwenye kuweza kukusamehe,Yeye hashindwi na kitu.
Wanadamu hawana uwezo wa kusamehe dhambi.
Siku moja nilipokuwa mjini Dar. ( Mitaa ya samora evenue,mitaa ya posta) nalimuona mtu mmoja aliyekamatwa na watu wenye hasira juu yake.
Mtu yule alikuwa akihisiwa kuwa ni mwizi,hivyo wakampiga kwa kumwagia tindikali usoni mwake na mwilini mwake kisha mtu mmoja akabeba nyundo kubwa,nyundo zile za kupasua miamba,au zile za kuvunja maghorofa ya mjini akataka ampige nayo kichwani,lakini bahati nzuri palikuwa na askari pembeni aliyezuia kumpiga mtu huyo,hivyo wakampeleka kituoni polisi akiwa hajitambui kwa kumwagiwa tindikali.
Sasa,
~ Je ni sawa kumuhukumu mtuhumiwa kwa kumpiga hali sheria zipo?
~ Je ni kweli wenye kumpiga kwa mawe mwivi,wao hawana makosa/dhambi?
~ Kwa nini asichukuliwe sheria mwivi? ( Maana nchi ina sheria zote,zipo sheria za waharifu.)
Watu wa namna hii wanafanana na wale waliotaka kumpiga mawe mwanamke aliyefumaniwa uzinzi. ( Yoh.8:7-8 )
Haleluya…
Kupitia andiko letu la fundisho hili ( Yoh 8:7-9 ) tunajifunza mambo mengi,lakini machache kati ya mengi ni haya;
 Kukubali kosa kabla ya kusamehewa.
 Yesu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi.
 Panapo uovu dhamiri inaweza kukushtaki.
 hakuna hukumu tena baada ya msamaha wa dhambi.
Wenye kuhukumu makosa,wao pia ni wakosa wenye kustahili hukumu.
 Hukumu za kibinadamu hapa chini jua,utolewa kwa upendeleo.

 KUKUBALI KOSA KABLA YA KUSAMEHEWA.
~ Mwanamke aliyefumaniwa uzinzi,alijikubali kwamba amefanya kosa,ndio maana tunaona hakujibu chochote cha kujitetea mbele za Yesu. Sababu kama asingekubali kosa lake angeliweza kujitetea,lakini alikaa kimya hata akasamehewa.
~ Mara nyingi sisi tunajihesabia haki penye makosa.
~ Yeye mwenye kujihesabia haki hali ni mdhambi,hawezi kupokea msamaha wa kweli. Kwa sababu kanuni ya kusamehewa ni lazima mmoja akubali makosa yake ndipo msamaha uachiliwe na msamaha wa namna hii uwa na nguvu sana.

YESU KRISTO ANAYO AMRI DUNIANI YA KUSAMEHE DHAMBI.
Imeandikwa;
“ Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. “Luka 5:24
Hakuna mwanadamu anayepaswa kumuhukumu mwanadamu mwenzake kwa sababu ya dhambi aliyotenda sababu mwenye kuhukumu ni Mungu mwenyewe.

DHIMIRI HUSHTAKI PANAPO DHAMBI.
~Wale majamaa walishtakiwa na dhamiri zao ingawa walikuwa na lengo baya,tena na lengo la kumjaribu Bwana Yesu. Lakini mioyo yao ikawasuta.
~ Mara nyingi tutendapo makosa,dhamiri zetu hutushtaki kuwa tumekosea. Pale penye uovu ndipo dhamiri inagonga ndani yako,hivyo usikiapo hukumu ya dhamiri ndani ya moyo wako,mara moja ingia katika toba.

 HAKUNA HUKUMU YA ADHABU BAADA YA MSAMAHA.
~ Yule mwanamke alisamehewa dhambi zake,kisha biblia inasema akaenda zake,wala hatuoni tena wale majamaa wakitaka kumuhukumu maana hakuna adhabu ya dhambi tena mahali penye msamaha.
Tunasoma;“ Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. ” Warumi 8:1

 WENYE KUHUKUMU MAKOSA YA WATU,NAO NI WAKOSAJI.
~ Ile mijamaa kumbe na yenyewe yalikuwa na makosa ndio maana hakuna hata mmoja wao aliyedhubutu kumtupia jiwe yule mwanamke.
~ Leo,wapo watu wenye kuhukumu wenzao wakidhania kuwa wao wapo salama kumbe ni sawa na yale majamaa yenye dhambi.

HUKUMU ZA KIBINADAMU HUTOLEWA KIPENDELEO.
~ Siku zote mwanadamu mwenye kuhukumu wenzake hawezi kuhukumu kwa haki. Ndio maana haki haipo hata mahakamani kabisa,bali haki ipo kwake Mungu tu.
Tazama ( Yoh.8:3-11 )
Utagundua kwamba waandishi na mafarisayo walimlenga mwanamke peke yake katika lile kosa la uzinzi,utafikiri mwanamke huyo alikuwa akizini peke yake pasipo mwanaume. Sababu uzinzi hufanywa na watu wawili yaani mwanamke na mwanaume waliokubaliana kufanya dhambi hiyo.
Hivyo;
Kosa la uzinzi likawa ni la upande mmoja tu,yaani mwanamke ndio kafumaniwa, mwanaume je!!
Hii inadhihilisha kwamba hukumu za kibinadamu zimepindishwa na dhambi sababu mwenye kuhukumu naye si safi,hivyo hukumu za kibinadamu hutolewa kwa upendeleo. Mungu pekee yake ni mwenye haki asiyependelea.
Kumbuka jambo moja kwamba,
Usiizoelee dhambi,chukia dhambi na mkimbilie Bwana Yesu siku ya leo ili akusamehe dhambi zote,uokoke na kuanza maisha mapya ya wokovu.
Sikuambii ukafanye dhambi kwa sababu ipo neema ya msamaha,la hasha! Bali yakupasa kuikimbia dhambi yoyote ile,ndio maana hata Yesu alimwambia yule mwanamke usitende dhambi tena.
~ Kwa huduma ya maombi na maombezi nipigie kwa namba yangu hii;
0655~11 11 49.
UBARIKIWE.

Comments